Mwandishi wetu, Amani
DAR ES SALAAM: Majozi! Kifo cha Profesa Iddi Suleiman Nyangarika Mkilaha (60) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilichodaiwa kilitokana na kujipiga risasi wakati akisafisha bastola bafuni, kimeacha maswali 5 kwa baadhi ya watu, Amani limechimba.
Tukio hilo la kusikitisha lilijiri Juni 25, mwaka huu, nyumbani kwake, Boko Basihaya jijini Dar muda mfupi baada ya kurejea kutoka safarini kikazi mjini Dodoma.
Gazeti la Amani lilishiriki mazishi ya marehemu huyo yaliyofanyika jijini Dar ambapo baadhi ya waombolezaji walisikika wakijiuliza maswali hayo lakini bila majibu.
SWALI LA KWANZA
“Kama kweli marehemu alijipiga risasi akiwa bafuni ni nini kilimsukuma kuingia huko na silaha hiyo, sehemu ambayo inajulikana hutumika kwa kuogea tu?” alihoji mwombolezaji mmoja.
SWALI LA PILI
“Hili linashangaza sana. Mtu kama profesa unataka kuniambia alikuwa hajui taratibu na usafishaji salama wa silaha? Au ndiyo vile tena, siku ikifika,” alisikika mwombolezaji mwingine.
SWALI LA TATU
“Baada ya kusikika mlio wa bastola ambao haujulikani ni wa kujipiga au kupigwa, nani alikuwa wa kwanza kusikia mlio wa risasi? Na wakati anaingia bafuni, familia yake ilikuwa wapi, sebuleni au haikuwepo nyumbani?” swali hili liliulizwa na mwombolezi wa kwanza.
SWALI LA NNE
“Je, ilikuwa kawaida ya profesa kwenda kusafishia silaha yake bafuni? Kama ndiyo ni nani alimuaga wakati anakwenda kufanya zoezi hilo?” aliuliza mwingine.
Baadhi ya waombolezaji kutoka nyumbani kuelekea makaburini, walikwenda mbele zaidi kwa kulitaka jeshi la polisi kutamka neno moja juu ya kifo cha profesa huyo, kwamba kama kweli alijipiga risasi ilikuwa kwa lengo la kujiua au kwa bahati mbaya?
FAMILIA YAJIFUMBA MDOMO
Hata hivyo, mmoja wa wanandugu alipoulizwa na gazeti hili undani wa kifo cha profesa alisema hilo ni fumbo ambalo polisi bado hawajatoa taarifa na hata wao kama ndugu bado wako gizani.
“Sina cha kuzungumza zaidi ya kile ambacho umekisikia na hata mimi najua hivyo, ninachoamini anayejua ukweli wa kilichotokea ni marehemu na Mungu mwenyewe,” alisema ndugu huyo bila kutaja jina lake akisema hakuona sababu ya kufanya hivyo.
Naye msemaji wa familia hiyo, Nurdin Mkilaha alisema kuwa, familia inachojua siku ya marehemu ilifika likatokea la kutokea, hakuna lingine na kama kuna siri ya kifo chake, anajua mwenyewe na Mungu!
WAFANYAKAZI CHUO KIKUU WANENA
Aidha, baadhi ya wafanyakazi wa chuo kikuu ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao, waliliomba jeshi la polisi kitengo cha intelijensia kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa kifo cha mfanyakazi mwenzao.
JESHI LA POLISI
Mpaka juzi, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema kuwa, bado wanachunguza juu ya kifo hicho na kusema jeshi lake linaangalia kama kuna mambo yalimuumiza marehemu mpaka kuchukua hatua hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, CP Christopher Fuime yeye alisema, marehemu alikutwa bafuni kwake akiwa amejipiga risasi sehemu ya juu ya mwili.
Mwili wa Profesa Mkilaha ulizikwa Juni, 27 mwaka huu kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar na kuhudhuriwa na baadhi ya maprofesa na wanavyuo mbalimbali. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako naye alishiriki maziko ya marehemu huyo.
No comments:
Post a Comment