Shoo hiyo iliyoandaliwa na kituo cha redio cha Jembe Fm na kupewa jina la Jembeka Festival inatarajiwa kuacha historia ya aina yake kwa wapenzi wa burudani nchini hasa wakazi wa Mwanza.
Ni shoo ya aina yake ya kimataifa ambayo wakazi wa Jiji la Mwanza wanabahatika kuipata ikiwa imesheheni wanamuziki lukuki wenye kazi tamu masikioni.
Kwa mara ya kwanza mwanamuziki wa Marekani Shaffer Chimere Smith maarufu Neyo atafanya shoo nchini katika jiji hilo maarufu kwa samaki na mawe makubwa.
Wapenzi wa muziki wanatarajia kupata burudani ya nguvu kutoka kwa nyota huyu ambaye amewahi kutamba na nyimbo kali kama Miss Independent, Sexy Love, “Because of You”, “So Sick”, Let Me Love You” “Go On Girl” Mad” One In A Million” na nyinginezo.
Neyo atasimama jukwaa moja na Diamond Platnum a.k.a Simba msanii wa bongofleva anayekimbiza sio tu nchini bali Afrika nzima.
Diamond naye anatarajiwa kushusha shoo ya nguvu kupitia nyimbo zake zinazotamba kimataifa zikiwemo Nana, Utanipenda, Make Me Sing,Number One, Nasema Nawe, Bum Bum na nyingine kibao kutoka kwa nyota huyu anayeng’ara Afrika.
Kolabo zake na wasanii wenye majina makubwa barani Afrika kama Davido,A.K.A,Mafikizolo,Iyanya,Mr Flavour, Waje, Akothee, Bracket na wengine huenda zikamfanya Diamond Platnum amfunike Neyo, lakini mwisho wa siku kila mashabiki ndio watakaoamua.
Shoo hiyo haitawakutanisha nyota hao pekee, watakuwepo na wasanii wengine wanaofanya vizuri Bongo akiwamo Nay wa Mitego, Ruby, Maua Sama, Mr Blue, Fid Q, Stamina, Mo Music na Baraka Da Prince.
Wale waliokuwa wakivutiwa zaidi na muziki wa Bongo Fleva ya enzi zile mzee mzima Juma Nature ‘Kiroboto’ atakuwa jukwaani kushusha burudani ya nguvu.
Nyota huyu asiyechuja atakumbushia nyimbo zake matata kama Sitaki demu, Mtoto Idd, Ugali, Hakuna Kulala, Inaniuma Sana, Mzee wa Busara, Sonia, Jinsi Kijana, Hili Game, Dogo na nyingine kadhaa ambazo amewahi kutamba nazo mkongwe huyu.
No comments:
Post a Comment