Wednesday 13 April 2016

OMBA OMBA KUKAMATWA

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameamuru watu wanaoomba mitaani katika maeneo mbalimbali jijini wakamatwe, waache kufanya shughuli hiyo isiyo halali. Ameagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kuanzia Jumatatu, waanze kuwakamata ‘ombaomba’ hao .


Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam, alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisema watu hao wanaosimama barabarani katika maeneo ya jiji, muda wao umefika kikomo kwani maeneo hayo si sahihi kwa ajili ya shughuli hiyo.
Alisema ni vyema watu hao wakaenda katika vituo mbalimbali vilivyoanzishwa na wasamaria kwa ajili ya wenye uhitaji badala ya kusimama mitaani katika maeneo ya jiji kuomba. “Nimegundua kuwa asilimia 80 ya ombaomba wamekuja Dar es Salaam na nauli zao hivyo naomba warudi kwa nauli zao na hao asilimia 20 waende kwenye hivi vituo,” alisema Makonda.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwataka ombaomba hao kuondoka wenyewe bila kusubiri kuondolewa na Polisi. Pia aliwataka wenyeviti wa Serikali za mitaa kuanza wenyewe kuwaondoa kwa kusema kwani kuendelea kuwaacha kunasababisha kujaa na kuleta kero.
“Msisubiri Polisi wafanye kazi hiyo pekee yao, lazima na wenyeviti mshiriki kuwaondoa na ninaamini tukishirikiana tutawaondoa wote na jiji litabaki shwari,” alisema Sirro. Agizo hilo la kuwakamata wanaoomba mitaani, limekuja baada ya hivi karibuni Makonda kupiga marufuku wapitia njia kuwapatia fedha watu hao, ambao wengi wamekuwa wakitumia watoto wadogo kuomba.
Agizo la kutaka omba omba wakamatwe kuondokana na vitendo hivyo jijini, limewahi kutolewa pia na aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba ambaye aliamuru waondolewe warudishwe wanakotoka.
Hata hivyo jiji hilo la Dar es Salaam limeendelea kugubikwa na wimbi la watu hao wanaoomba ambao baadhi wamekuwa wakitumia watoto wadogo ambao huvizia watu na kuwaomba fedha.
Bomoa bomoa Katika hatua nyingine, Makonda amewataka watu wote waliojenga magorofa bila maeneo ya maegesho ya magari, kufika katika ofisi yake Jumatatu kujadili kubomoa majengo yao au kulipa faini na kujenga maegesho hayo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!