Pages

Monday, 11 April 2016

KIKWETE ATUNUKIWA TUZO YA MALARIA NEW YORK

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akiwa na Ray



New York. Katika kutambua mchango wake wa mapambano dhidi ya Malaria, Rais mstaafu Jakaya Kikwete juzi alitunikiwa tuzo maalumu kwa kusimamia muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya ugonjwa huo.


Kikwete alitunukiwa tuzo hiyo ya White House Summit Awards katika hafla ya kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa kampeni za kidunia za kutokomeza Malaria (Malari No More).
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini New York, Marekani, Kikwete alisema ushirikiano uliopo baina ya nchi za Afrika, mashirika ya kimataifa na kampuni binafsi utasaidia kumaliza ugonjwa huo.
“Ugonjwa wa malaria unatakiwa kutokomezwa barani Afrika kwa sababu unapoteza maisha ya watu wengi, bajeti kubwa katika huduma ya afya inatumika katika kuutibu. Unaweza kutokomezwa. Kama Zanzibar wameweza kutokemeza malaria, mkienda Zanzibar kutembea msiwe na wasiwasi kupata malaria,” alisema.
Akijibu swali la nini kimechangia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na malaria, Kikwete alitaja sababu kadhaa, ikiwamo utashi wa kisiasa wa kusimamia na kuongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
“Mchanganyiko wa mambo matatu umesaidia kupunguza idadi ya watoto wanaofariki kwa malaria, lakini pia matumizi ya vyandarua vyenye viatilifu ambapo zaidi ya vyandarua milioni 24.2 vimesambazwa, kumechangia wanafunzi kuendelea na masomo yao bila kukatishwa mara kwa mara sababu ya malaria,” alisema.
Mwanzilishi wa Malaria No More, Ray Chamber alimsifu Kikwete kwa kuwa kiongozi aliye mstari wa mbele kuukabili ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment