Thursday, 23 June 2016

MAGUFULI AIBUA AKAUNTI ZA WIZI


  • Ashitukia tri. 5.5 za miamala ya simu bila kodi
  • Ataka NMB irudishe bil. 7/- kiinua mgongo hewa
  • Ashauri riba za mikopo kwenye mabenki ziwe nafuu
  • Ataka BOT idhibiti kushuka kwa thamani ya Sh.
RAIS John Magufuli, ametoa maagizo tisa kwa Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ametaka kutekelezwa haraka likiwamo la kuiagiza benki ya NMB kurudisha mara moja Sh. bilioni saba walizowalipa wafanyakazi hewa 2,800 kama mafao ya kustaafu.







Aidha, Rais Magufuli alisema idadi ya wafanyakazi hewa kwa sasa imefikia 12,446 na kuagiza kusitishwa ajira serikalini na promosheni kwa wafanyakazi kwa muda wa mwezi mmoja hadi kazi ya kubaini wafanyakazi hewa itakapokamilika.
Pia amezitaka Wizara ya Fedha na BoT, kuyabana maduka ya kubadilishia fedha za kigeni.
Rais Magufli alisema hayo jana jijini Dar es Saalam wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya BoT. Benki Kuu ilianzishwa Juni 14, 1966.
Rais Magufuli alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili BoT ambazo zinapaswa kutatuliwa haraka.
Alisema BoT na Wizara ya Fedha zinapaswa kuhakikisha taasisi za kifedha na benki zinawafikia wakazi wa vijijini kuliko walioko kujiwekeza vijijini.
Alisema BoT na Wizara ya Fedha zinapaswa kushughulikia tatizo la kuwapo kwa riba kubwa katika benki kunakosababisha wajasiriamali wadogowadogo kushindwa kwenda kukopa.
Alisema benki nyingi nchini zimekuwa na tabia ya kufanya biashara ya kukopeshana na serikali na kuwakandamiza wajasiriamali kwa kuwawekea riba kubwa.
“Kuna wajasiriamali wadogo wadogo wanashindwa kwenda kukopa benki kutokana na kuwapo kwa riba kubwa, hata walioweza kukopa wanashindwa kulipa kutokana na riba kuwa kubwa, hivyo ninawaagiza mtatue tatizo hili,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, BoT na Wizara ya Fedha, alisema, zinapaswa kulinda thamani ya shilingi ambayo inaporomoka sana.
Alisema nchi yoyote duniani inataka kulinda thamani ya fedha yake, hivyo BoT inapaswa kushirikiana na vyombo vingine kuhakikisha thamani ya shilingi haishuki.
Alisema suala la kudhibiti shilingi kutokushuka limekuwa likipigiwa kelele miaka mingi lakini utekelezaji wake unashindwa, hivyo Rais Magufuli alimtaka Gavana Mkuu wa BoT, Profesa Benno Ndulu kutekeleza suala hilo.
Alisema endapo suala hilo litafanikiwa, hata suala la utakatishaji fedha nalo litafanikiwa.
Rais Magufuli pia aliagiza kulindwa kwa usalama na ubora wa huduma katika kutuma na kupokea fedha katika mitandao ya simu kwa wananchi.
Rais Magufuli alisema hadi kufikia Machi mwaka huu Sh. trilioni 5.5 zilitumwa kwa njia ya simu katika kampuni za simu, na akamtaka Prof. Ndulu kuhakikisha serikali nayo inanufaika na huduma hiyo kwa kupata kodi.
“Mshirikiane na TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano) katika kufanikisha hilo,” alisema Rais Magufuli kwa sababu "ni lazima serikali inufaike na huduma hiyo.”
“BoT mnapaswa kujipanga, bila ya kufanya hivyo tutaishia kuwa wasindikizaji.”
Rais Magufuli pia aliitaka BoT na Wizara ya Fedha kufanya usimamizi katika vyombo vingine vya fedha.
Alisema maduka ya kubadilishia fedha za kigeni yanapaswa kusimamiwa vizuri kwani hutumiwa sana katika utakatishaji wa fedha.

