Saturday 16 April 2016

SUDAN KUSINI SASA RASMI EAC

RAIS John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, Salva Kiir, wamesaini mkataba wa kuiwezesha nchi hiyo kuwa mwanachama kamili wa jumuiya hiyo.


Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kihistoria iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli aliipongeza nchi hiyo na kusema anajivunia tukio hilo la kihistoria kutokea wakati Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa EAC kwa kuwa ukurasa mpya wa ushirikiano na uhusiano na nchi hiyo umefunguliwa.
Aliongeza kuwa, Sudan Kusini kihistoria imekuwa na uhusiano ya karibu na nchi za Afrika Mashariki katika nyanja mbalimbali, ikiwemo mwingiliano wa tamaduni, ushirikiano wa kibiashara na uchumi na ukaribu wa kijiografia.
Aidha, alieleza kuwa kujiunga kwa Sudan Kusini kwenye EAC kunaifanya Jumuiya kuwa na soko kubwa lenye takriban watu milioni 160. Aliongeza kuwa, ili Jumuiya hiyo iwe na maendeleo endelevu, suala la kudumisha amani ni la msingi huku akiwahimiza Sudan Kusini kuendeleza juhudi kwenye mazungumzo ya amani.
‘’Dhana ya mtangamano ni kukuza biashara, uwekezaji na miundombinu ili kujiletea maendeleo endelevu katika Jumuiya yetu, hivyo nahimiza umuhimu wa nchi wanachama kudumisha amani ili kufikia malengo tuliyojiwekea,‘’ alisema Magufuli aliyempongeza Kiir kwa jitihada za kuhakikisha nchi yake inajiunga EAC haraka, ambapo miezi minne baada ya Uhuru wake iliomba kujiunga na Jumuiya hiyo na kufanikiwa kuupata uanachama kamili baada ya miaka mitano.
Naye Kiir alieleza kufurahishwa kwake na hatua iliyofikiwa na nchi yake ya kuwa mwanachama kamili wa EAC. Aidha, alimshukuru Rais Magufuli na marais wa nchi zote wanachama kwa kuiunga mkono nchi yake kwa kauli moja.
Kiir aliongeza kuwa uamuzi wa nchi yake wa kujiunga na jumuiya ni wa dhati na kwamba una nia ya kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla, ambapo nchi yake imeshaanza kufanyia mabadiliko mifumo mbalimbali kwenye Serikali yake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za mtangamano ikiwemo kuunda Wizara inayoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Pia, Rais Kiir ametangaza kufunguliwa rasmi kwa Ubalozi nchini na amemteua Balozi Mariano Deng Ngor kuwa Balozi wa Sudan Kusini Tanzania. Sudan Kusini ilipata uhuru wake Julai 9, 2011 na iliomba kujiunga na EAC Novemba mwaka huo kabla ya Machi mwaka huu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Rais Magufuli kutangaza kuipa nchi hiyo uanachama kamili wakati wa Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi wa EAC Arusha.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!