SERIKALI imetangaza kutoa bure vifaa vya kujifungulia wajawazito katika hospitali zote za umma nchini. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana wakati wa mkutano wa kumpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi hiyo. Uliandaliwa na Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT).
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na itatoa vifaa bure kwa wanawake wanaokwenda kujifungua na kwamba serikali imejipanga kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi. Kwa mwaka, zaidi ya wanawake milioni 1.9 nchini wamekuwa wakijifungua na sasa serikali imewatua mzigo wa vifaa hivyo na sasa watakuwa wakifikiria jambo la kujifungua salama tu. Pia alisema kila hospitali ya wilaya itatoa huduma kwa watoto wasiotimiza siku za kuzaliwa (njiti) ili kuwezesha watoto hao kuishi. Pia alisema serikali itaajiri zaidi madaktari, wauguzi na wakunga ili kuboresha huduma za afya hasa vijijini. Waziri huyo alisema kila siku Watanzania 24 wanafariki kutokana na matatizo ya uzazi. Alisema kutokana na hali hiyo vituo 136 vya afya nchini vitatoa huduma ya dharura ya upasuaji na wataweza kuokoa vifo 950 kwa mwaka. Alisema mpango uliopo ni kuwa na huduma hizo kwa kila kata ili wanawake waweze kujifungua salama. Pia alisema katika sekta ya jinsia watahakikisha riba za mikopo zinashuka ili wanawake wengi wafaidike na mikopo hiyo. Pia alisema Makamu wa Rais atazindua kampeni hivi karibuni kuhakikisha kila mwanamke anakuwa na akaunti ya benki ili kama hata akitaka kuchangia katika vyama vya kuweka na kukopa Vicoba awe anatumia akaunti hiyo. Aidha alisema wameweka mikakati ya kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kupitia taasisi za kifedha bila kutumia hati za nyumba au mashamba.













No comments:
Post a Comment