Pages

Thursday 7 April 2016

WATANO WAFA KWA KUANGUKIWA NA NYUMBA DAR

Wakazi wa Kawe wakiangalia nyumba iliyobomoka

Dar es Salaam. Watu watano wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi kuangukiwa na kifusi na mti wakiwa wamelala, ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa karo la majitaka la nyumba ya jirani iliyo juu ya mlima.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa karo hilo na kwamba maji yaliyotoka kwa kasi yaling’oa mti, kifusi na kisha kuifunika nyumba ya jirani iliyojengwa bondeni na kusababisha vifo hivyo.
Alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri katika Mtaa wa Ukwamani Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, na waliokufa ni Ephraim Manguli (47), watoto wake Daniel Ephraim (5) na Frederick Ephraim (1). Wengine ni mjukuu wa mwenye nyumba hiyo, Greyson Clarence (3) pamoja na msichana wa kazi za ndani aliyetambulika kwa jina moja la Maria.
“Majeruhi ni pamoja na Emilia Nakiete (19) aliyejeruhiwa mkono wa kulia na kidevu na Fadhili Fariji (8) aliyejeruhiwa mguu wa kulia. Wengine watatu walitibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa. Majeruhi wawili bado wamelazwa na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo,” alisema Kamanda Fuime.
Baada ya kutafutwa, mmiliki wa nyumba hiyo Blandina Clarence Akilizao (49), alisema nyumba yake ilikuwa na wapangaji sita wenye familia, huku familia yake ikiwa na watu saba.
“Ndani ya nyumba nilikuwa na watoto wawili, wadogo zangu wawili na wajukuu wawili, pia kulikuwa na familia tano zilizokuwa na watu 17 jumla,” alisema mama huyo kwa uchungu.
Blandina alisema nyumba hiyo aliachiwa na mumewe aliyefariki dunia mwaka 2000 na kwamba hivi sasa hana msaada wowote, kwani akiba ya fedha aliyokuwa nayo kiasi cha Sh200,000 imefukiwa na kifusi na hajui namna ya kuipata.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mpangaji, Msafiri Nyamolelo alisema ajali hiyo ilitokea ghafla na kabla ya ukuta kuanguka, ulisikika mlipuko na baadaye kelele za maji, kisha kishindo kikubwa juu ya paa.
“Karo lilipasuka na kwa kuwa ardhi hiyo hapo juu kwa muda mrefu ni dampo lenye mifuko mingi, ardhi ilikuwa imeoza, hivyo miti mikubwa ambayo iliota huko iling’oka baada ya karo kupasuka na kutua juu ya paa la nyumba sambamba na udongo kutoka juu nao ukafunika,” alisimulia Nyamolelo.
Akizungumzia tukio hilo, Katibu Mtendaji wa Mtaa wa Ukwamani, Kata ya Kawe Kassim Mbezi alisema chanzo cha ajali ni kupasuka kwa karo la choo na maji yaliyomwagika ambayo yaliuzoa mti huo na kifusi kilisombwa na kuifunika nyumba hiyo.
“Tulipofika eneo la tukio tuliwakimbiza majeruhi wote Mwananyamala, lakini kwa bahati mbaya walifariki baada ya kufika mapokezi wote walitoka wakiwa bado wanahema, lakini ilipofika saa tatu asubuhi tukaambiwa kwamba kulikuwa na ‘house girl’ hivyo baada ya kufukuafukua tukaupata mkono na baadaye kuufikia mwili mzima, huyu tulimtoa akiwa tayari amefariki,” alisema Mbezi.
Mbezi alitoa wito kwa wakazi wa bonde hilo kuhama kwa kuwa gema bado linaonekana na ni hatari na changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na maafa kabla ya kutokea.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment