Speciosa Silvevesta akionesha mwili wake wenye makovu kutokana na kumwagiwa tindikali na mumewe.
Na Waandishi Wetu, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mwanadada Speciosa Silvevesta (33) anaugulia maumivu makali kufuatia madai yake kwamba, alimwagiwa tindikakli na mume wake aliyemtaja kwa jina la Richard Majega huku mwanaume huyo naye akikanusha vikali na kutoa ufafanuzi mzito, Uwazi lina kila kitu.
Akisimulia mkasa mzima kwa Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar ambako amefikia akisaka matibabu, Speciosa alisema tukio hilo lilimkumba mwaka jana akiwa jijini Mwanza.
“Awali nilikuwa nikiishi Shinyanga na mume wangu na tulifanikiwa kujenga chuo lakini siku ambayo alinimwagia tindikali nilikuwa Mwanza ambapo nilihamishia makazi yangu kutoka Shinyanga baada ya kushindwana na mume wangu.
“Niliamua kumwachia shule ambayo tuliijenga wote na magari nane nikaenda kuishi Mwanza na kuanzisha maisha na watoto wangu niliowazaa na mwanaume mwingine.
Speciosa Silvevesta kabla hajamwagiwa tindikali.
“Siku moja alikuja Mwanza mpaka nilipokuwa nafanyia kazi, nikamkaribisha. Wakati wa kuondoka ulipofika nilifunga biashara, akasema anataka kwenda kuwaona watoto, nikampeleka.
“Kesho yake akaja tena, akaniambia nirudi Shinyanga nikamwambia siwezi, nimechoka,” alisema mwanamke huyo.
Akiendelea kusimulia mkasa wake, mwanamke huyo aliyedai kuishi na mumewe kwa miaka 10, alisema:
“Siku moja alikuja tena kwenye biashara yangu, akanikuta naumwa, nikafunga duka mapema tukaondoka wote. Kufika njiani akasema anipeleke akaninunulie chakula, lakini nilikataa.
“Ghafla alitokea kijana mmoja akanimwagia maji kama ya moto machoni kisha yakashuka chini huku nikisikia maumivu makali, nikawa namuita mume wangu, hukuitika lakini mara nikamsikia akisema; ‘wana mapanga.’ Na yeye akakimbia.
Mwanamke huyo anasema baadaye mume wake alimsaidia kumpeleka Hospitali ya Bugando kulekule Mwanza halafu Hospitali ya Taifa, Muhimbili jijini Dar kwa matibabu ya upasuaji.
“Nilikuja Dar na huyohuyo mume wangu, tukafikia gesti. Lakini siku moja kabla ya kwenda kufanyiwa upasuaji tukiwa tumelala aliniuliza swali kwamba, iwapo nitamfahamu mtu aliyenimwagia tindikali nitamfanya nini? Nikamwambia nimeshamsamehe huyo mtu.
“Baada ya matibabu ya Dar nilirudi nyumbani, Kahama (Shinyanga) kuwapa taarifa ndugu kuwa nilimwagiwa tindikali na niliwaambia wanangu kuwa siyo baba yao aliyenimwagia tindikali.
“Baadaye nilitakiwa nirudi Muhimbili kufanyiwa upasuaji mwingine, nikawa na mume wangu kama awali. Tukiwa gesti aliniuliza tena kwamba, nikimjua aliyenimwagia tindikali nitamfanyeje? Nikamwambia nilisema nimemsamehe, akaniambia ‘ni mimi ndiyo nilikumwagia tindikali kwa kuwa nilikuwa nataka urudi nyumbani ukawa hutaki.’
“Nililia sana mpaka nikashindwa kufanyiwa upasuaji kwa kuwa presha ikawa juu. Niliogopa kumwambia daktari lakini baadaye nikafanyiwa hivyohivyo, niliporudi nyumbani nilikuwa kama naweweseka, sikwenda kumshtaki popote,” alisimulia mwanamke huyo.
Alisema: Kwa sasa niko tena Dar, nahitaji msaada, nawaomba Watanzania wenzangu wanisaidie nipate matibabu kwa sababu hospitali wanahitaji shilingi milioni 6 na mimi sina. Kama unavyoniona, sioni sawasawa, ngozi usoni hadi kwenye kifua imechunika, imevimba, napata maumivu makali sana.”
Kutoa wala si utajiri ni moyo tu wa kuguswa. Kama umeguswa na yaliyomkuta dada huyo, msaidie kwa namna yoyote ile ukitumia namba ya simu: 0713 535 549.
MUME NAYE AFUNGUKA MAZITO
Hata hivyo, ukiachana na madai ya mwanamke huyo, Uwazi lilifuata maadili ya taaluma ya habari kwa kumtafuta Majega ili ajibu madai ya mkewe.
Naye alisema si kweli kwamba alimmwagia mkewe tindikali bali ni yeye aliyemhudumia baada ya tukio na kutumia zaidi ya shilingi milioni 30 kwa matibabu.
“Siku ya tukio Januari 5, mwaka jana kuna mtu tulikutana naye akammwagia tindikali nami ilinipata pajani. Lakini nilijitahidi sana kumgharamia matibabu pale Bugando.
“Iliposhindikana nikaomba rufaa, tukahamishiwa Muhimbili ambako alilazwa. Kutokana na joto kwenye wodi ilibidi ninunue Noah iwe kama wodi yake kwani alikuwa akishinda humo akitumia kiyoyozi cha gari ndipo alikuwa akipata usingizi.
“Kifupi ni kwamba kuna ndugu zake (majina yanahifadhiwa ndiyo walimtia maneno kuwa eti mimi ndiye niliyemmwagia wakati siyo kweli kabisa. Mwandishi, inaingia akilini mtu afanye kitendo kama hicho kisha amwambie aliyetendewa? Ningekuwa na haja gani ya kumhangaikia?
“Nampa ushauri wa bure kwamba kwenda kwenye vyombo vya habari haisaidii kwa sababu mahakama na polisi wanajua kila kitu kuhusu mfarakano wetu. Arudi tu kwangu aite viongozi wa kanisa akiri mbele yao kwamba amenikosea tena mbaya zaidi kwa kunisingizia jambo hilo zito, ananichafua bure.
“Mimi nitamsamehe nitampa nyumba moja aishi na kumhudumia japokuwa ndoa imeshaharibika lakini nimezaa naye, sina haja ya kueleza yale aliyoyafanya kwangu kwa sababu tumeshafanya vikao vingi na viongozi wa dini na kusuluhishwa.”
No comments:
Post a Comment