Sunday, 15 May 2016
Chanzo Kikuu Cha Mafanikio Na Furaha Kwenye Maisha yako.
Habari za leo mwanafalsafa mwenzangu?
Karibu kwenye kipengele chetu hiki cha FALSAFA MPYA YA MAISHA ambapo tunajijengea falsafa ambayo itatuwezesha kuwa na maisha bora yenye mafanikio na furaha.
Tumeshajifunza sana kuhusu mafanikio na mbinu za kufikia mafanikio. Na pia tumeshajifunza sana kuhusu furaha na vyanzo vya furaha kwenye maisha yetu. Hivyo kwa sasa nategemea utakuwa na mafanikio na furaha, kwa sababu ni maisha ya mafanikio na furaha ndiyo maisha bora kuishi.
Lakini kwa bahati mbaya sana wengi bado hawana mafanikio wala furaha. Wanaishi maisha ya kupita tu kama wanasubiri kitu fulani, hawapati kitu hiko na maisha yao yanazidi kuwa magumu. Leo tutakwenda kuviangalia vitu hivi viwili kwa pamoja, ili tuone njia bora ya kuwa navyo vyote kwa pamoja ili tuwe na maisha bora.
Maisha bora yanaanza na sisi wenyewe na kwa kupitia falsafa hii mpya ya maisha kila mmoja wetu ataweza kuwa na maisha bora sana kwake.
Mafanikio.
Mafanikio kwa lugha rahisi ambayo kila mtu anaweza kuielewa na kuifanyia kazi ni kupata kile ambacho unakitaka. Hivyo mafanikio yoyote yanaanza na hitaji au ndoto au malengo. Ambapo unapanga kupata kitu fulani ambacho ni muhimu kwako au kinahitajika ili maisha yako yaweze kwenda vizuri. Baada ya kujua hiki unachokitaka sasa unakifanyia kazi, unaweza juhudi kubwa kuhakikisha unapata hiki unachokitaka. Na pale unapokipata ndiyo mafanikio.
Elewa vizuri hapo ya kwamba mafanikio ni kupata kile unachotaka, bila ya kujali ni kikubwa au kidogo, na wala hatujaweka fedha au mali hapo. Hii ina maana kwamba mafanikio yana maana tofauti kwa watu tofauti na kwa nyakati tofauti. Unapopata kile unachotaka kwenye kazi yako basi unakuwa na kazi yenye mafanikio. Hivyo pia kwa biashara yako na hata maisha yako kwa ujumla.
Mafanikio yanaanza na wewe kwa kujua kile unachokitaka na kukifanyia kazi. Kitu hiki kinakuwa muhimu kwako na kinakuwa na maana kwenye maisha yako. Unapoelewa hili ni rahisi kuishi maisha ya mafanikio kwa sababu kila hatua utakayopiga utaiona ni muhimu kwako kufika kule unakotaka kufika.
Furaha.
Furaha ni kupenda kile ambacho unakipata. Unapokuwa umepanga kupata kitu, na ukaweza kukipata, unapokipenda kitu hiko ndipo furaha yako inapoanzia. Siyo kitu kile kinaleta furaha, bali wewe unavyokichukulia kitu hiko ndiyo chanzo cha furaha yako.
Hapa ndipo watu wengi wanapokosea kwa kuahirisha furaha zao. Unakuta mtu amepanga kupata kitu fulani, anakifanyia kazi na kukipata, lakini akishakipata anagundua kuna kingine kikubwa zaidi na hivyo kuhamisha furaha yake kwamba akipata kile kikubwa zaidi ndiyo atakuwa na furaha. Sasa changamoto ni kwamba mchezo huu hauna mwisho. Kwa kitu chochote unachotaka, ukikipata bado utaona kuna nafasi ya kupata zaidi. Ukifuata njia hii kila mara utakuwa unaahirisha furaha na hakuna siku utakayofika na kusema leo nimefikia kilele cha furaha.
