Sunday, 22 May 2016

Askari asimulia siku ya mwisho ya kinyogoli kazini



Marehemu Kinyogoli enzu za uhai wake.
Dar es Salaam. Saa chache kabla ya kifo chake, Ally Salum Kinyogoli, aliyekuwa askari wa usalama barabarani, alisikika akisema; “wanawake watamtoa roho.”



Hayo yamebainishwa na mmoja wa wafanyakazi wenzake (jina linahifadhiwa) aliyekuwa naye zamu siku hiyo ambaye pia alieleza kuwa marehemu alimwachia wasia na kumwambia awe makini kwani wanawake ni hatari.
Kinyogoli aliyefariki Jumatano na kuzikwa juzi kwenye Makaburi ya Mzambarauni Kitunda, alipigwa risasi nyumbani kwake na watu wasiojulikana.
Watu hao waliokuwa wamejiziba usoni, walichukua ufunguo wa gari la Kinyogoli lakini hata hivyo hawakuondoka na gari hilo wala kitu kingine.
Hata hivyo, hadi juzi tayari watu 15 akiwamo mke wa marehemu walikuwa wanashikiliwa na polisi wakihojiwa kuhusu mauaji ya Kinyogoli. Akisimulia nyakati za mwisho za marehemu Kinyogoli, askari huyo alisema saa chache kabla hawajamaliza kazi, marehemu alikuwa akimkanya kwa kumwambia kuwa wanawake ni hatari.
“Siku hiyo alikuwa anapenda kusema wanawake hatari na hata saa chache kabla hatujaachana baada ya kumaliza kazi aliniambia wanawake wanamsumbua na watamtoa roho,” alisema askari huyo na kuongeza:
“Malalamiko yake yalikuwa juu ya wanawake, kuna wakati aligonga meza na kujisonya huku akisema wanawake bwana wasumbufu sana, sina imani nao hata, kidogo,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventure Mushongi alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.
“Kwa kifupi upelelezi unaendelea, wenzetu wa Kanda Maalumu wana nafasi nzuri ya kulisemea hili ikiwamo kamatakamata inayoendelea,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao walikwenda nyumbani kwa Kinyogoli na alipotoka nje ndipo walipofyatua risasi zilizosababisha kifo chake.
“Matukio ya kuuawa kwa askari yanatokea sana kwa sababu askari wanawakamata wahalifu hivyo tutahakikisha wale wote waliofanya ukatili huo wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Sirro.
Alisema watahakikisha wale wote waliofanya mauaji wanakamatwa hata wakienda mbali watafuatwa huko waliko ili waweze kuchukuliwa hatua.
Mgogoro wa familia
Jana, katika mahojiano na gazeti hili, mama mlezi wa marehemu Coletha Ndima alisema marehemu aliwahi kumwambia kuwa ana mgogoro na mke wake lakini hakumweleza ni upi.
Kadhalika, Ndima alieleza kuwa marehemu aliwahi kuwaambia ataoa mke wa pili lakini bado alikuwa hajatambulishwa kwenye familia hiyo.
“Aliwahi hata kuleta baadhi ya samani zake kwa sababu alidai kuwa mke wake, anauza baadhi ya vyombo,” alisema Ndima.
Alijipanga kuipokea Yanga
Kinyogoli ambaye alijipatia umaarufu kwa kutoa taarifa za hali ya foleni barabarani kwenye vyombo vya habari nchini alikuwa pia ni shabiki mkubwa wa timu ya Yanga.
Rafiki mwingine wa marehemu (jina linahifadhiwa) aliliambia gazeti hili kuwa, saa chache kabla hawajaachana Kinyogoli alimwambia kuwa juzi hatafika kazini kwa kuwa atakwenda kuipokea timu hiyo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere (JNIA).
“Aah... nakumbuka mara ya mwisho aliniambia hatakuja kazini juzi kwa sababu saa tano atakuwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kuipokea timu anayoipenda Yanga,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!