Thursday, 7 April 2016

Materu, mshona viatu, mkulima anayetafuta shahada ya uzamivu



Materu akiwa katika biashara zake za kuuza

Siku zote kilio cha vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu nchini kimekuwa ni ukosefu wa ajira.
Kwa kuwa ndoto ya wengi ni kupata kazi, malazi bora, magari na hata fursa za kufanya anasa, ukosefu wa ajira umekuwa kikwazo kikubwa cha kutimiza ndoto walizonazo.



Kimsingi, mawazo na mtazamo kuhusu maisha wakiwa vyuoni, huwa tofauti na hali halisi wanapohitimu masomo.


Wengi hubaki wakizunguka na bahasha zenye barua ya maombi ya kazi kwenye ofisi mbalimbali bila mafanikio na hivyo kuishia kulalamikia ugumu wa maisha kwa kukosa ajira.
Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha EATV, Elikunda Materu anasema alianza kufikiria kujiajiri tangu akiwa kidato cha kwanza.
“Kwa sababu nilikulia kijijini hivyo nikajifunza kushona viatu, nilipoanza kidato cha kwanza niliamua kuwa mshona viatu vya wanafunzi wenzangu,” anasema.
Tangu hapo Materu akajulikana kwa jina la mshona viatu. Wanafunzi wote walioharibikiwa viatu walikimbilia kwake naye hakuwaangusha kwani alitumia vyema siku za mwisho wa wiki kutengeneza viatu na kujipatia chochote.
Baada ya safari ndefu ya kuishi kwa madhila kama mtoto anayetoka familia masikini, sasa Materu ni msomi wa shahada ya uzamili, huku akiwa njiani kuanza masomo ya shahada ya udaktari wa falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Nje ya taaluma, Materu ni mkulima hodari wa mazao ya mbogamboga na matunda. Pia, anamiliki mgahawa uitwao ‘Intelligent Fast Food’ uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Kujiunga chuo kikuu
Siku zote alitamani kuwa mwandishi wa habari, hivyo akaamua kusomea taaluma hiyo.
Mwaka 2008 alijiunga na Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) zamani kilikuwa kikiitwa Tumaini akianza masomo yake ya uandishi wa habari.
Kwa kuwa alikuwa miongoni mwa wanafunzi waliobahatika kupata mkopo wa elimu ya juu, maisha yake yalikuwa mepesi tofauti na awali.
“Sikuwa muoga wa kuthubutu, nilipopata mkopo wangu kwa mara ya kwanza nilichukua baadhi ya fedha nikazitumia kama mtaji,”anasema.
Wakati huu hakuendelea kushona viatu. Akiwa mwaka wa kwanza, alianzisha biashara ya mitumba ya viatu na nguo akiwauzia wanafunzi wenzake.
“Biashara yangu iliongezeka siku hadi siku, nikapata faida kubwa iliyoniwezesha kununua shamba katika kijiji cha Mgongo kilicho karibu na chuo,” anasema.
Jitihada zake zilimfanya awe miongoni mwa wanafunzi waliopata kazi baada ya kuhitimu masomo yake.
“Nilipata kazi kwenye redio moja ya mjini Iringa, nikitangaza kipindi cha Kiingereza kuanzisha saa 11.00 hadi saa 12.00 jioni. Kazi haikunibana hata kidogo, wakati huu nilipata muda mwingi wa kufanya biashara zangu,” anaeleza.
Mbali na utangazaji, Materu alikuwa mtaalamu wa kompyuta na Tehama akikisaidia kituo hicho cha redio.
“Ukiniuliza niliwezaje kufanya hayo yote kwa pamoja, nitakujibu kuwa nilikuwa na njaa ya mafanikio na nilifahamu mafanikio yoyote huja kwa jitihada na kuwa na mipango sahihi,” anasema.
Hakutosheka na hali hiyo, akiwa bado kazini alijiunga na masomo ya shahada ya uzamili katika masoko na ujasiriamali huku akiendelea na kilimo cha mahindi na mbogamboga.
“Nililima matunda, mbogamboga na mahindi. Niliuza mazao yangu sokoni na niliajiri vijana 10 ambao walikuwa wakinisaidia kazi za shamba na biashara zangu za mitumba,” anasema na kuongeza:
“Shahada yangu ya pili nimesoma kwa kujilipia ada mwenyewe, wakati huu sikuwa na wasiwasi juu ya ugumu wa maisha.’’
Moja ya vitu vinavyomshangaza ni pale anapowaona vijana wenzake wakilia ugumu wa maisha kwa kukosa kazi, hasa katika nchi yenye fursa ambazo kwa hakika zinahitaji uthubutu na dhamira ili kuzifaidi.
Baadaye alipata kazi ya utangazaji katika kituo cha televisheni ya EATV akiwa mtangazaji na mwandishi wa habari.
“Mpaka sasa nafanya kazi kwenye redio na televisheni hasa kwenye kipindi maarufu cha Hotmix, naamini naweza kuwabadilisha vijana wenzangu kupitia taaluma yangu, wasifikirie kuajiriwa. Hakuna aliyeajiriwa akafanikiwa kimaisha,” anasema.
Mtazamo kuhusu kilimo
Anasema kuwa licha ya sekta ya kilimo kukabiliwa na changamoto nyingi, aliamua kuwekeza huko bila kujali athari zake.
“Napenda kuwatumia wataalamu wa kilimo kunishauri, bila elimu ya uhakika huwezi kufanya kilimo cha kisasa,” anasema.
Ndoto yake ni kulima mazao ya chakula ambayo atakuwa akiyatumia kwenye mgahawa wake.
Anasema mtaji wa biashara zake alizofungua jijini Dar es Salaam ulitokana na zile alizokuwa akifanya mkoani Iringa.
“Nimefanikiwa kumiliki nyumba nzuri, Kwa sasa ninamiliki kilimo, nyumba, gari, najikimu pamoja na kuendesha biashara nyingine ikiwamo katika sekta ya mavazi,” anasema.
Ushauri wake
Materu anaishauri Serikali kubadilisha mitalaa ya elimu kutoka ile ya nadharia kwenda katika mitalaa ya vitendo.
Anasema kinachowakwaza wahitimu wengi ni kwa sababu hawajaandaliwa kupambana na changamoto za kimaisha kupitia stadi za maisha, hivyo wengi wanasubiri kuajiriwa.
“Bibi yangu alinifundisha kushona viatu tangu nikiwa mdogo, nilijifunza elimu ya kujitegemea kutoka kwa wazazi wangu na leo hii sitateseka kutafuta kazi kama wenzangu,” anaeleza.
Anasema ni aibu kwa mwanafunzi kuhitimu kidato cha sita akiwa hajui hata kushona nguo yake iliyochanika.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!