Monday, 20 June 2016

Nduna Songea Mbano shujaa kabila la Wangoni


HUWEZI kusimulia historia ya vita ya Majimaji bila kumtaja shujaa wa kabila la Wangoni Nduna Songea Mbano. Jina lake limepewa hadhi kwa kuuita mji wa Songea. Awali mji huo ulijulikana kwa jina la Ndonde hadi mwaka 1906. Songea alikuwa ni miongoni mwa wasaidizi ( Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la Wangoni (Nkosi) Chifu Mputa bin Gwezerapasi Gama.


Wasaidizi wengine walikuwa ni Mgendera Mawaso Gama, Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba Mbano, Mtekateka Muyamuya Tawete, Fratela Fusi Gama. Wengine ni Maji ya kuhanga Komba, Zimanimoto Gama, Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna Mkomanile ambaye alikuwa ni mwanamke pekee katika kundi hilo.
Nduna Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake. Chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea katika kuwaongoza manduna wenzake na wapiganaji wa vita ya Majimaji kiujumla. Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Maji Maji Songea, Philipo Maligissu anasema, sifa kubwa zilizompa umaarufu Nduna Songea Mbano ni weledi wake katika kuandaa mikakati ya kivita, na misimamo isiyotetereka katika kusimamia uamuzi anaofanya.
Maligissu anasema katika viwanja vya makumbusho hayo kuwa, Songea Mbano alikuwa maarufu ukilinganisha na wenzake 11. Mbano aliweza kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo hilo ulianza kujitokeza Julai 12 mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani kwa Mkuu wa Wilaya wa Wajerumani Luteni Engelhardt.
Maligissu anasema, kwa rekodi zinaonesha kuwa tarehe hiyo Nduna Songea Mbano alionekana kuwa ni mtu wa kipekee katika idadi ya manduna 11 kwa kitendo chake cha kukataa tamko la utawala mpya wa Wajerumani la kutaka Wangoni wakomeshe biashara ya utumwa. Siku hiyo ilikuwa ni siku rasmi kwa utawala wa kikoloni kuanzishwa katika mji wa Songea chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la Kijerumani ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Jeshi kwa kanda ya Kusini.
Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao katika maeneo ya ukanda wa kusini walikutana na upinzani kutoka tawala za Kiafrika hususani za Wangoni. Maligissu anasema, Wangoni walikuwa na tabia ya kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na kuwapeleka Songea kuwafanyisha kazi katika maeneo yao ya utawala.
Tabia hiyo ya Wangoni iliwachukiza Wajerumani kwa kuwa wageni hao walikuwa wanaheshimu makubaliano yaliyofikiwa kutoka kwenye mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885. Katika mkutano huo moja ya makubaliano ilikuwa ni pamoja na kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima likomeshe biashara ya utumwa.
Wajerumani walikuwa wamejiimarisha katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Walipofika Ruvuma wakatoa tamko kwa Wangoni hawaruhusiwi na hawataruhusiwa tena kwenda Lindi, Mtwara na maeneo mengine kuchukua mateka na kwamba mateka wote waliokuwa chini ya himaya ya Wangoni waachiwe huru. Baada ya Wajerumani kutoa tamko hilo Nduna Songea Mbano alijitokeza akapinga agizo hilo.
Nduna Songea Mbano alisema, utawala wa kabila la Wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na kwamba msimamo wao ni kutoutambua utawala wa Kijerumani na hivyo hautatekeleza agizo la wageni hao. Anasema, tamko la Wajerumani lina lengo la kudhoofisha utawala wa Machifu na Manduna katika maeneo yao kwa kuwa walifuata kanuni zao za kimila na kitamaduni.
Kutokana na msimamo huo, Wajerumani walimuona Mbano kuwa ni mtu hatari katika utawala wao hivyo wakaanza kufuatilia nyendo zake kwa sababu alionekana ni kiongozi shupavu, mwenye misimamo mikali na anayezingatia heshima na utu wa kabila lake. Alionekana ni mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yoyote kwa kushirikiana na wananchi ambao walikuwa wanamheshimu na kumsikiliza.
Maligissu anasema, Mbano alikuwa na uwezo wa kuwaunganisha wananchi na kuwa na umoja, upendo na mshikamano na kwamba alikuwa akiwaelekeza jambo walilifanya kwa umakini na kwa ukamilifu. Anasema, kuanzia hapo Nduna Songea Mbano aliendelea kujizolea umaarufu baada ya kutamka kuwa yupo tayari kwa lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za Kiafrika zinadharauliwa na wakoloni.
Waliamua kuwaalika Machifu na Manduna wote Julai 13 mwaka 1897 Bomani kwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza katika nchi ya Ungoni na kuwaeleza kuwa mtu yeyote katika eneo atakayekaidi amri yoyote kutoka kwa uongozi wa Wajerumani atapigwa risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha. Siku hiyo hiyo Machifu na Manduna walichukuliwa hadi juu ya mlima wa shabaha wa Chandamari uliopo katikati ya mji wa Songea na kuonyeshwa nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi katika mwili wa binadamu.
