Mahakama ya Wilaya ya Morogoro imeamuru mwili wa mtoto, David Mng’ombe (8) mkazi wa Gairo kuzikwa kwa imani ya dini ya Kikristo baada ya kuwapo kwa mvutano baina ya baba wa mtoto, Shukuru Mng’ombe na mama yake, Emilia Chitemo kuhusu dini.
Mtoto huyo alifariki dunia Mei 5, mwaka huu katika kijiji cha Msingisi Wilaya ya Gairo, lakini ulitokea mvutano kati ya wazazi kuhusu dini ya kumzikia mtoto kwakuwa wazazi wana imani tofauti za dini, na kila mzazi alitaka kumzika kwa dini yake.
Emilia alishinikiza mwanawe azikwe kwa imani ya dini ya Kiislamu kwa maelezo mtoto huyo alimzaa kwa mazingira ya imani hiyo, na hakupata matunzo ya baba ambaye ni Mkristo.
Hata hivyo, kutokana na mvutano huo Emilia aliamua kufungua kesi mahakamani akitaka mahakama impe mamlaka ya kumzika mwanawe kwa imani ya dini ya Kiislamu.
Emilia hakuweza kuthibitisha madai yake, lakini mahakama ilikubaliana na ushahidi wa Shukuru ambaye alitoa vielelezo mahakamani vilivyoonyesha mtoto alizaliwa katika ukristo na kadi ya bima ya afya ya mtoto ilisomeka jina la David Shukuru Mng’ombe.
Awali akitoa ushahidi wa kuthibitisha kuwa mtoto ni wake huku akiongozwa na wakili Profesa Siliacus Binamungu, baba wa mtoto huyo alidai kuwa mvutano huo wa kugombea maiti ulikuja baada ya kuachana na mzazi mwenzake, ambaye baadaye aliolewa na mwanamume Muislamu ambako alibadili dini na kuwa Muislamu.
Hakimu Alicele Mwankesela aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alitoa hukumu iliyompa mamlaka Shukuru kumzika mwanawe kwa dini ya Kikristo.
Umuzi huo haukukubaliwa na upande wa Emilia, ambao walianza kutoa kauli za vitisho na kumlazimu hakimu kulitaka Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi kwenye msiba huo hadi shughuli za mazishi zitakapomalizika.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment