“HALI ngumu ya maisha inafanya tukate miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, tunajua tunaharibu mazingira lakini lazima watoto wapate chakula, Hapa Bahi kipindi kirefu cha mwaka ni ukame, tunalima tunapata chakula kidogo kisichoweza kutosheleza mwaka mzima,” anasema mkazi wa kijiji cha Mpwamatwa wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Mkwayi Paulo.
“Hapa barabarani tunapouza mkaa tumekuwa tukiishi kwa wasiwasi sana, hata gari likisimama tunalazimika kukimbia kwa hofu ya kuogopa kukamatwa. “Ni vyema sasa serikali inatulipia ada ya watoto shuleni baada ya Rais John Magufuli kutangaza elimu bure. Hii umetusaidia kutua mzigo mzito sasa sisi wananchi wa hali ya chini, lakini kwenye chakula sisi watu wa Bahi mvua zinapokosekana hali inakuwa ni mbaya sana. Kazi ya kuchoma mkaa imekuwa ikitusaidia kupata fedha kwa ajili ya kununua chakula,” anasema mwananchi huyo.
Naye Saidi Andrea anayeishi Mkakatika wilayani humo anasema amekuwa akiuza gunia moja la mkaa kwa Sh 15,000 na kwa siku anaweza kuuza magunia mawili hadi matatu. “Hali hii ya ukataji miti inatuathiri hata sisi kwa sababu vyanzo vya maji vinaathirika kwa kukauka. Shida ndiyo inatupelekea kufanya yote haya lakini nikisaidiwa ujuzi wowote wa kuniingizia pesa kama mbadala, naacha hii kazi hata sasa,” anasema Andrea.
Anasema biashara hiyo imekuwa pia ikiathiri afya yake kwa kuwa mara kwa mara anapata ugonjwa wa kukohoa unaosababishwa na vumbi la mkaa. Bahi kama yalivyo maeneo mengi nchini yamekuwa yakikabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, hali ambayo imekuwa ikichangiwa na ukame. Hata hivyo, umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira nchini unachochewa zaidi na ukweli kwamba maliasili pamoja na mazingira ni muhimu katika ustawi wa maisha ya watu na ndiyo muhimili katika sekta za uzalishaji kikiwemo kilimo, utalii, uvuvi na madini.
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi inakusudia kurekebisha sheria ndogo ya ushuru ili kuwabana wauza mkaa ambao wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu mazingira. Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Rachel Chuwa, anasema kutokana na kukithiri kwa uharibifu wa mazingira kwa kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, wanakusudia kuboresha sheria ndogo ya halmashauri. Sheria hiyo ilikuwa ikiruhusu ushuru kwa wauza mkaa iwe Sh 2,000 kwa gunia hivyo kusababisha ongezeko la biashara hiyo.
“Sheria iliyopo inaruhusu kuchukua ushuru tumegundua inaendelea kusababisha uharibifu wa mazingira sasa badala ya Sh 2,000 tunataka iwe juu zaidi ili wanaofanya hivyo waachane na biashara hiyo,” anasema Chuwa. Anasema, kuna uharibifu wa mazingira katika halmashauri hiyo kutokana na sababu kadhaa ukiwemo ukosefu wa mvua za kutosha hivyo kusababisha wananchi wachome mkaa kujipatia kipato.
Anayataja maeneo yanayoongoza kwa uharibifu kuwa ni kijiji cha Mpangwe, kata ya Mwitikira, Mkakatika, Uhelela na mpakani mwa wilaya ya Bahi na Manyoni mkoani Singida. Chuwa anasema pia uharibifu huo wa mazingira umeyakumba maeneo ya misitu ya Babayu, Msisi na Lamaiti. Pia katika kudhibiti uharibifu huo anasema wamekuwa wakishirikiana na Wakala wa Taifa wa Misitu (TFS) ambao wamekuwa wakifanya msako na kukamata wauzaji na wasafirishaji mkaa kwenye vizuizi.
