MAMA wa familia iliyouawa katika ajali ya kifusi iliyoua watu watano jijini Dar es Salaam wakiwemo baba na watoto wake wawili na binti wao wa kazi, Gaudensia Ephraim alinusurika baada ya yeye kudamkia katika biashara yake ya kukaanga maandazi.
Mume wa Gaudensia, Ephraim Manguli (47), watoto wake wawili Danford (5) na Fredy Ephraim (2) pamoja na binti wao wa kazi aliyetambulika kwa jina moja la Mariam, walikufa baada ya nyumba walimokuwa wakiishi kufunikwa na kifusi kwenye eneo la Kawe katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam juzi asubuhi.
Baba mzazi wa Ephraim, Mzee Philemon Manguli alisema kama isingekuwa biashara hiyo na mkwewe angefariki katika ajali hiyo iliyotokea alfajiri ya Jumatano Aprili 6, mwaka huu na kusababisha vifo hivyo.
Alisema Gaudensia hufanya biashara ya kukaanga maandazi hivyo alidamka alfajiri kwenda katika biashara yake na wakati yupo huko alitaarifiwa kutokea kwa ajali hiyo na alipofika nyumbani akakuta nyumba imeanguka na familia yake imefukiwa.
“Mkwe wangu yeye hufanya biashara ya kukaanga maandazi, na wakati ajali inatokea tayari alikuwa katika biashara yake mtaa wa pili na alipoarifiwa na kurudi nyumbani ndio akakuta ajali hiyo ambayo iliua mumewe, watoto wawe wawili, binti yake wa kazi pamoja na mjukuu wa mwenye nyumba walimokuwa wakiishi,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya mkwewe ambaye hakuwa katika hali nzuri ya kuzungumza, Manguli alisema huenda mkwewe angefariki kama angekuwa ndani alfajiri ile, ila biashara yake ndiyo imemuokoa.
Manguli ameliambia gazeti hili kuwa msiba huo wa kijana wake aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya ulinzi ya Mahela Night Wash imempa jeraha ambalo hatokaa kulisahau maishani mwake.
“Siamini hadi sasa kama mwanangu amefariki pamoja na wajukuu zangu Danfod na Fredy, lakini ndio hivyo ni mapenzi ya Mungu, ila sijui la kufanya,” alisema kwa huzuni Mzee Manguli.
Alisema jambo lingine la kusikitisha kwao ni namna misiba ilivyomuandama kwani wiki moja iliyopita hapo hapo nyumbani kwake alifariki mdogo wake na kusafirisha hadi kijijini kwao Mahenge mkoani Morogoro kwa maziko.
“Ijumaa iliyopita mimi na marehemu mwanangu, tumerudi kutoka Mahenge kumzika baba yake mdogo, na leo tena matanga yamerejea hapa hapa kwangu,” alisema Manguli.
Kuhusu taratibu za mazishi, msemaji wa familia hiyo, Mchungaji Geoffrey Masanju alisema maandalizi yanaendelea na kutokana na hali ngumu ya familia hiyo kwa sasa kutokana na kufululiza kwa misiba hiyo, wanatarajia kuzika Jumamosi katika makaburi ya Kinondoni.
“Mazishi yanataraji kufanyika Jumamosi katika Makaburi ya Kinondoni, lakini kubwa zaidi tunasubiri michango kutoka kwa ndugu na jamaa pamoja na Ofisi ya Mbunge wa Kawe ili kufanikisha mazishi haya,” alisema Mchungaji Masanju.
Masanju alisema mawasiliano baina yao na wazazi wa binti wa kazi aliyemtaja kwa jina la Mariam mwenyeji wa Musoma mkoani Mara yanaendelea ili kufahamu kama naye atazikwa pamoja na wenzake au atasafirishwa ijapokuwa uwezo wa kusafirisha kama wao kwa sasa ni mdogo.
Alisema msaada mkubwa wanaoutegemea wa kufanikisha maziko hayo ni kutoka kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye tangu kutokea kwa tukio alituma mwakilishi wake ili kusaidiana na familia.
No comments:
Post a Comment