Sunday, 3 April 2016
MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA NCHINI
Serikali imesema maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi yamepungua kutoka asilimia 10 kwa mwaka 1990 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012, kutokana na kazi ya uhamasishaji wa kujikinga na maambukizi ya zinaa zinazofanywa na taasisi binafsi nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangala, aliyaeleza hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua ofisi za Taasisi ya T-Marck na ghala la kuhifadhia zana za kujikinga na maambukizi ya zinaa kama condom za kike na kiume na vidonge vya uzazi wa mpango.
Alisema serikali pia inaendelea kushirikiana na mashirika binafsi katika kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya uzazi wa mpango na kumaliza tatizo la maambukizi ya magonjwa ya zinaa pamoja na mimba zisizotarajiwa nchini.
"Asilimia 66 za kazi zinazofanywa na madaktari nchini ni kinga na uhamasishaji wa kuzuia maambukizi," alisema Dk. Kigwangala.
Alisema ni "kazi ambayo pia inayofanywa na taasisi binafsi kwa kushirikiana na serikali na asilimia 34 pekee ni kazi za matibabu zinafanywa na madaktari.
"Hivyo kama serikali tunaunga mkono juhudi hizi za taasisi binafsi za kutoa elimu ya uzazi na kumaliza maambukizi."
Aidha, Dk. Kigwangala alisema serikali inaendelea na utaratibu wa kuzikagua taasisi binafsi ambazo hazifanyi kazi kwa mujibu wa usajili walioomba ili kuzifungia.
Alisema serikali ya awamu ya tano haiwezi kuendelea kuwa na taasisi binafsi za kiujanja ujanja ambazo zimepata usahili lakini hazijulikani kazi zinazofanya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa T-Marc, Dayana Kisaka, alisema uzinduzi wa ofisi hizo na ghala la kuhifadhia dawa utarahisisha utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema tangu kuanza kutoa huduma hizo nchini mwaka 2004, tayari wameshatoa huduma ya condom za kiume aina ya dume milioni 15 na condom za kike aina ya Lady pepeta milioni 6.9 pamoja na vidonge vya uzazi wa mpango milioni 15.2.
Utoaji huo una lengo la kusaidia jamii kuondokana na maambukizi pamoja na kuzuia mimba zisizotarajiwa, alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment