POLISI mkoani Kilimanjaro inawashikilia watu 13, akiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Karansi, Wilaya ya Siha, kwa madai ya kutekeleza amri ya wazee wa mila ya kumcharaza bakora na kumsababishia kifo, Abedi Akyoo (53), aliyetuhumiwa kuiba kuku.





Akyoo, anadaiwa kuchapwa zaidi ya viboko 70 na kundi la vijana wa rika wa kabila la Wameru, baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho, aliyetajwa kwa jina la Augusti Kawau (49), kudaiwa kutoa amri ya kushughulikiwa kutokana na tuhuma za wizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha mauaji hayo kutokea katika eneo la Miti Mirefu, majira ya saa 11:30 jioni ya Juni 21, mwaka huu.
“Ni kweli tumewakamata wananchi 13 wa vijiji vya Karansi na Kandashi, Wilaya ya Siha kwa kusababisha mauaji ya Abedi Akyoo, aliyetuhumiwa kuiba kuku," alisema Mutafungwa.
"Huyu aliuawa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wanaodai kusimamia mila wa kabila la Wameru. Pia bado kuna watu tunawatafuta kutokana na mauaji haya.”
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufani ya Taifa ya Magonjwa ya Kifua Kikuu (Kibong’oto), alisema.
Kamanda huyo aliiambia Nipashe kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo na itakapokamilisha kazi hiyo, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio, zinaeleza kuwa Akyoo alichapwa viboko hivyo na watu wanaodaiwa kusimamia mila wa kabila la Wameru na viongozi wa mila wa jamii ya wafugaji wa Kimasai baada ya kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya wizi wa kuku katika kijiji hicho.
Kwa mujibu wa majirani (majina yamehifadhiwa), wazee hao walihisi Akyoo alikuwa akijihusisha na wizi huo, ndipo walipomchukua na kumpeleka porini na kumcharaza viboko kwa mujibu wa sheria za kimila.
Wanaoshikiliwa pamoja na Kawau ni Daniel Isaya (20), Isack Kanaeli (29), Lengai Lengosi (28), Richard Noe (30) Josephati Ngoipa (29), Kanaeli Ayubu (34) na Abiaza Elipokea (38).
Wengine ni Bahati Naksi (32), Ayubu Kanangira (65), John Sokoine (61), Josephat Lomnyaki (61) Andrea Kanangira (49) na John Mshiu (52).
Mbali na sheria ya kuwashughulikia wezi kuchapwa viboko, Mei 12, mwaka huu, zaidi ya wakazi 200 wa Kata ya Karansi wilayani humo, wakiwa katika mkutano uliondaliwa na wazee wa mila wa Kimeru, walipitisha uamuzi wa kuchapwa viboko 60 hadi 70 wanaume watakaovaa suruali chini ya kiuno na wanawake watakaokutwa wamevaa sketi fupi.