Saturday, 4 June 2016

GIZA NENE LATANDA WALIOCHINJWA TANGA



WAKATI Polisi mkoani Tanga wamedai kufanya msako mkali, kuna hali ya sintofahamu kufuatia mauaji ya kuchinja watu wanane kwenye eneo la Kibatini mkoani humu Jumanne iliyopita,




Ambapo wahusika wa mauaji hayo wakiwa hawajajulikana huku serikali na vyombo vya dola vikiwa kimya kutoa undani wa suala hilo.
Viongozi wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama walikuwa na kikao kizito mjini Tanga juzi, lakini waliondoka kurejea Dar es Salaam bila kutaka kuingia kwa undani juu ya uhalifu huo au wahusika.
Polisi wa Tanga walisema jana msako wa kutafuta wahusika wa mauaji hayo ulikuwa unaendelea ukishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuahidi kutoa taarifa kamili watuhumiwa wakikamatwa.
Katika uhalifu ambao vyombo vya usalama havijaweka wazi kama ni ujambazi au ugaidi, watu wanane walichinjwa na watu wasiojulikana, ambao walikuwa wanadaiwa kulipa kisasi cha vijana wao kukamatwa na polisi wiki moja iliyopita kwenye eneo la Kibatini mkoani Tanga.
Watu waliouawa ni pamoja na Mjumbe wa serikali ya kijiji, Issa Hussein (50), Mkola Hussein (40), Hamisi Issa (20) na Mikidadi Hassan (70).
Wengine waliouawa ni raia wa Kenya aliyefahamika kwa jina moja tu la Mahmoud anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40, Issa Ramadhani (25) na wachunga ng'ombe wawili waliofahamika kwa jina moja moja tu la Kadiri na Salum.
Tukio hilo la mauaji ya kuchinja lilikuwa la tatu kutokea nchini katika kipindi cha uliopita baada ya Mei 25, 201, Aneth Msuya (30) kuchinjwa na watu wasiojulikana katika eneo la Kigamboni, Dar es Salaam na pia Mei 19, 2016 na watu watatu walichinjwa katika msikiti wa mtaa wa Utemini wilayani Nyamagana, Mwanza.
Matukio hayo yameongeza hofu nchini kutokana na usalama wananchi kutishiwa kufuatia kuibuka kwa wimbi hilo la watu kuuawa kwa kuchinjwa bila ya wahusika kukamatwa.
Kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na taarifa za kuwapo kwa magaidi kwenye mapango ya Amboni yaliyopo mkoani humu.
Pia Mei 8, mwaka huu, kuna kundi la vijana wa Kitanzania waliodai wanaishi jijini Tanga walikuwa wamesambaza mkanda wa video kwenye mitandao ya kijamii wakiahidi kuanzisha mashambulizi ya kigaidi nchini.
Wakuu wa ulinzi na usalama waliokutana na kuondoka Tanga ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu, waliongoza kikao cha viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Viongozi hao ambao pia walihudhuria mazishi yaliyofanyika kwenye makaburi ya Mzizima mkoani Tanga na kusisitiza uchunguzi wa kusaka wahalifu hao ulikuwa unaendelea.
Hata hivyo, viongozi hao waliondoka na siri moyoni kutokana na kutotaka kufafanua chanzo na wahusika wakuu wa mauaji hayo ya kuchinja.
Polisi Tanga wasisitiza kuendelea na msako
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Leonard Paulo, alisema jana kuwa wanaendelea na msako katika eneo hilo na kwamba hawataondoka mpaka watakapokamilisha na kujiridhisha kwamba hali ya amani imerejea kwenye eneo hilo la Kibatini.
“Baada ya mazishi askari hawakuondoka bali walikuwa wakizungukia maeneo hayo hivyo wananchi wasiwe na hofu kwamba wameachwa peke yao,”aliongeza Kamanda Paulo.
Wakazi wa eneo la mauaji wazidi kuhama
WAKAZI wa mtaa wa Mleni eneo la Kibatini Jijini Tanga kulikotokea mauaji wanazidi kuyahama makazi yao kutokana na kugubikwa na hofu.
Tangu kutokea kwa mauaji hayo watu wamekuwa wakikimbia maeneo hayo na jana wananchi walikuwa wakivunja nyumba zao na kutoa vyombo nje na kuvipakia kwenye magari tayari kwa kuhamia eneo la Kona Z lililopo kilometa takriban 30 kutoka makazi ya awali kwa hofu ya kuuawa.
Wakizungumza na Nipashe kwenye eneo la tukio baadhi ya wananchi hao wameeleza kuwa walilazimika kuyahama makazi yao kutokana na hali ya usalama kwenye maeneo hayo kutoimarishwa na hivyo kuhofia kutokea tena kwa
tukio la kuchinjwa.

Mkazi wa eneo hilo, Bistida Augustine, alisema eneo hilo siyo salama kutokana na wasiwasi wa kutokuwapo kwa ulinzi madhubuti.
Naye Mei King, alidai kuwa wameona ni muhimu kuhama kwani watu waliofanya uhalifu huo wanaweza kurudi tena kwani walikuwa wanafuatilia watoto wao waliokamatwa na polisi.
“Ni bora kwenda kuishi chini ya miti badala ya kuishi ndani ya nyumba hizo baada ya ndugu zetu kuuliwa kinyama,” aliongeza Mei.
Mbunge wa Jimbo la Tanga, Mussa Mbaruku (CUF) na Naibu meya wa Jiji hilo, Mohamed Haniu, ambao walitoa usafiri wa lori, walikuwepo wakati wakazi hao wakihama na kueleza wanakubaliana na sababu zao za kutokana na tishio la usalama.
TISHIO LA IS
Kundi la watu waliojiita kuwa wapiganaji wa Kiislamu waliweka video mtandaoni wakidai kuwepo nchini Tanzania hivi karibuni.

Tovuti ya Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) ilikuwa na video hiyo, Mei 18, mwaka huu, ambayo ilionyesha watu hao wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa vitambaa.
Ukurasa wa Twitter ambao unasambaza video hiyo ya dakika tano unasema wanaume hao ni tawi la Afrika Mashariki la kundi linalojiita Dola ya Kiislamu au Islamic State (IS).
Alipoulizwa juu ya tishio hilo, Kamanda Paulo alikataa kuzungumzia suala la mkanda huo wa video na kushikilia msimamo wake kuwa kwa sasa wanaendelea na msako wa wahalifu hao.
Imeandikwa na Lulu George na Dege Masoli, Tanga

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!