Tuesday, 21 June 2016

ALBINO WATAKA MAKABURI YAO KUJENGWA KWA ZEGE


WADAU wa mapambano dhidi ya mauaji na unyanyapaa wa watu wenye ualbino, wamefikiana juu ya hatua nne za kuwalinda, ikiwamo kujengea makaburi yao kwa zege.



Mbali na azimio hilo, pia wamekubaliana kuwawezesha vifaa vya ujenzi kama saruji na nondo, ili kuimarisha nyumba zao kuepuka uvamizi wa wafanyabiashara wa viungo vya watu wenye ualbino.
Sambamba na hilo, wadau hao pia wamewahimiza waendesha mashtaka na polisi wanaoshughulikia kesi za watu wenye ualbino, kupewa kozi maalum ili kuharakisha usikilizwaji wa kesi hizo.

Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero alisema jana maazimio hayo yamefikiwa katika kongamano la siku tatu lililomalizika juzi jijini. Alisema maazimio hayo yatawasilishwa katika Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa ili nchi wanachama zianze utekelezaji.
“Mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yanaendelea kutokea katika bara la Afrika kutokana na ujinga kuhusu chanzo cha kisayansi cha ulemavu wa ngozi, vitendo vya kishirikina na hatua zisizoridhisha za serikali,” alisema.
Alisema ili kudhibiti vitendo viovu wanavyofanyiwa watu wenye ualbino, pamoja na mambo mengine, wamependekeza serikali kutoa nondo na vitasa madhubuti vya milango kwa makazi ya watu wenye wa kundi hilo, hasa katika maeneo ya vijijini ikiwa hatua ya kujikinga dhidi ya mashambulizi.
Alisema ripoti ya vyama vya kiraia inaonyesha kulikuwa na matukio karibu 500 katika nchi 25 yaliyoripotiwa.
Alisema hata hivyo, matukio mengi ya ukatili dhidi ya albino hayaripotiwi kutokana na usiri katika masuala ya ushirikina, ushiriki wa familia na uwezekano wa ushiriki wa matajiri na watu wenye mamlaka ndani ya serikali.
“Masuala ya haki za binadamu yanayowakabili yanayowakabili watu wenye uabino ni dharura katika nchi kadhaa za ukanda wa maziwa makuu na ni lazima kushughulikiwa kwa hatua maalum na za ufanisi,” alisema.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alisema kwa kiasi kikubwa, kongamano hilo limeyatazama vyema mapendekezo yaliyowasilishwa na serikari.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under The Same Sun, Vicky Ntetema alisema katika kuzuia mauaji ya watu wenye ualbino, kutakuwa na uhakiki katika mipaka wakati mtoto au mtu mwenye ualbino anapovuka kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Alvaro Rodriguez, aliishauri serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha katika bajeti yake kwa ajili ya mambo yanayowahusu watu wenye ualbino na kiasi hicho kiongezwe maradufu kila mwaka.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki 150 kutoka nchi 29 za kanda ya Afrika ikiwa ni pamoja na Serikali, Mashirika yasiyokuwa ya Serikari, Taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wanaharakati, Wataaam wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na wasomi.


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!