Pages

Monday, 4 April 2016

WENYE TB WAKITIBIWA WATAOKOA NA WENGINE


MACHI 24 kila mwaka, Tanzania huwa inaungana na nchi nyingine kuadhimisha siku ya kifua kikuu duniani.
Siku hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa kifua kikuu. Siku hiyo pia ni fursa kwa wadau wakiwemo wataalamu wa afya, wagonjwa, watafiti, viongozi wa serikali, wanasiasa na jamii kwa ujumla kujitathmini na kupima ni wapi tulipofikia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. Kwa mwaka huu kauli mbiu inasema ‘Tuungane kutokomeza kifua kikuu’.
Kauli hiyo inaweka msukumo kwa Tanzania kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya kifua kikuu ili kuibua wagonjwa wengi zaidi, kuwawezesha kupata tiba na kuzuia maambukizi mapya. Nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ikiwemo Tanzania zimepewa changamoto katika utekelezaji wa mkakati mpya wa dunia wa utokomezaji wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2035.
Mkakati huo unataka kuongeza kasi katika kutokomeza kifua kikuu kwa kuwafikia wagonjwa wote, kupunguza kasi ya idadi ya wagonjwa wapya kwa asilimia 90, kuwatibu na kuwaponyesha wote, kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo kwa asilimia 95 na kukomesha masumbuko yote yatokanayo na kifua kikuu. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema, kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea wanaojulikana kitaalamu kama mycobacteria tuberculosis.
Anasema mtu anayeugua ugonjwa huo na ambaye hajaanza matibabu akikohoa, kuongea, kuimba au kupiga chafya, vimelea huingia hewani na mtu yeyote atakayekuwa karibu anaweza kuambukizwa.
“Vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu huenea kwa njia ya hewa na havichagui nani wa kumuambukiza awe tajiri, masikini, mfupi, mrefu, mnene, mwembamba, mtoto, mkubwa, mwanamke au mwanaume; yeyote anaweza kuambukizwa. Vimelea hivi hutoka kwa mgonjwa wa kifua kikuu ambaye hajaanza matibabu na kuambukiza watu wengine,” anasema Waziri Mwalimu.
Aina za kifua kikuu
Anasema kuna aina mbili kuu za kifua kikuu kikiwemo cha mapafu kinachoshambulia mapafu na aina nyingine ni kifua kikuu cha nje ya mapafu. Katika aina ya pili, sehemu yoyote zaidi ya mapafu hushambuliwa na ugonjwa huo, mfano tezi, uti wa mgongo, ngozi, mifupa, moyo, utumbo, ini, figo na nyinginezo.
Dalili za ugonjwa Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kukohoa kwa wiki mbili mfululizo au zaidi, homa za mara kwa mara hasa nyakati za jioni, kutokwa na jasho jingi usiku kuliko kawaida, kukosa hamu ya kula na kupungua uzito na kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu. Mtu anayeugua kifua kikuu anaweza kuwa na dalili moja tu kati ya hizo au zote zilizotajwa hapo juu. Waziri Mwalimu anashauri mtu aonapo mojawapo ya dalili hizo awahi katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi wa tiba, kwa kuwa ugonjwa huo unatibika.
Dawa za kifua kikuu zipo na zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kote. Matibabu ya ugonjwa huo hutolewa bure. Ugonjwa unaoua wengi Waziri Mwalimu anasema licha ya kwamba kifua kikuu kinatibika, ndiyo ugonjwa wa pekee wa kuambukiza unaosababisha vifo vingi katika jamii kwa kuwa watu watatu hufariki dunia kila baada ya dakika moja kwa ugonjwa huo.
Anasema takwimu zinaonesha kuwa kwa Tanzania takribani watu 12,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu. “Katika hali hii, ugonjwa wa kifua kikuu katika nchi yetu bado ni janga kubwa hata baada ya miaka 10 tokea Tanzania ilipotangaza kuwa kifua kikuu ni janga la kitaifa kama ilivyoainishwa katika Azimio la Maputo la mwaka 2005,” anasema Mwalimu.
Anahimiza kila mtu katika nafasi yake zikiwemo asasi za kiraia, idara za serikali, mashirika binafsi, wanahabari na wadau wa maendeleo kuunganisha nguvu ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini. Waziri Mwalimu anataja mikoa inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu kuwa ni Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mara, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Tabora na Tanga.
Anasema takwimu za mwaka 2015 zinaonesha kuwa mikoa hiyo imechangia zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu waliogundulika Tanzania Bara na visiwani. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita wastani wa wagonjwa wapya 63,000 wamekuwa wakigundulika na kuanzishiwa matibabu kila mwaka.
“Kwa takwimu hizi kutoka katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya inaonesha wazi kuwa ugonjwa wa kifua kikuu bado ni tatizo kubwa katika nchi yetu. Hali hii imedhihirishwa na matokeo ya utafiti wa kwanza wa kitaifa wa kutathmini kiwango cha maambukizi ya kifua kikuu uliofanyika mwaka 2012/13 ambayo yameonesha kuwa pamoja na juhudi zote zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali, ugunduzi wa wagonjwa wa kifua kikuu ndio umefikia wastani wa asilimia 50 tu,” anasema.