Kama ni fedha kila siku kuna fedha zaidi, ukipata mamilioni kuna mabilioni, ukipata mabilioni kuna matrilioni. Kama ni mali kila hatua zipo zaidi, kama ni gari kila ulilonalo kuna bora zaidi ya hilo. Hivyo njia pekee ya kuwa na furaha siyo kusubiri mpaka upate cha juu, bali kupenda kile ulichopata sasa.
Na unaweza kupenda kile ulichonacho sasa kwa kutambua mchango ambao kimekuletea kwenye maisha yako. Unaweza kudharau kazi uliyonayo sasa siyo unayoitaka kwenye maisha, lakini ukasahau kwamba kazi hiyo ndiyo inakuwezesha kuendesha maisha yako kwa sasa. Unaweza kuona biashara uliyonayo siyo bora kama unavyotaka lakini ukasahau kwamba angalau una sehemu ya kuanzia.
Anza na kupenda kile ambacho umepata, kile ambacho unacho na maisha yako yatakuwa ya furaha. Na hii haijalishi ni vitu vizuri kiasi gani unavyo kwenye maisha, bali ni jinsi gani unaviona ni muhimu kwenye maisha yako. Ndiyo maana tunasema furaha hailetwi na kitu, bali mtazamo wako mwenyewe kwenye vitu vinavyokuzunguka.
Tuviweke pamoja.
Sasa tukiviweka pamoja, mafanikio na furaha ndiyo tunapata maisha bora sana kwetu. Na kwa pamoja inakuwa kwamba kuna kitu ambacho tunakitaka na tunaweka juhudi kukipata na tukishakipata tunapenda kile tulichopata. Haijalishi kama ni kitu kikubwa au kidogo, bali tunajua tumekipata kwa juhudi zetu na tunaona mchango wa kitu hiko kwenye maisha yetu.
Kwa njia hii ni marufuku kwako wewe kama mwanafalsafa kusema maisha yako hayana mafanikio wala furaha, kwa sababu tayari ufunguo mkuu wa mafanikio na furaha unao. Achana na zile ndoto za mchana za kusubiri mpaka ufikie hatua za juu ndiyo useme una mafanikio na furaha. Anza na kile ambacho unacho sasa, na kadiri unavyokithamini ndivyo unavyoweza kuchimba ndani zaidi na kupata zaidi.
Hii ina maana kwamba kadiri unavyoona maisha yako ni ya hovyo na huna cha kufurahia, ndivyo unavyokaribisha hali hizo ambazo ni za hovyo. Lakini ukiweza kubadili mtazamo huo na kuona maisha yako ni ya mafanikio na furaha, ndivyo utakavyokaribisha hali zinazoleta mafanikio zaidi na furaha. Na kumbuka hubadili tu mtazamo kujifurahisha, bali unaubadili kwa uhalisia kwa kuchukulia kwa uzito kile unachotaka na kile unachokipata.
Tahadhari.
Tumalize kwa tahadhari kwamba kukosa kile unachotaka hakumaanishi ya kwamba huna mafanikio na hakupaswi kuwa chanzo cha wewe kukosa furaha. Kwa sababu siyo mara zote unazoweza kupata kile unachotaka, changamoto ni nyingi. Muhimu ni wewe kujua unaendelea kuchukua hatua, na kila hatua ndogo unayopiga ni mafanikio. Pale unaposhindwa na kuweza kuanza tena ni mafanikio. Na furaha unayo muda wote, kwa kupenda vile ambavyo unavyo kwa sasa.
Mafanikio na furaha tayari unavyo hapo ulipo sasa, bila ya kujali unapitia wapi. Ni wajibu wako kuendelea kuvitumia ili kuwa na masiha bora na kuendelea kuwa na maisha bora.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea falsafa hii mpya ya maisha yako, ambayo itakuletea maisha ya furaha na mafanikio.
Rafiki na Kocha wako.
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment