Saturday 9 April 2016

KIWANDA KINGINE CHA GESI CHAZINDULIWA

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limezindua kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Songosongo wilayani Kilwa mkoa wa Lindi chenye uwezo wa kupokea futi za ujazo milioni 70 kwa siku kutoka kwenye visima na kwa kuanzia kitapokea futi za ujazo milioni moja.


Kwa sasa wanafanya majaribio hadi kufikia Juni 30, mwaka huu futi zote za ujazo milioni 70 zitakuwa zimeungana na gesi inayotoka Mnazi Bay katika eneo la Somangafungu na kuanza kusafirishwa kwa bomba la gesi kwenda jijini Dar es Salaam.
Akizindua mtambo huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio, alisema kufikia Juni 30, mwaka huu bomba la gesi litasafirisha gesi ya futi za ujazo bilioni 10.27 kwenda jijini Dar es Salaam.
Dk Mataragio alisema mitambo ya Songosongo ina uwezo wa kuchakata futi za ujazo milioni 140 katoka visima vinne na Kisima cha Kiliwani -North kitatoa gesi futi za ujazo milioni 20 hadi 30 kwa siku.
“Kwa kuwa mitambo yetu bado ni mipya kitaalamu hatuwezi kuingiza gesi nyingi kwa wakati mmoja, hivyo gesi huingizwa katika mitambo kidogo kidogo kupima uwezo wake lakini mpaka mwezi Juni gesi yote itakuwa imefika jijini Dar es Salaam kwa kutumia bomba la gesi,” alisema Dk Mataragio.
Alisema majaribio yanafanyika ili kupima uwezo wa mitambo kuhimili kiwango cha gesi inayoingia na kuichakata katika viwango vinavyotakiwa na ujazaji wa gesi kwenye bomba na kupima mgandamizo wa gesi.
Pia kuisukuma kwenda Somangafungu ambapo itakutana na ile inayotoka Madimba na kisha kuweka katika mgandamizo sawa na kusafirishwa hadi Dar es Salaam.
Dk Mataragio alisema mitambo hiyo ya kuchakata gesi ya Songosongo inayomilikiwa na serikali kwa asilimia 100, kwa sasa itakuwa ikipokea gesi kutoka katika vitalu viwili ambavyo ni Kiliwani inayomilikiwa na Ndovu Resources na Songosongo inayomilikiwa na Pan African Energy Tanzanie-PAET.
Alisema miundombinu hiyo ya Songosongo na ile ya Madimba iliyopo mkoani Mtwara ilizinduliwa rasmi Oktoba 2015 na Rais mstaafu Jakaya Kikwete lakini ya Songosongo ilichelewa kukamilika kutokana na miundombinu ya kisiwani kuchelewesha kufika kwa malighafi za ujenzi.
Mkurugenzi huyo alisema baada ya uzinduzi wa mtambo huo, changamoto waliyobaki nayo ni kuongezeka kwa gesi wakati wakiwa na mteja mkubwa mmoja tu ambaye ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao wanatumia kiasi kidogo huku viwanda na wateja wa majumbani wakiwa wachache.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, wanajipanga kusambaza gesi katika maeneo ya majumbani na viwandani Dar es Salaam na katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda (EPZA) ya Mkuranga, Bagamoyo na Ruvu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!