Thursday, 30 June 2016

Rufani dhidi ya Kitilya kuanza kunguruma kesho


JALADA la kesi ya kujipatia dola za Marekani milioni sita (Sh. bilioni 1.3), inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, limetinga Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.




Kesi hiyo itaanza kusikilizwa kesho mbele ya Jaji Edson Mkasimongwa, baada ya Mahakama ya Rufani kuamuru ipangiwe jaji mwingine wa kusikiliza maombi ya Jamhuri kupinga kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha dhidi ya washtakiwa.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alikata rufani mahakamani hapo, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kupinga uamuzi wa kutupiliwa mbali rufani yao dhidi ya kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha.
Rufani hiyo ilisikilizwa na jopo la majaji watatu, Bernad Luanda, Salum Massati na Aristoclas Kaijage wa mahakama hiyo. Jopo hilo liliamuru jalada la kesi hiyo kurudishwa Mahakama Kuu na kupangiwa jaji mwingine wa kusikiliza maombi ya Jamhuri.
Mei 6, mwaka huu, Mahakama Kuu iliyokuwa imeketi chini ya Jaji Mfawidhi Mosses Mzuna, ilitupilia mbali rufani hiyo, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha pingamizi la awali kwamba rufani hiyo imewasilishwa kinyume cha sheria na kwamba itupiliwe mbali.
Aidha, mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi la upande wa utetezi kwamba haina mamlaka ya kusikiliza rufani hiyo dhidi ya washtakiwa.
Upande wa Jamhuri, uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu Timon Vitalis, akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Theophil Mutakyawa na Shadrack Kimaro.
Upande wa Utetezi uliongozwa na Dk. Ringo Tenga akisaidiwa na Majura Magafu, Steve Axwesso, Alex Mgongolwa na Godiwn Nyaisa.
Katika maombi ya msingi, upande wa Jamhuri umewasilisha hoja zao kupinga uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Emmilius Mchauru, kulifuta shtaka la utakatishaji fedha haramu dhidi ya washtakiwa.
Hoja ya nyingine, Hakimu Mchauru alikosea kusema hati ya mashtaka ina dosari wakati siyo kweli.
Hoja ya tatu, upande wa Jamhuri unaeleza kwamba uliomba nafasi kwa kuwa kifungu cha 234 kidogo cha (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hakimpi hakimu madaraka ya kuuruhusu kubadilisha hati kama kweli mahakama iliona ina dosari za kisheria.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wote wako rumande ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996 na meneja Mwandamizi wa benki ya Stanbic, Shose Sinare na mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili Mosi, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka manane, likiwamo la kutakatisha fedha dola za Marekani milioni sita, mali ya serikali

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!