Thursday, 28 April 2016

WAZEE WALEMAVU KUPATIWA HUDUMA YA MAJI BURE DAR


SHIRIKA la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), limesema litatoa huduma ya majisafi bure kwa wazee, walemavu na yatima wote ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kuunganishiwa huduma hiyo



Aidha, shirika hilo limesema litajenga vituo vya kunywea maji katika sehemu mbalimbali za jiji hilo hususan maeneo ya stendi ya mabasi ya Ubungo, Buguruni Chama, Magomeni Mapipa na stendi ya zamani ya mabasi yaendayo mikoani ya Kisutu.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja, wakati akizungumza na wanaharakati wa Mtandao wa Kijinsia (TGNP), jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ifikapo Desemba 31, mwaka huu watahakikisha kampeni yao ya ‘Mama Tua Ndoo ya Maji Kichwani’ inawafikia wakazi wengi wa Dar es Salaam hususan wa hali ya chini
“Mimi pamoja na menejimenti yangu tunaenda kumtua mama ndoo ya maji kichwani mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kwani maji yatakuwa mengi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam pamoja na Pwani,” alisema Luhemeja.
Kwa upande wao TGNP, wamepongeza juhudi zinazofanywa na shirika hilo, pamoja na juhudi zao za kusaidia jamii inayoizunguka.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Kampeni ya Mama Tua Ndoo Kichwani kutoka TGNP, Martha Samwel, aliitaka Dawasco kuhakikisha inapeleka huduma ya majisafi na salama katika sehemu zote muhimu ikiwamo shuleni na hospitalini ili kumpunguzia mwanamke adha ya kutafuta maji kutoka umbali mrefu pamoja na kumwepusha mwanamke kubakwa.
NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!