Wednesday, 11 May 2016

SERIKALI YAINGIZA MILIONI 12 ZA SUKARI







WAKATI wafanyabiashara waliohodhi tani za sukari wakiendelea kuumbuliwa, serikali imeingiza nchini tani 11,959 za sukari karibu sawa na kilo milioni


Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake, Oysterbay jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema sukari hiyo ni sehemu ya tani 70,000 zilizoagizwa kutoka nchi ya kigeni, ambayo haikuitaja.

Majaliwa alisema serikali ilishaanza kusambaza sukari hiyo sehemu mbalimbali za nchi na inatakiwa kuuzwa kwa bei ya Sh. 1,800 kwa kilo.
Majaliwa alisema tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, tani 3,000 mikoa ya Kanda ya Ziwa, tani 2,000 mikoa ya Kusini, tani 2,000 Nyanda za Juu Kusini na tani 2,000 mikoa ya Kanda ya Kati.
Aidha, alisema keshokutwa wanatarajia kupokea tani nyingine 24,000 ambazo hadi Jumapili zitakuwa zimetolewa bandarini na kuanza kusambazwa siku itakayofuata.
“Tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye, zinaweza zikafika mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi Juni,” alisema na kuongeza:
“Nakiri tuna upungufu mkubwa wa sukari nchini kwa mfumo rasmi, lakini sukari tunayo, lakini kwa hali iliyofikiwa sasa kama wafanyabiashara wangefanya biashara vizuri kusingekuwa na upungufu, ingeenda sambamba na namna tulivyopanga kuagiza sukari yenye lengo la kuziba pengo linalopungua kutokana na uzalishaji wetu wa ndani,” alisema Majaliwa.
Alisema mahitaji ya nchi ni tani 420,000 ambapo uzalishaji wa viwanda ni tani 320,000 na upungufu ni tani 100,000 ambao serikali huweka utaratibu wa kuagiza.
Alisisitiza kuwa mkakati wa serikali ni kuimarisha viwanda vya ndani lengo likiwa ni kudhibiti bidhaa ambazo Tanzania inaweza kuzizalisha kupitia viwanda vyake.
Aidha, Majaliwa amewatoa hofu Watanzania kuhusu uhaba huo uliojitokeza hivi karibuni ambao umesababishwa na watu wachache.
“Rais ameagiza watu waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Waziri Mkuu amewataka wasambazaji wa sukari waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawauzie wananchi kwa bei elekezi ya Sh. 1,800.
Pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wa wilaya kuhakikisha wanasimamia ukaguzi ili kubaini wale waliohodhi bidhaa hiyo.
Kuhusu mkakati wa serikali kuongeza uzalishaji wa sukari, Majaliwa alisema lengo ni ifikapo mwaka 2019 tatizo la uhaba linakwisha.
“Wananchi wasiogope, serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
Aliongeza: “Tunao mkakati wa kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga kwa ajili hiyo,” alisema Majaliwa.
Alisema serikali imetenga maeneo matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma ambako wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi pengo lililopo litakapomalizwa.
“Mkakati ni kuboresha viwanda vya ndani, kila kiwanda kina upungufu wake na mikakati yao, lakini kama serikali tuna wajibu wa kukaa nao na kuwaeleza namna ya kuviboresha, tumekubaliana miaka minne ya uboreshaji ili tupunguze uagizaji wa kutoka nje,” alisema.
Kadhalika, alisema hata viwanda vikianza uzalishaji, serikali itadhibiti uagizaji wa sukari inayotoka nje .
Kuhusu Baraza la Madiwani kurudisha hisa za Uda, Waziri Mkuu alisema kama jiji wanataka kuzirudisha zipo taratibu wanatakiwa kuzifuata ikiwamo kufuata sheria kama itawaruhusu kufanya hivyo.
Alisema mradi huo unamilikiwa na serikali kwa asilimia 49 huku sekta binafsi ikiwa na asilimia 51.
TAKUKURU YAKAMATA TANI 1,840 BANDARINI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, limekamata tani 1,840 zilizokuwa zimehifadhiwa Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miezi mitano.
Kiasi hicho cha sukari kilikuwa kimehifdhiwa katika makontena 70 kinadaiwa ni mali ya Mbunge wa CCM Jimbo la Mpendae Zanzibar, Salim Turky, kilibainika baada ya Takukuru kupewa taarifa na vyanzo vyao vya habari.
