Monday, 30 May 2016

Watanzania kupata saruji ya bei nafuu

KAMPUNI ya saruji ya Dangote imetangaza bei ya saruji yake kuwa itakuwa Sh 10,000 popote, ikiwa ni punguzo.
Imesema punguzo hilo linalenga kuongeza ushindani kwenye soko la bidhaa hiyo nchini na kuwezesha watanzania wengi kununua saruji.


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, SadaLadan-Baki, alisema bei ya saruji yao aina ya 32.5R itauzwa bei hiyo ya Sh 10,000 kwa mfuko wa kilo 50; na saruji ya 42.5R itauzwa Sh 10,500 kwa mfuko wa kilo 50 kutoka kiwandani mpaka popote itakapouzwa, ikiwemo jijini Dar es Salaam, ambako bidhaa hiyo inapatikana.
Hatua hii imetajwa kuwa inafanya saruji ya Dangote kuwa ya bei nafuu kuliko nyingine, ambazo zinauzwa kati ya Sh 12,500 na Sh 14,000 jijini Dar es Salaam.
Sada alisema hatua hiyo itasaidia maendeleo ya miundombinu na kutilia mkazo mpango wa taifa wa kukabili tatizo la makazi nchini kutokana na takwimu kuonesha hapa nchini upo uhaba wa nyumba milioni tatu.
“Tunatambua uhitaji mkubwa wa miundo mbinu bora, na moja ya njia ya kulikabili tatizo hili ni kumfanya kila mtanzania kuweza kuwa na uwezo wa kununua rasilimali za ujenzi kwa kuweka bei mbadala kwa kila Mtanzania,” alisema Sada.
Uongozi huo wa kampuni ulisema bei hiyo elekezi kati ya Sh 10,000 na 10,500 imelenga jijini Dar es Salaam, ambako ndiko kitovu cha biashara, kinachoangaliwa na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, mkakati wao ni kuhakikisha bidhaa hiyo inasambaa nchi nzima na kwa bei ambayo itawezesha wananchi kuimudu.
Sada alisema katika kuwezesha bei hiyo inazingatiwa, kampuni imejizatiti katika uzalishaji na usambazaji kwa kuhakikisha bidhaa hiyo inakuwapo kwa wingi sokoni, kiasi cha kutosababisha uhaba unaoweza kushawishi wafanyabiashara kupandisha bei yake.
“Ni soko huria…lakini tutahakikisha tunasambaza mzigo kwa wingi na wasambazaji wanapata saruji kwa bei ya chini, itakayowezesha kuiuza kwa bei elekezi,” alisema baada ya kuulizwa ni namna gani watahakikisha wafanyabiashara wanazingatia bei elekezi.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kampuni, licha ya Dar es Salaam ambako lipo soko kubwa, maeneo mengine ambayo saruji ya Dangote inasambazwa, ni pamoja na Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Mbeya, Dodoma na Tanga.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!