Mbali na kuiwakilisha vema nchi Kimataifa pia muziki huo umekuwa ukichangia pato la Taifa na kuboresha maisha ya baadhi ya Watanzania.
Msanii kutoka Tandale, Diamond Platnumz ni miongoni mwa wasanii hao baada ya kufanya vema kimataifa sasa anarudi nyumbani na kuiambia jamii asante.
Katika mahojiano yake na Starehe Diamond alisema alianza kuwashukuru wananchi wa Tandale kwa kuwalipia bima ya afya baadhi yao na kusaidia kutatua matatizo ya baadhi ya shule.
Alisema ameguswa zaidi na changamoto wanazokutana nazo wanafunzi kutokana na kukumbuka alikotoka.
“Unajua mimi nimesoma kwa shida, nimekuwa kwa shida, nimeishi kwa shida, sitamani kuona mtu mwingine akipitia hayo ndiyo maana ninapoweza kusaidia nafanya hivyo, ” alisema Diamond.
Alisema ameanza na Jiji la Dar es Salaam kwa sababu ndiko alikokulia na maeneo yenye mahitaji anayafahamu sasa anajipanga kwenda mikoani.
Alifafanua kila jambo lina wakati wake, lakini mipango yake ni kuhakikisha kidogo anachokipata anakipeleka kwa wanafunzi ambao anaamini hawana jinsi zaidi ya kusoma na hawana wa kuwatetea zaidi ya anayefahamu maisha halisi ya shule za Kayumba.
Katika kuonyesha amelipania hilo ameungana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutatua tatizo la madawati kwa kutumia Sh 48 milioni kutengeneza madawati imara yatakayodumu kwa miaka mitano kwa ajili ya shule za mkoa huo.
Alisema Makonda anapambana kuwasaidia wanafunzi wanaosoma katika mazingira kama aliyosomea yeye, hivyo hana budi kuungana naye katika mapambano hayo.
Diamond ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa lebo ya muziki (WCB) alisema kutokana na mkuu wa mkoa huyo kuchukulia sanaa ni moja ya taaluma kama nyingine wameona ni vema kurudisha faida wanayoipata kwa jamii hasa anapoona kuna mafanikio katika kazi wanayofanya.
“Tunamshukuru Paul Makonda kukubali kuwa mlezi wetu WCB, tutahakikisha kila tunalolifanya tutafanya kwa bidii kwa lengo la kutomuangusha mlezi wetu, ambaye ameonekana hataki masihara katika kazi.
“Tutahakikisha tunaendelea kusaidia kundi kubwa la vijana hususani katika sanaa kwa kuwashika mikono kukuza vipaji vyao,” alisema Diamond.
Makonda alisema msanii huyo amekuwa wa kwanza nchini kuguswa na kufanya jambo la kizalendo la kuunga mkono jitihada za Serikali.
“Namshukuru Diamond na uongozi wa WCB kwa kuisaidia jamii hususani wadogo zenu waliopo shuleni, mmeonyesha uzalendo wa hali ya juu kuungana na jitihada za Rais John Magufuli katika kuhakikisha elimu bure inapatikana na kuhakikisha changamoto mbalimbali zinamalizika,” alisema.
Atengeneza ajira 43
Licha ya kufanya vizuri katika kazi zake za muziki, Diamond amefanikiwa kutengeneza ajira 43 mpaka sasa na anatarajiwa kutengeneza ajira kwa wasomi kadhaa baada ya kuanzisha kampuni nyingine.
Kujituma kwa msanii huyu kunaifanya Tanzania kuanza kufikiria upya ni namna gani inaweza kutumia vipaji katika kutengeneza ajira kwa wasomi wanaozalishwa kila uchao katika vyuo vikuu mbalimbali na kukosa ajira.
Makonda alisema licha ya kutoa msaada huo, Diamond ana nafasi ya kuajiri wasomi na wataalamu mbalimbali kutokana na kuanzisha kampuni hiyo ya WCB inayojihusisha na masuala mbalimbali ikiwamo kuibua vipaji vipya.
“Diamond kupitia kampuni yake atahitaji watu wa sheria atakaowatumia wakati wa kuingia mikataba, wataalamu wa teknolojia watakaosimamia blog, nembo za kazi zake, watunza fedha kwa ajili ya kusimamia mapato na matumizi,” alisema Makonda.
Kuhusu WCB
WCB ni kampuni inayomilikiwa na mwanamuziki Diamond inajishughulisha na kurekodi video na audio na kusimamia wasanii (record label).
Ndani ya kampuni hiyo iliyoajiri wafanyakazi 43 kuna studio ya kupiga picha .
Kampuni inajihusisha pia na kuandaa matangazo ya biashara.
Kwa upande wa wasanii waliosaini mkataba la lebo ya kampuni hiyo, wanasimamiwa katika usambazaji wa kazi zao, utangazaji, kurekodi kazi za muziki video na audio, huku shughuli za msanii husika ikiwa ni utunzi, uimbaji na shoo.
No comments:
Post a Comment