Watoto wa familia hiyo ambao ni viziwi, hawaongei na wanatembea kwa kusota.
– Watoto wanne ni viziwi, hawaongei, wanatembea kwa kusota, mama yao akatwa mguu
Na Imelda Mtema, UWAZI
DAR ES SALAAM: Inauma sana! Asha Hamis, mkazi wa Micheweni Kaskasini Pemba visiwani Zanzibar, anateseka kufuatia mguu wake wa kushoto kukatwa huku watoto wake wanne wakiwa ni walemavu wa kutoongea, kusikia na kutotembea, Uwazi linasikitika naye.
Akizungumza kwa uchungu akiwa nyumbani kwa ndugu yake, Kawe jijini Dar wiki iliyopita, mama huyo alisema tatizo lake lilianza kama utani mwaka jana kupitia mguu wake huo ambapo ilikuwa kama fangasi lakini siku zilivyozidi kwenda mbele, mguu huo ulikuwa ukitoboka kiasi ambacho uliweza kupitisha hata kijiti na kutokea upande wa pili.
AKIMBILIA HOSPITALI
Akiendelea kuzungumza huku machozi yakimtiririka, mama huyo alisema baada ya kuona hali ya mguu huo siyo nzuri alikwenda Hospitali ya Micheweni iliyopo visiwani humo ambapo madaktari walipompima waligundua ana ugonjwa wa kisukari hivyo walianza tiba ya kumsafisha kidonda na kumpatia dawa. Anasema aliuguza mguu huo kwa miezi minne.
MAJANGA TENA KWAKE
Mama huyo aliendelea kusema: “Baada ya kuuguza mguu huo na kupona, maumivu yalihamia mguu wa kushoto ambapo ulikuwa ukiuma sana na kuvimba mpaka ukaanza kubadilika rangi na kuwa mweusi kama mkaa. Niliporudi hospitali walinipa rufaa ya kuja Dar kwenye Hospitali ya Abbas (Kariakoo) kwa uchunguzi zaidi.
AKATWA MGUU
“Kiukweli maumivu ya mguu wangu huu siwezi kuyafananisha na kitu chochote. Pale walianza kunisafisha kwanza na kila walipokuwa wakisafisha vidole vilikuwa vikinyofoka vyenyewe hivyo waliamua kunihamishia hapa Hospital ya Kairuki Mikocheni ambapo waliponipima waliona hakuna tiba zaidi ya kukata sehemu ya mbele ya mguu wangu.
“Hakuna kitu kilichokuwa kikiniuma kama kila nilipokuwa nikisafishwa vidole vyangu kunyofoka vyenyewe. Nilikuwa najua sina uhai tena,” alisema mwanamke huyo.
MGUU WAKATWA TENA
Asha aliendelea kusema kuwa, licha ya kukatwa eneo hilo, bado hali ilizidi kuwa mbaya ambapo daktari wake baada ya kumuona alimshauri kuwa ili kuepuka sumu isipande juu zaidi mguu huo ukatwe tena eneo la karibu na goti ambapo alifanya hivyo.
“Sikuwa na jinsi nilivyoambiwa natakiwa kukatwa tena mguu. Nilikubali kutokana na maumivu makali niliyokuwa nayapata. Baada ya hapo walinipa magongo haya kwa ajili ya kuanzia maisha mapya ya bila mguu mmoja,” alisema kwa huzuni.
KINACHOMUUMA ZAIDI
Aliendelea kusema kuwa, kinachomuuma zaidi ni jinsi gani atakavyoweza kuimudu familia yake ambayo ilikuwa ikimtegemea kwa kila kitu kwani watoto wake wanne wote ni walemavu, mumewe naye ni mgonjwa na maisha wanayoishi ni magumu sana.
“Nalia sana kwani sijui nitaishije katika hali hii? Watoto wangu walemavu, hawasikii, hawaongei, wakitembea ni kwa kujiburuza tangu wakiwa wadogo-. Mtumwa ana miaka 21, Idris 18, Naomba 17 na Ibralah 15.
“Walikuwa wakinitegemea mimi kwa kila kitu maana wanatakiwa kuogeshwa, kulishwa na kufanyiwa kila kitu na hali yangu ni duni mno,” alisema mama huyo.
Msomaji uliyeguswa na hali ya mama huyu, kumbuka msemo wa kutoa si utajiri, inategemea moyo wako ulimeguswa vipi, tunaishi kwa neema ya Mungu, hakuna anayejua kesho. Hivyo unaweza kumsaidia kwa chochote ukitumia mawasiliano yake ambayo ni 0653 367442 au 0777 969202.
No comments:
Post a Comment