Akielezea tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi wa uchunguzi Takukuru, Leonard Mtalai, alisema kiasi hicho cha sukari kontena 30 zilikuwa zimehifadhiwa katika Bandari ya Dar es Salaam na kontena 40 katika bandari kavu iliyopo Ubungo.
“Takukuru tulipata taarifa kutoka kwa watu wema kuwa kuna kiasi cha kontena 70 za sukari zipo bandarini na mfanyabishara huyo hataki kuiingiza sokoni, hivyo tukafanya uchunguzi na tukajiridhisha kuwa ni kweli,” alisema Mtalai.
Mtalai alisema walimwita Turky na kumuuliza kama sukari hiyo ni yake, na kwamba alikiri, hivyo Takukuru ilipitia taarifa za mzigo huo kama ulikuwa unadaiwa au la.
Matalai alisema Takukuru imempa saa 36 mfanyabiashara huyo awe ameshaitoa sukari hiyo bandarini na kuiingiza sokoni, kwani taratibu zote zilishakamilika muda mrefu.
Alisema sukari hiyo itauzwa kwa bei elekezi ya Sh.1,800 kwa kilo kama agizo la serikali linavyoelekeza.
Naye Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Joctan Kyamuhanga, alisema taratibu za kuondoa kontena hizo zilikamilika muda mrefu.
Alisema Turky ni mfanyabiashara wa sukari wa muda mrefu, na kwamba sukari hiyo ilikaa mwezi mmoja bandarini ikisubiri kupata kibali.
Hata hivyo, Turky ambaye alikuwapo wakati Takukuru wakikagua makontena hayo, alisema yeye siyo mmiliki wa sukari hiyo bali ni mdau aliyetaka sukari itoke kwa uharaka bandarini.
Alisema sukari haikufichwa wala kukwama bali kulikuwapo na utaratibu uliokuwa unasubiriwa.
Alisema sukari hiyo ilifika muda mrefu bandarini hapo, lakini ilikuwa inapelekwa Burundi na Kampuni ya Zenji General Traders.
Alisema kutokana na hali ya kisiasa Burundi kuwa mbaya, sukari hiyo iliuzwa na kununuliwa na Kampuni ya Al-Naeem ambayo Mkurugenzi Mtendaji wake ni Haruni Daudi Zacharia.
“Kutokana na uhaba wa sukari hapa nchini, ndiyo maana tukaona sukari hiyo ibaki hapa nchini, kwa hiyo sio muda mrefu imekaa hapa bandarini, huyu ni 'business partner'(mfanyabiashara mwenzake) wangu,” alisema Turky.
Alisema sukari hiyo iliwasili hapa nchini miezi mitatu iliyopita na ilinunuliwa kwa Dola za Kimarekani 420 kwa tani moja.
Alisema sukari hiyo itaondolewa bandarini hapo mara moja na itaingizwa sokoni.
Kwa upande wa Zacharia, alisema sukari hiyo iliwasili nchini Machi 3, mwaka huu, na Mei 5, mwaka huu walipewa kibali cha kuitoa sukari bandarini, na siku nne baadaye walipata kibali kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuwa sukari hiyo ilikuwa salama kwa walaji.
Mkurugenzi wa Shughuli za Maendeleo wa Kitengo cha Huduma ya Makontena Banadarini (TICTS), Donald Talawa, alisema mzigo huo ulipokelewa miezi mitano iliyopita, lakini hadi jana gharama za TICTS zilikuwa hazijalipwa.
MAKONDA AVAMIA GHOROFA AKAMATA SUKARI
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema tayari wamekatama jumla ya tani 54,860 za sukari, zilizofichwa na wafanyabiashara mbalimbali jijini hapa.
Aidha, ameahidi kutoa taarifa ndani ya saa 24, kuanzia jana, juu ya hatua ambazo watachukua wakati wakiendelea kubaini sukari nyingine zilizofichwa.
Makonda aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaaam, mara baada ya kutembelea jengo la ghorofa tisa lililokuwa limeficha mifuko 160 ya sukari maeneo ya Kinondoni Hananasif.
