Tuesday, 12 April 2016

KHANGA: RAFIKI WA MWANAMKE ASIYEPITWA NA WAKATI



Dar es Salaam. Mwanamke wa Kiafrika kama ilivyo ada na mafundisho anayopata tangu akiwa mdogo ni kujisetiri.
Mafundisho hayo hayajabagua dini wala kabila, zote zinahimiza binti kujisetiri, huku kina mama wakifanya kazi ya ziada kuwahimiza mabinti wa kike kujifunga khanga, tena siyo shingoni bali kiunoni.


‘Aso hili ana lile’, ‘Kuvuja kwa pakacha nafuu ya mchukuzi’, ‘Alaa Kumbe’, ‘Raha ya ndoa muwe wanne’ ni baadhi ya maneno maarufu ya khanga zilizowahi kupendwa nchini.
Mwanamke huwa huru anapovaa khanga awapo jikoni, nyumbani akifanya kazi ndogondogo.
Asili ya vazi hili ni pwani ya Afrika Mashariki kama maeneo ya Mombasa nchini Kenya na visiwani Zanzibar ndiyo walikuwa watu wa kwanza kulivaa na kuliheshimu.
Muuza khanga katika soko la Tandika jijini Dar es Salaam, Husna Kitwana anasema miaka mitano au sita nyuma alikuwa anauza khanga kutokana na majina hasa za mipasho, lakini siku za hivi karibuni zenye maneno ya Mungu ndiyo zinanunuliwa zaidi.
Anasema biashara hiyo imepungua kutokana na watu kuvaa vazi hilo wakati maalumu, tofauti na siku za nyuma lilipokuwa vazi rasmi. Anafafanua wasichana na kina mama , wanavaa nguo bila khanga, umaarufu wa madera ambayo yana mitandio pia umechangia kupunguza soko la khanga. Anaitaja sababu nyingine ya biashara hiyo kuzorota kuwa ni kuingia mtindo wa vikoi. “Ni aghalabu kumkuta msichana ananunua khanga badala yake atanunua kikoi kizito kiko kwenye fasheni, ”anasema.
Mwigizaji Riyama Ally anasema kwa kawaida hawezi kuvaa kanga akatoka kwa sababu haimkai vema, lakini hakosi kuwa nayo kwa sababu sifa ya mwanamke, mali ya mwanamke, asili ya mwanamke wa Kiswahili ni khanga. “Navaa kanga nikiwa jikoni. Wazungu, wasomi , vijana wa siku hizi wanavaa aproni, navaa wakati wa kuswali, kulala na kwa kweli nikimuona mwanamke amevaa vazi hilo hufurahi, ” anasema.
Riyama anaeleza hawezi kutembea bila khanga, hata akiwa na kitu kingine kama mtandio, kikoi hujiona amepungukiwa, lakini akiwa na khanga kwenye mkoba safarini hujiamini kwa lolote.
Anasema siku hizi watu hawanunui khanga kwa ajili ya majina, wananunua kwa kuvutiwa na rangi, kama wanahitajika kuvaa kwenye tukio fulani. “Wengi wanakwepa majina ya mipasho, badala yake hupenda yale mazuri kama yenye maneno ya Mungu, ya mapenzi, lakini zamani ilikuwa kanga inatumika katika kupasha huyu akivaa yenye neno hili na mwenzake anamjibu kwa kuvaa yenye neno kali zaidi, ”anasema.
Anasisitiza heshima ya kanga ipo pale pale kwa mwanamke `na ambaye anakaa mbali nayo ipo siku atatamani apate hata kipande ajistiri nacho.
Msanii Lina Sanga anasema anashangaa licha ya kupenda kuvaa nguo za kisasa anaithamini khanga na kuipa nafasi katika nguo kama zilivyo nyingine.
Anasema hana khanga nyingi na huvaa akiwa anafanya shughuli ndogondogo, hupenda kuziangalia hasa zikiwa zimepangwa vema kabatini. “Ukweli sivai sana khanga, lakini mama yangu alikuwa akitutaka kuzivaa tukiwa nyumbani, nimeendelea kuithamini siku zote, ” anasema Lina.
Dondoo za matumizi ya vazi la kanga
Khanga ni kiungo muhimu kwa mwanamke kutokana na kuitumia katika mazingira maalumu ikiwamo katika misiba, kuona wagonjwa, harusini au anapokwenda kujifungua.
Kujifungua
Wazazi wengi hasa wa Kiswahili hata awe na daraja gani la kifedha, anapokwenda kujifungua huwa na khanga na hata mtoto mchanga akivalishwa nguo nadhifu juu kutakuwa na khanga ameviringishwa.
“Night Dress”
Wanawake wengi hutumia vazi hilo wakati wa kulala, hivyo vazi hilo kuchuana vikali na night dress.
“Napenda nikiwa na mpenzi wangu avae khanga wakati anapanda kitandani au ananiandalia chakula cha usiku badala ya kuvaa gauni la kulalia, ”anasema Zarafi Mustapha aliyekutwa na gazeti hili akinunua khanga.
Zawadi kwenye sherehe, misiba
Ni kawaida kukiwa na sherehe yoyote watu kutunzana khanga, lakini hata katika misiba waliofiwa wanapokuja kuogeshwa na marafiki zao kwa watu wa Pwani hutumia khanga kama kifuta jasho kwa wapendwa wao waliofiwa.
Lakini, khanga pia hutumika kama vazi maalumu kwenye misiba, ambako kina mama licha ya kuvaa mavazi yao ya asili huzivaa zikiwa na maneno ya kumtukuza Mungu na zilizofanana. Neno maarufu linalotumika ni sare, kwa maana wote huvaa aina moja ya khanga.
Mitindo
Wabunifu wameiona fursa katika vazi hilo na kuandaa fasheni shoo za khanga kama “Kanga za Kale Fasheni Shoo”.
Fungate
Maharusi wengi wa Kiafrika wanapokuwa katika fungate baada ya kufunga ndoa huvaa khanga kwa siku saba zote ambazo huwa ndani.
Ulinzi njiani
Mwanamke anayethamini ulinzi, hakosi khanga katika mkoba wake na wengi huona hiyo kama ulinzi wao wanapopata dharura kulingana na maumbile yao.
Majina maarufu ya khanga
Khanga za zamani zilikuwa na majina kulingana na maua, kwa sababu hazikuwa na maua mengi ilikuwa rahisi kuzifahamu ikiwamo Karafuu, jicho la ng’ombe, Sutu, Pakacha, Kawa, Boi Manda au Chanuo.
Majina mengine ni Nyumba kunga, Kuti kavu, Kiti cha Bwana, Tai ya Bwana na Sikio la Kufa.
Katika majina ya khanga kulingana na maua, kulikuwa na ambazo zina maana kwa mfano sutu ilikuwa khanga maalumu kwa maharusi yaani ilitumika wakati wa fungate.
Sheria kwa wanawari wa zamani, akimaliza fungate nguo alizokuwa akitumia ndani ikiwamo hiyo khanga aina ya sutu, kilemba huchukuliwa na somo aliyekuwa akikaa nae.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!