Lengo la Wajerumani kufanya hivyo ni kuwaonesha wenyeji kwamba, silaha jadi na za kimila za Wangoni haziwezi kushindana na nguvu ya risasi. Licha ya Wajerumani kutoa vitisho, Mbano aliendelea kushikilia msimamo wa awali wa kuchukia utawala huo wa wageni, aliwatetea Waafrika hadi ilipotokea vita ya Majimaji. Mbano anatoa ushindani mkubwa katika vita hiyo na kuonesha ustadi kwenye mapigano.
Katika sehemu zote ambazo Wajerumani walipigana wameandika kuwa hawakupata ushindi mkubwa kama waliopata katika mkoa wa Ruvuma zamani nchi ya Ungoni. Viongozi wao Wangoni hawakuwa wanafiki, walijitoa kusaka ukombozi wa kweli na hadhi ya tamaduni zao. Idadi ya watu wengi walionyongwa katika historia ya nchi yetu walitoka katika himaya ya Nduna Songea Mbano na ushahidi upo wazi kuwa watu 67 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa akiwemo yeye.
Katika kuonesha kuwa Mbano alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa weledi bila kusaliti dhamira yake kuanzia mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi la kupambana na utawala wa Wajerumani. Akaanza kuchukua watu na kuwapeleka juu ya mlima wa Chandamari, alifanya nao mkutano na kutoa mafunzo ya kivita na kuwaelekeza kwa nini wanawachukia Wajerumani.
Katika mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina madhara ya kuukubali utawala wa Wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi wake ya kuwaondoa wageni hao. Anawaeleza wananchi kuwa, eneo hilo ni lao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya utawala wao sasa inakuwaje waletewe watawala mpya wakati hawauhitaji. Chokochoko hizo zilizaa vita ya Majimaji, na wakati mapigano yakiendelea Wajerumani walianza kumtafuta Mbano ili wamkamate na kufanya naye mazungumzo ya maridhiano.
Wakati huo Mbano alikuwa amejificha kwenye pango lililopo kwenye mlima wa Chandamari na usiku hukutana na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita. Maligissu anasema, Mbano alikuwa anaishi na ndugu zake katika eneo la Mateka katika Manispaa ya Songea. Kwa mujibu wa Maligissu, wakati wa vita Mbano alikuwa anajificha katika pango hilo ili Wajerumani wasimkamate mpaka atakapotimiza malengo yake.
Wajerumani walipoona wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na vita hiyo waliamua kuwakamata ndugu, jamaa na wafamilia ya Mbano. Miongoni wa waliokamatwa ni Chifu Mputa Gama na manduna wengine. Walifungwa gerezani kwa lengo la kumdhoofisha Mbano ili abadili msimamo na akubaliane na matakwa ya Wajerumani.
Baada ya Wajerumani kufanya hivyo, Mbano alipata taarifa na akaamua kutoka kwenye pango hilo na kwenda kwa wageni hao kutaka watu wake waachiwe ili mapigano yaendelee. Wajerumani walimkamata, akawekwa gerezani. Utawala wa Wajerumani waliamua kuwa hukumu kwa wafugwa hao akiwemo chifu wa kabila la Wangoni ni kunyogwa hadi kufa.
Wafungwa hao waliamuliwa kuchimba shimo kubwa bila kujua kuwa shimo hilo ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao. Ilipofika siku ya kutekeleza hukumu walinyongwa kwa zamu kwa siku mbili. Maiti 66 waliwekwa kwenye kaburi hilo, walizikwa kwa pamoja. Nduna Songea Mbano walimuacha ili aweze kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi kwa kuwa waliamini kuwa yeye ni kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na kusikilizwa.
Tangu siku hiyo alipoachwa bila kunyongwa Mbano aliwasumbua Wajerumani kwa kuwashinikiza wamnyonge kama walivyowafanyia ndugu zake kwa maelezo kwamba haoni sababu ya yeye kuishi wakati wenzake wamekufa. Mbano anawaeleza Wajerumani kuwa kama hawataki kumnyonga hataki kula wala kunywa chochote mpaka afe.
Wajerumani walisikiliza hoja za Mbano, wakaamua kumnyonga na kumzika katika kaburi la pekee yake wakiamini kuwa ni mtu wa pekee mwenye ushujaa, uamuzi madhubuti na misimamo isiyoyumba. Walimuenzi kwa kubadili jina la mji wa Ndonde na kuuita jina la Songea na hadi sasa mji huo unafahamika hivyo ukiwa na hazina kubwa ya historia na utalii wa kitamaduni.
Kila mmoja wetu hana budi kujiuliza ni mafundisho gano anaweza kuyapata katika historia ya nchi yetu na mchango mkubwa alioutoa Nduna Songea Mbano. Kizazi cha sasa kinapaswa kujiuliza kama kina moyo wa ushujaa kama wa Mbano, uzalendo heshima na usawa kama ilivyo kuwa kwa mababu zetu. Tanzania ni nchi yetu, kila mmoja atimize wajibu kwa kuwa mzalendo ili kizazi cha sasa na vijavyo vifaidi matunda ya uhuru.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!