Saturday, 2 April 2016

MBUNGE MWINGINE KORTIN KWA RUSHWA



Dar es Salaam. Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka mawili; kuomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Felchesmi Mramba na kumshinikiza kiongozi huyo kuwafungia umeme ndugu na rafiki yake.



Mbunge huyo ambaye hivi karibuni aling’olewa uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) na Spika, Job Ndugai katika mabadiliko aliyosema ni ya kawaida, anakuwa mbunge wa nne kufikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma rushwa. Juzi, wabunge watatu; Kangi Lugola (Mwibara), Sadiq Murad (Mvomero) na Victor Mwambalaswa (Lupa) walifikishwa na kusomewa shtaka la kuomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Gairo, Morogoro, Mbwana Magote.
Ndassa alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Dennis Lekayo ambaye alidai mbele ya Hakimu Mkazi Emillius Mchauru kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam kinyume cha kifungu cha 15 (2) cha Sheria ya Takukuru.
Katika shtaka la kwanza, alidai kuwa siku ya tukio, mshtakiwa huyo kwa nafasi yake ndani ya PIC, aliomba rushwa ya Sh30 milioni kutoka kwa Mramba kamati hiyo iweze kutoa hati safi ya ukaguzi wa ripoti ya hesabu za mwaka 2015/2016 kwa shirika hilo.
Katika shtaka la pili, alidai kuwa siku hiyohiyo, mshtakiwa huyo alimshinikiza Mramba kumpatia umeme ndugu yake Ndassa, aliyetajwa kwa jina la Matanga Mbushi na rafiki yake Lameck Mahewa ili kamati yake iweze kutoa hati safi ya ukaguzi wa ripoti ya hesabu ya mwaka 2015/2016 kwa shirika hilo.
Mshtakiwa alikana mashtaka na Wakili Lekayo aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo akaiomba ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Pia, wakili huyo alisema dhamana ya mshtakiwa iko wazi lakini akaiomba Mahakama iiwekee masharti magumu ili asiweze kuingilia uchunguzi unaoendelea kufanywa.
Hata hivyo, Wakili Erasto Mgenge anayemtetea Ndassa aliiomba Mahakama itoe dhamana isiyo na masharti magumu kwa sababu hiyo ni haki ya kila mtu.
Katika hilo, Hakimu Mchauru alimtaka Ndassa kujidhamini mwenyewe na kuwa na mdhamini mmoja atakaye saini hati ya dhamana ya Sh10 milioni kila mmoja pamoja na yeye mshtakiwa kujidhamini mwenyewe masharti ambayo aliyatimiza na kuachiwa huru kwa dhamana.
Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 18 itakapotajwa tena.

Ilivyokuwa mahakamani
Mbunge huyo alifikishwa mahakamani hapo saa 3.45 asubuhi akiwa katika gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser na kwenda kuketi kwenye benchi akisubiri kupandishwa kizimbani.
Ndassa aliyekuwa amevalia kaunda suti nyeusi na viatu vyeusi, alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka saa 4.37 asubuhi.
Alitoka mahakamani hapo saa 4.52 asubuhi akiwa ameongozana na wakili wake Mgenge na kusema kwa kifupi; “...Hata kama tunatafutana sio hivi!” kisha akaingia katika gari lake aina ya Toyota Prado rangi ya silva na kuondoka.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!