Anasema, kwa sasa kipaumbele kipo kwenye kupanda miti. Mwaka huu wananchi wamepanda miche ya miti 220,000 katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo. “Mwaka ujao tutajizatiti kupanda miti mingi zaidi,” anasema Chuwa. Mkurugenzi huyo anasema jamii inatakiwa kuona umuhimu wa kupanda miti na kuitunza ili iweze kufaa kwa vizazi vijavyo ikiwemo kupanda miti ya matunda kama michungwa, mipera, miembe ili mwananchi aweze kufaidi kwa kupata kivuli na matunda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Danford Chisomi anasema ukataji miti limekuwa tatizo kubwa katika wilaya hiyo. Aidha ushuru wa mkaa ulikuwa ni moja ya vyanzo vya mapato katika halmashauri lakini kinachoonekana sasa ni uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea. “Tutabadilisha baadhi ya vipengele na kuweka kiasi kikubwa cha ushuru ili wanaofanya biashara ya mkaa wakatafute kazi nyingine za kufanya,” anasema.
Kadhalika anasema bei ya mkaa ikipanda wananchi nao watatafuta vyanzo vingine vya nishati kama kutumia majiko ya gesi, mafuta na hata umeme ili kuondokana na tatizo la ukataji miti ovyo. Pia anasema wanaendelea na mikakati ya kuhakikisha kila tarafa inakuwa na vitalu vya miti ili visaidie kusambaza miche hiyo kwenye maeneo ya kata na vijiji na wananchi watapewa elimu ya kuitunza miche hiyo ili iweze kukua.
Diwani wa Kata ya Bahi, Agustino Ndowo anasema kuna umuhimu mkubwa sana kwa wananchi kupewa elimu ya kutunza mazingira. Ndowo anasema wananchi pia wanatakiwa kutumia majiko banifu ambayo yanatumia mkaa mchache na hata kutumia mkaa wa karatasi na randa za mbao ili kujiepusha na ukataji miti ovyo. Anasema sasa kuna matumizi ya gesi na kama wananchi wataelimishwa watatumia nishati mbadala ya mkaa ili kuweza kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira.
Blandina Magawa ambaye ni Diwani wa Kata ya Ibugule wilaya ya Bahi anasema changamoto ya uharibifu wa mazingira ni kubwa ni muhimu wananchi wakafundishwa kuachana na uharibifu huo. Anabainisha kuwa wengi wanaochoma mkaa wanafanya hivyo ili kujiongezea kipato, ukitoa elimu wanaweza kuachana na kukata miti ovyo kwani katika maeneo mengi wananchi wamekuwa wakikata miti ovyo bila kupanda miti mingine hali ambayo inaweza kusababisha madhara kwa siku za usoni.
Sasa kwenye baadhi ya vijiji wamejiwekea sheria mtu akikutwa anakata mti anatozwa faini. “Mtu akikata mti tumejipangia faini, atachukuliwa hatua kwa gharama ambazo zinapangwa na Serikali ya Kijiji,” anasema. Hata wananchi wengi wanaofanya makosa kama hayo wanapokamatwa kimbilio lao linakuwa kwa madiwani hali ambayo wananchi wanachukulia kuwa madiwani wamekuwa wakitetea waharibifu wa mazingira jambo ambalo si kweli.
Vilevile anawataka wanasiasa kusimama kwenye nafasi yao katika vita hii ya uharibifu wa mazingira na kuacha kutetea watu wa namna hiyo ili kuweza kuokoa mazingira. Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Francis Mwonga anasema mazingira ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya nchi. Kutokana na hilo anaona kuna umuhimu wa kuyalinda ikiwemo kulinda vyanzo vya maji ili viweze kutumiwa kwa njia endelevu ili viweze kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.
Pia anasema sasa wamepiga marufuku shughuli za kibinadamu karibu na chanzo cha maji cha Mzakwe ambacho ni tegemeo kwa Mji wa Dodoma. Anasema kumekuwa na wavamizi kwenye chanzo cha maji ili kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa. Wakati juhudi zikuchukuliwa kuwabana wanaochoma mkaa, ni vyema pia juhudi zikaongezwa katika kuwapatia shughuli mbadala wananchi hao kama vile ufugaji wa nyuki sambamba na kupunguza soko la mkaa kwa kuwapa wananchi nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.
No comments:
Post a Comment