Alisema kushuka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi 5.2 za sasa kuendane na uhalisia wa maisha ya watanzania.
Rais pia alizitaka BoT na Wizara ya Fedha kushirikiana vizuri kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kutoka katika kampuni za uchimbaji madini na kampuni za simu.
Alisema tabia ya kampuni za uchimbaji madini kulalamika kila mwaka kuwa zinapata hasara isijitokeze tena, hivyo serikali ikusanye kodi sawasawa.
“Kila siku yanalalamika yanapata hasara, kila mwaka, hivyo ni visingizio ili yasilipe kodi, kama wanapata hasara waondoke, kwa nini wanaendelea kung’ang’ania nchini?" aliuliza.
“Ni mara kumi tukose makampuni ya kuchimba lakini madini yetu yanabaki, watayakuta watoto wetu.”
Pia Rais Magufuli aliagiza BoT na Wizara ya Fedha kuwa na akaunti moja ya kuhifadhia fedha zote za serikali (single treasury account) ili kuondokana na kuwapo kwa ulipaji wa hundi hewa.
Alisema ni jambo la ajabu kwa Tanzania kushindwa kuwa na akaunti hiyo wakati nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Rwanda, Uganda na Kenya wameweza.
Rais Magufuli pia aliagiza BoT na Wizara ya Fedha kuangalia upya akaunti zenye fedha lakini ambazo hazijatumiwa kwa muda mrefu.
Alisema amebaini kuna akaunti nyingi za fedha ambazo zina fedha za Serikali na zimekaa kwa miaka mingi zikiwa na fedha ambazo zinatumika kutoroshea fedha kwenda nje ya nchi.
“Sitaki kuzitaja akaunti hizo, nyie wenyewe mnazijua, kuna moja niliikuta ikiwa na Sh. Bilioni 23 imekaa kwa zaidi ya miaka 10 na walitaka kuitumia kutoroshea fedha kwenda nje, sasa ninawaagiza mkazifunge,” alisema Magufuli.
Rais Magufuli alitoa agizo lingine kwa BoT na Wizara ya Fedha ambalo ni kuhakikisha mabenki na taasisi za benki ambazo zinakiuka masharti, pamoja na benki za serikali zinazojiendesha kwa hasara zichukuliwe hatua mara moja.
Rais Magufuli alitolea mfano wa benki ya Twiga Bancorp ambayo iliwahi kupata hasara ya Sh. Bilioni 18.
Alisema katika utawala wake, hataibembeleza benki yoyote ambayo haitafanya vizuri.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuna taasisi za kifedha na benki za serikali ambazo zilianzishwa kupitia BoT lakini hadi leo hazijulikani zinamilikiwa na nani na ziko wapi.
Aliagiza zichukuliwe hatua mara moja, akitolea mfano wa Pride.
WAFANYAKAZI HEWA
Rais Magufuli alisema idadi ya wafanyakazi hewa nchini imezidi kuongezeka, na kwamba hadi kufikia jana walikuwa 12,446.
Alisema kutokana na kuwapo kwa idadi hiyo, zaidi ya wafanyakazi hewa 2,800 walilipwa Sh. bilioni saba kama mafao ya kustaafu na benki ya NMB.
Alisema kutokana na malipo hayo, ameiagiza Wizara ya Fedha na benki ya NMB kuzirudisha fedha hizo mara moja.
Rais Magufuli alisema kutokana na kukithiri kwa tatizo la wafanyakazi hewa, ameagiza Utumishi kusitisha kuajiri wafanyakazi wapya kwa muda wa mwezi mmoja hadi pale kazi ya kuhakiki watumishi hewa itakapomalizika.
“Nimeishangaa sana Hazina," alisema Rais Magufuli. "Wakati tunapambana na kuwaondoa watumishi hewa wao wanaendelea na kuajiri watumishi wengine, sasa nimeagiza kazi hiyo isimame.
Rais Magufuli alisema mbali na kusitisha ajira zote serikalini, pia ameagiza kusimamishwa kwa promosheni za wafanyakazi serikalini kwa mwezi moja hadi kazi ya kuhakiki wafanyazi hewa litakapokamilika.
Alisema serikali inatumia zaidi ya Sh.bilioni 577 kila mwezi kulipa mishahara ya wafanyakazi, hivyo kufanya fedha inayobakia kwa ajili ya maendeleo kuwa kidogo.
Alisema tatizo la wafanyakazi hewa na ulipwaji wa mafao hewa kwa watumishi wa serikali ni ugonjwa mkubwa unaoweza kufananishwa na saratani nchini.
Rais Magufuli Machi 15, mwaka huu wakati akiwaapisha wakuu wapya wa mikoa jijini Dar es Salaam alitoa agizo kwa wakuu wote wa mikoa kwa kuwapa siku 15 kuhakikisha wanawabaini wafanyakazi hewa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!