Monday, 4 April 2016

MAMBOYA: KITUO CHA MAPUMZIKO MSAFARA WA WATUMWA

Magofu ya ofisi ya serikali ya utawala wa kikoloni.
KIJIJI cha Mamboya kilichopo tarafa ya Magole, katika wilaya Kilosa, Morogoro ni miongoni mwa maeneo ya historia yaliyotumiwa kama mapumziko ya muda ya watumwa waliokuwa wakitokea Kigoma Ujiji, Tabora na mikoa mingine ya Kanda ya Kati kuekelea Soko Kuu la Biashara ya Watumwa, Bagamoyo.
Wafanyabiashara wa pembe za ndovu waliwatumia watumwa kubeba mizigo yao wakitokea mikoa ya Bara, kwenda katika Soko Kuu la Watumwa mjini Bagamoyo. Wafanyabiashara hao wa Kiarabu wakiwa na pembe za ndovu na watumwa walikuwa wakitoka maeneo ya Ziwa Tanganyika hususan Kigoma Ujiji na Tabora na wakifikia eneo la Mamboya mkoani Morogoro wanapumzika ili kupata nguvu za kuelekea Bagamoyo na wengine kusafirishwa kwenda Zanzibar.
Biashara ya Watumwa ilianza kufanyika mwanzoni mwa karne ya 19 na Mji wa Bagamoyo ulikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara hiyo. Kijiji cha Mamboya ingawa bado hakina umaarufu wa kihistoria yalikuwa ni mapito ya wafanyabiashara wa Pembe za Ndovu na Watumwa walibebeshwa mizigo hiyo wakitoka mikoa ya Ziwa Tanganyika kwenda Bagamoyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazee wa kijiji cha Mamboya, Kayanda Kagoso na Kaniki Mathias wanaeleza kuwa kijiji hicho kina historia kuu mbili ambazo ni ujio wa wamisionari wa kwanza wa Kanisa la Anglikana na pili kuwepo kwa njia ya watumwa. Kagoso na Mathias wanasema kuwa watumwa hao baada ya kupita sehemu mbalimbali walipofika eneo la Mamboya walipumzishwa kwa muda kabla ya kuendelea na safari.
“Kijiji cha Mamboya kina historia ya kipekee, kwanza ujio wa kwanza wa wamisionari wa Kanisa la Anglikana walijenga kanisa lao hapa na pili watumwa waliokuwa wakisafirishwa walipitishwa hapa na waliokuwa dhaifu waliachwa eneo hili la Mamboya,” anasema Kagoso. Kagoso anasema watumwa waliokuwa bado na nguvu waliendelea na safari wakipitia vijiji mbalimbali vikiwemo vya Kitete, Msowero, Rudewa, Kimamba na kufikishwa eneo la Kilakala Morogoro kabla ya kuelekea Bagamoyo.
Mzee Kagoso anasema Mwarabu wa kwanza kufikia katika kijiji cha Mamboya alikuwa ni Sultani Majid na inahisiwa kwamba alifika maeneo hayo kati ya miaka ya 1870, wakati huo biashara ya watumwa ilipokuwa imeshamiri katika mwambao wa Pwani ya Afrika Mashariki. Kagoso anasimulia kuwa watumwa walipofika kwenye jabali la jiwe linalofahamika kwa jina la Mlima wa ‘Mele’ walipumzishwa kwa muda kabla ya kuendelea na safari yao.
Mele ni neno la labila la Wakaguru likiwa na maana ya maziwa.’ Pia anaeleza kuwa pamoja na sehemu hiyo kuwa ni mapito ya biashara ya watumwa, jabali la jiwe hilo pia palitumika kama kituo cha kuwakutanisha wajumbe wa baraza kutolea mashauri na adhabu kwa wakosaji. Kagoso pia anasema Wanyamwezi waliotoka Tabora kwenda Bagamoyo walioshindwa kuendelea na safari waliachwa katika kijiji cha Mamboya.
“Katika Msafara wao walikuwa watu wengi wakiwemo wazee na vijana, na walipofika Kituo cha Rubeho, wilaya ya Kilosa, walipokelekwa mlima wa Mamboya eneo la Nyhuwei Ngholongo, sehemu inayoitwa Maduma. Kagoso ambaye amerithishwa simulizi hizo kutoka kwa baba zake ambao wameshafariki miaka mingi iliyopita, anasema, Wanyamwezi kutoka Tabora waliobakia Mamboya walikuwa chini ya uongozi wa Minuka Limtu.
Anasema kizazi hicho kilichoachwa wakati wa utumwa sasa kimetoweka na zimeachwa koo za familia zao na wengi wenye asili ya mikoa ya Ziwa Tanganyika na Tabora hawafahamu chimbuko la historia ya biashara ya utumwa na ya kijiji cha Mamboya. Kumbukumbu na maandiko ya kihistoria kuhusiana na biashara hiyo, ilikuja kuzuiliwa mnamo mwaka 1873 na kukomeshwa kabisa ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19.
Mzee Kagoso, pia anaelezea kwa kina umaarufu mwingine wa kijiji hicho juu ya historia ya Kanisa la kwanza la Anglikana ambalo baadaye lilienea katika mikoa mbalimbali nchini. Hivyo anasema utawala wa Mdewa Chimola wa Maluwe katika kijiji cha Mamboya mnamo mwaka 1877 ulishuhudia mzungu wa kwanza aliyetajwa kwa jina la Msitias. Yeye alikuja kueneza Injili ambapo alipokelewa na Mdewa Chimola.
Baada ya kupokelewa mzungu huyo alijenga kanisa la kwanza Mlimani Maluwe mwaka 1879 na baadaye wazungu wengine waenezaji wa Injili walifika eneo la Mamboya na walishiriki kufungua shule ili waumini wajifunze kusoma, kuandika na kuhesabu. Pamoja na urithi wa historia zinazofaa kuhifadhiwa kwa ajili ya kumbukumbu za kizazi cha sasa na kijacho, kijiji cha Mamboya kipo nyuma kimaendeleo yanayochangiwa na ubovu wa Miundombinu ya Barabara. Kijiji cha Mamboya kipo umbali wa kilometa 10 kutoka barabara kuu ya Morogoro- Dodoma eneo la kijiji cha Magumbike, wilayani Kilosa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!