Saturday 2 April 2016

SABA KIZIMBANI KWA KULA NJAMA KUTOROSHA TUMBILI 61


WASHTAKIWA saba wa kesi ya kusafirisha wanyamapori hai 61 aina ya tumbili kwenda nchini Armenia, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi na kusomewa mashtaka manne likiwamo la uhujumu uchumi.


Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Joackim Tiganga, mawakili wa serikali watatu, Wankyo Saimon na Salim Msemo, wakiongozwa na Abdalah Chavula walieleza mahakama hiyo kwamba washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa.
Wakili Saimon aliieleza mahakama hiyo kuwa shtaka la kwanza la uhujumu uchumi linawahusu washtakiwa wote, ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi Wanyamapori, Dk Charles Mulokozi na Ofisa Mfawidhi Kanda ya Kaskazini anayehusika na matumizi endelevu ya wanyamapori nchini (CITES), Nyangabo Musika.
Wengine ni maofisa wanyamapori, Martina Nyakangara na Very Antony, wafanyabiashara Iddy Misanya na Artem Vardanian na wa mwisho ni Meneja wa Hoteli ya North Sea, Eduard Vardanyan.
Alieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Februari 1 hadi Machi 22 mwaka huu wakiwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro walikula njama ya kutenda kosa la kusafirisha nyara za serikali.
Wakili Saimon akisaidiwa na wakili Msemo walisema shtaka la pili linawahusu washtakiwa wote kwa pamoja ambapo washtakiwa wengine wakiwa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutumia nyadhifa zao walishirikiana kula njama za kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Armenia.
Walidai kuwa katika shtaka hilo washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa na njama za kusafirisha wanyama hao 61 wenye thamani ya dola za Marekani 7,320 sawa na kiasi cha Sh 15,872,029 bila kibali cha Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!