Tuesday, 17 May 2016

FAHAMU KUHUSU UGONJWA WA HOMA YA TUMBO (TYPHOID FEVER)

Homa ya Tumbo (Typhoid Fever)

Homa ya tumbo ikijulikana kama Typhoid fever kwa kiingereza ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria aina ya Salmoneilla typhi. Hii ni homa hatari inayoweza kuathiri ogani nyingi mwilini, na huambukizwa hasa kwa njia ya chakula.


Jinsi Ugonjwa Unavyotokea

Ugonjwa wa homa ya tumbo husababishwa na bakteria aina ya Salmoneilla typhi na Salmoneilla paratyphi. Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya kula chakula au maji yenye vijududu hivi.
Baada ya bakteria kuingia kwenye mwili kupitia maji au chakula, huvamia utumbo mdogo na kuingia kwenye mishipa ya damu. Huingia kwenye bandama, ini na ute wa damu na kuzaliana na baadae kuingia kwenye mishipa ya damu tena. Hapa ndipo homa na dalili nyingine huanza. Huendelea kusambaa kwenye utumbo, kongosho na mishipa ya limfu.

Dalili

Dalili za homa ya tumbo huanza kujionesha siku 7 – 14 baada ya vijidudu kuingia mwilini na ugonjwa kudumu kwa wiki 2 mpaka 4.. Dalili za homa ya tumbo hujumuisha
  • Homa
  • Kukosa hamu ya chakula
  • Tumbo kuuma
  • Kukosa choo
  • Kichwa kuuma
  • Kujisikia vibaya mwili mzima na kuchoka
Homa. Homa huanza na kupanda polepole kadri siku zinavyoenda. Unaweza ukawa unahisi baridi au joto kali zaidi ya kawaida. Baadae unaweza kupata homa kali inayoweza kuambatana na kutokwa jasho au kutetemeka.
Maumivu ya Tumbo. Ugonjwa huu huambatana na maumivu ya tumbo, ambayo yanaweza kusambaa tumbo lote. Unaweza kupata maumivu hata pale unapoligusa tumbo. Tumbo linaweza kuvimba pia.
Kukosa Choo. Vijidudu vya salmoneilla hushambulia utumbo na kusababisha ushindwe kufanya kazi vizuri. Hali hii husababisha kukosa choo, siku kadhaa baada ya dalili za homa kuanza. Hali ya kukosa choo huweza kukaa kwa siku kadhaa.
Kuharisha.  Unaweza kuanza kuharisha baada ya kuanza kupata dalili za homa ya tumbo. Wakati mwingine choo kinaweza kuwa na damu damu kama utumbo ukiathiriwa na kutoboka.
Pamoja na dalili hizo, mgonjwa huchoka, kupata maumivu sehemu mbalimbali za mwili, kukosa hamu ya kula na mwili kuosa nguvu.
Homa ya tumbo isiyotibiwa huweza kuleta kupoteza fahamu, utumbo kutoboka, damu kumwagika tumboni na hatimaye kifo.
Asilimia 10 ya watu wenye homa ya tumbo dalili hujirudia wiki moja mpaka 2 baada ya kupona. Matibabu kwa dawa za kuua bakteria (antibiotics) ni muhimu.

Matibabu

Homa ya tumbo hutibiwa kwa dawa za kuua bakteria (antibiotics). Mgonjwa huanza kupata nafuu siku ya kwanza mpaka ya pili baada ya kuanza dawa na kupona kabisa baada ya siku 7 mpaka 10.
Mgonjwa anaweza kutibiwa kwa kupewa dawa za kunywa akiwa nyumbani au kulazwa na kutibiwa akiwa hospitalini. Hii inategemea na hali ya mgonjwa.
Dawa za kuua bakteria (antibiotics) hutumika kutibu ugonjwa huu. Ciprofloxacin, Cefotaxime na Azithromycin hutumika kutibu homa ya tumbo ambayo sio kali, ikiwa kali sindano za Ciprofloxacin au Ceftriaxone hutumika kutibu ugonjwa huu. matibabu huenda kwa siku 7 mpaka 14.
Pamoja na dawa za kuua bakteria (antibiotics), dawa za kutuliza homa na maji ya dripu hutolewa ili kumuimarisha mgonjwa.
Ikiwa homa ya tumbo inajirudia, basi itabidi mgonjwa tibiwe kwa dawa za kuua bakteria. Anaweza kuhitaji matibabu kwa muda mrefu zaidi.

Kujikinga na Ugonjwa

Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya chakula au maji yaliyoingiliwa na vijidudu. Ili kujikinga ni muhimu zuingatie yafuatayo:
  • Nawa mikono kwa maji safi kabla na baada ya kula chakula au matunda.
  • Nawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka chooni.
  • Osha matunda kwa maji safi kabla ya kuyatumia
  • Tumia maji safi yaliyochemshwa au kutakaswa kwa ajili ya kunywa.
  • Ni muhimu mtu mwenye ugonjwa ta taifodi asihusike kwenye maandalizi ya chakula (upishi) ili asiambukize watu wengine.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!