Alibainisha kuwa, katika Wilaya ya Ilala wamekamata tani 52,000, Temeke tani 2,700 huku Kinondoni wakikamata mifuko 160.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wake kupekua jengo zima kama kuna sukari nyingine, lakini pia kuna taarifa ya kigogo ambaye ameficha tani nyingi za sukari, tunaendelea kuchunguza na ndani ya saa 24 tutatoa taarifa juu ya hatua tutakazozichukua,” alisema Makonda.
Pia, aliwataka wananchi kutoa taarifa za watu wanaoshiriki kuficha sukari katika maeneo wanayoishi badala ya kuiachia kazi hiyo Jeshi la Polisi pekee.
“Wafanyabishara wakubwa wameamua kuficha sukari ili kuikomoa serikali, lakini ni wajibu wa wananchi kuwafichua kwa sababu wanaopata shida ni wenyewe na siyo Rais John Magufuli, “ alisema Makonda.
Akiwa katika jengo hilo, Makonda alionyeshwa mifuko 160 yenye ujazo wa kilo 20 na 25, ambayo ilikuwa imechanganywa na mifuko ya ‘gypsum’ huku mmiliki wa jengo hilo, Bushiru Haruni Ismail, akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.
Kadhalika, katika ukaguzi huo, ilikutwa mifuko yenye nembo ya `Kilombero Sugar’ na TBS, na kushindwa kufahamika mara moja ni ya kazi gani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime, alisema mtuhumiwa huyo walimkamatwa juzi baada ya kubainika kwa tukio hilo.
MTENDAJI ASAKWA KWA KUHONGWA MFUKO MMOJA
Wakati mmiliki wa jengo hilo akishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, Makonda pia ameagiza Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Hananasif, kukamatwa mara moja ili kuhojiwa kutokana na tuhuma za kuhongwa mfuko mmoja wa sukari wa kilo 25.
Kamanda Fuime, alimueleza Makonda kuwa mmiliki wa jengo hilo alimpatia mtendaji wa mtaa huo, mfuko huo wa sukari ili kutotoa taarifa juu ya tukio hilo.
“Naagiza kuanzia sasa huyu mtendaji naye awekwe ndani wakati tunaendelea na upelelezi,” alisema Makonda.
Mmiliki wa jengo alijitetea mbele ya Makonda kuwa, sukari hiyo alipewa na ndugu yake ambaye ni Haroon Zakaria, zaidi ya tani nne kwa ajili ya kuwagawia watoto yatima.
“Jengo hili nimelitumia kwa ajili ya kuhifadhi sukari ambayo ninatoa msaada kwa watoto yatima katika Msikiti wa Malakasi na mifuko iliyokutwa ni kwa ajili ya kupunguzia sukari kutoka kwenye mifuko mingine,” alisema.
Alibainisha kuwa, sukari hiyo alipatiwa kipindi cha miezi sita iliyopita na kwamba ilikuwa ni pamoja na vyakula vya nafaka kama mchele na maharagwe, na amekuwa akivigawa bure kwa wahitaji katika kipindi cha kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani,” alisema Ismail.
MIFUKO 256 YAKAMATWA MASASI
Jumla ya mifuko 256 sawa na kilo 6,400 za sukari ya mfanyabiashara maarufu aliyejulikana kwa jina la Tanganyika zimekamatwa maeneo ya maduka makubwa ya Mkuti Kaumu wilayani Masasi mkoani Mtwara katika moja ya vyumba vya kuhifadhia bidhaa kwenye maduka hayo.
Kubainika kufichwa kwa mifuko hiyo ya sukari na mfanyabiashara huyo, kumekutokana na msako mkali uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama juzi kwa lengo la kuwabaini baadhi ya wafanyabiashara ambao wameficha bidhaa hiyo ili wauze kwa bei ya juu kwa wananchi kinyume cha agizo la serikali.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Benard Ndutta, alisema kuwa wamefanikiwa kukamata sukari hiyo kutokana na msako waliofanya juzi kwa kuwatafuta wafanyabiashara ambao wameamua kuificha kwa makusudi ili wauze kwa bei ya juu na kujipatia kipato kikubwa zaidi.
Alisema serikali imeshatoa bei elekezi ya uuzaji wa sukari kuwa ni Sh. 1800 kwa wafanyabishara nchini na kwamba iwapo kuna mfanyabishara anaamua kwa makusudi kuficha sukari kwa kupinga agizo la serikali ili aweze kuuza bidhaa hiyo kwa bei tofauti na iliyotangazwa na serikali ni kuvunja kanuni na taratibu za nchi.
NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!