Anasema, matokeo hayo yanaonesha pia kuwa kiwango cha ukubwa wa tatizo la kifua kikuu nchini ni zaidi ya wagonjwa 295 wa kifua kikuu kwa kila watu 100,000. “Hii inamaanisha kuwa kila mwaka wastani wa watu 112,000 huugua ugonjwa wa kifua kikuu. Kwa ugonjwa wa kuambukiza kama kifua kikuu hii inaonesha bado tuna idadi kubwa ya wagonjwa waliopo kwenye jamii ambao tunawakosa kila mwaka ili kuwaweka katika matibabu,” anasema Waziri Mwalimu.
Anasema kwa mujibu wa takwimu za utafiti huo, WHO imeendelea kuiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 22 duniani zenye wagonjwa wengi wa kifua kikuu. Utafiti huo na tathmini nyingine za hivi karibuni zimeonesha ya kuwa wazee na watu wanaoishi katika maeneo ya vijijini na maeneo hatarishi yenye misongamano kama vile kwenye shule za bweni, magerezani na migodini wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata kifua kikuu tofauti na ilivyokuwa ikidhaniwa hapo awali.
Vituo vya afya binafsi
Pia takwimu za wizara za mwaka 2014 zinaonesha kuwa kuna ushiriki mdogo wa vituo vya afya vya binafsi na asasi zisizo za kiserikali katika kutoa huduma za kifua kikuu nchini. “Mathalani, hivi sasa ni asilimia 10 tu ya vituo vyote vya binafsi vinatoa huduma za kifua kikuu na ni asasi chache tu ambazo zinajihisisha na harakati za mapambano ya kifua kikuu katika mikoa na halmashauri zetu,” anasema.
Waziri Mwalimu anatoa rai kwa wamiliki wa vituo binafsi vya kutoa huduma za afya na kupanua zaidi wigo wa kutoa huduma za kifua kikuu katika taasisi zao. Anasema wizara imeanza mchakato wa kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma za kifua kikuu unakuwa ni lazima kwa vituo vyote vya serikali na binafsi. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo katika maeneo wanayoishi na bila ya kikwazo chochote.
Anasema, Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na watoa huduma wote, pamoja na kusimamia ubora wa huduma zote kwa upande wa kifua kikuu. “Tutaendelea kuvipatia vituo binafsi dawa za kutibu kifua kikuu, vifaa vya upimaji na vitendaji bila gharama yoyote kama ilivyo kwa vituo vya umma,” anasema Mwalimu.
Huduma iliyotukuka
Pia anawaagiza watumishi wote walioko kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanatoa huduma za kifua kikuu zilizo na ubora wa hali ya juu na kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wa kifua kikuu wanaogundulika, wanasajiliwa na kuanzishiwa tiba bila kuchelewa.
Anasema usimamizi hafifu na kutozingatia tiba husababisha kuongezeka kwa usugu wa dawa hivyo kuchangia kuwepo kwa kifua kikuu sugu. Tiba ya kifua kikuu sugu ni ghali na huchukua takribani miaka miwili mgonjwa kuweza kupona. Kifua kikuu mashuleni Waziri Mwalimu anasema hivi karibuni katika baadhi ya shule za sekondari za bweni katika mkoa wa Pwani zimekuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Tathmini zilizofanywa na idara za afya na elimu katika baadhi ya shule mkoani Pwani zimebaini kuwa mabweni mengi yana vyumba vidogo na msongamano mkubwa wa wanafunzi. “Mfano katika madarasa mawili ya shule moja walipatikana wanafunzi 16 kati ya wanafunzi 775 wenye kifua kikuu cha kuambukiza. Hali hii ni hatarishi sana na inaweza kuwa chanzo cha maambukizi na kuenea kwa kifua kikuu shuleni,” anasema.
Ni kwa msingi huo, Waziri amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri wafanye ukaguzi kwenye shule zote za bweni za umma na za binafsi ili kubaini mazingira hatarishi yanayosababisha kuwepo kwa maambukizi ya kifua kikuu miongoni mwa wanafunzi. Anasema kazi hiyo iende sambamba na uchunguzi wa kifua kikuu miongoni mwa wanafunzi wote katika shule zote za bweni za msingi na sekondari kwa kutumia fomu za uchunguzi wa ugonjwa huo na upimaji kwa wanafunzi watakaoonesha kuwa na dalili za kifua kikuu.
Amewaelekeza wamiliki wa shule zote kuhakikisha kuwa wanafanya kila jitihada kulinda afya za wanafunzi na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakaguzi wa afya shuleni. Anasema Wizara ya Afya imeanza kushauriana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuweka mikakati endelevu ya udhibiti wa kifua kikuu mashuleni.
Mafanikio Waziri Mwalimu anasema, kuna mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na kifua kikuu, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa tiba bure katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali na binafsi. Anasema, wigo wa tiba umeongezwa na pia huduma za kifua kikuu zimeboreshwa zikiwemo huduma shirikishi za kifua kikuu na Ukimwi.
“Kwa takwimu za 2015 asilimia 91 ya wagonjwa wote wenye maambukizi ya kifua kikuu walipima maambukizi ya VVU na kupata ushauri/nasaha. Pia wagonjwa wenye maambukizi mseto ya kifua kikuu na Ukimwi wanapata dawa za kupunguza makali ya VVU,” anasema.
Anasema, wizara kwa kupitia mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma inaendelea kuhakikisha kuwa dawa za kutibu kifua kikuu na kifua kikuu sugu zinaendelea kupatikana bila malipo. Wizara hiyo pia inakusudia kuweka sera kwa utoaji wa huduma za kifua kikuu ukiwemo uchunguzi na tiba kuwa ni wa lazima katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya yaani vya binafsi na serikali. Anasema ni wajibu wa kila moja kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kuutokomeza kabisa.

No comments:

Post a Comment