Pages

Thursday 7 April 2016

HISTORIA YA MTEMI MIRAMBO WA TABORA




JINA la Milambo ni maarufu sana hapa Tanzania na katika eneo lote la ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini ni watu wachache wanaoweza kueleza Milambo ni nani na alifanya nini hadi kustahili sifa kubwa kiasi hicho.



Kutokana na sifa hizo, hivi leo, kuna mtaa moja katika Jiji la Dar es Salaam uliopewa jina lake. Huko Tabora, Shule ya Sekondari na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vimepewa jina la Milambo. Kumbukumbu kama hizo zinaashiria kwamba Milambo alikuwa ni mtu maarufu.

Mtemi Milambo alizaliwa kwenye miaka ya 1840 katika tawala ndogo ya Ukune katika eneo la Unyamwezi, Mkoa wa Tabora Tanzania. Baba yake alikuwa mtemi Kasanda wa Uyowa katika wilaya ya sasa ya Urambo. Mama yake aliitwa Masele Nyakasi au Nyakashi wa uzawa wa Mtemi Kifumigulu mkimbu kutoka Ikungu aliyefika Usumbwa na kuanzisha tawala ndogo ya Ukune. Kifumigulu alikuwa ni mtoto wa Mapokela Kiumbe I mtemi wa Ikungu.

Kifumigulu na ndugu yake Magokola waliondoka Ikunga kwenda Usumbwa kuwinda tembo na kufanya biashara. Lakini baada ya kugundua kwamba wenyeji waliowakuta hawakuwa na nguvu, waliweza kuanzisha tawala mbili za Ukune na Uyogo.

Milambo mwenyewe alizaliwa Ukune kwani Nyakasi alipokuwa na mimba na kwa sababu alikuwa ni mimba ya kwanza alirudi kwa wazazi wake kwenda kujifungua.

Nyakasi alijifungua mtoto wa kiume aliyepewa jina la Mbula Mtelya.
Milambo alikulia Uyowa na baba yake mtemi Kasanda alipofariki, Milambo alirithi utawala wa Uyowa.

Kasanda alikuwa na Jeshi lake ambalo masimulizi yanaeleza kuwa aliliongoza kwa ushupavu mkubwa lakini kwa sababu Uyowa ilikuwa ni tawala ndogo yenye watu wapatao 4,000 wakati Milambo anatawazwa, hakuweza kuingia kwenye mapambano makubwa kama alivyofanya Milambo baadaye.

Kwa kutambua kikwazo hicho cha udogo wa tawala ya Uyowa aliyoirithi kutoka kwa baba yake, Milambo aliamua kuondokana na kikwazo hicho. Miaka miwili tu baada ya kuwa mtemi wa Uyowa, Milambo alivamia tawala ya jirani ya Ulyankulu na kuiunganisha na Uyowa na kuzitawala zote mbili kwa pamoja. Baadaye tawala hizo mbili zilikujajulikana kama Urambo jina ambalo linatumika hadi leo.

Milambo aliishi na kutawala katikati ya karne 19. Katika kipindi hicho mambo mengi yalikuwa yanatokea ulimwenguni ambayo yalianza kuligusa bara la Afrika ikiwemo Afrika Mashariki.

Unyamwenzi ni eneo kubwa lakini wananchi wake waligawanyika katika tawala nyingi ndogondogo zilizo huru na zisizo na mshikamano. Hali hiyo ilizifanya tawala hizo kuwa dhaifu kijeshi na katika ushindani kibiashara. Biashara kubwa ya wakati huo ilikuwa ni Pembe za tembo, watumwa na shaba.

Watemi wengi wa Kinyamwezi walipeleka misafara pwani kwenda kuuza pembe za tembo na kisha kununua, nguo, majembe, mahitaji ya kijeshi, shanga na vitu vingine vya wakati huo.

Katikati ya karne ya 19 wafanyabiashara wa Kiarabu waliingia Unyamwezi wakiongozwa na Musa Mzuri ambao walifanya makazi yao Unyanyambe, moja ya tawala muhimu ya Unyamwezi.

Baadaye alifika Muhammad bin Juma, baba yake Tippu Tipu. Muhammad Bin Juma alihalalisha ukazi wake Unyanyambe kwa kumuoa Kalunde, binti ya mtemi Fundikira wa Unyanyembe. Hapo ndipo ushindani wa kibiashara kati ya Waarabu na Wanyamwezi ulipojitokeza kwa nguvu zaidi.

Milambo hakupenda biashara yote idhibitiwe na waarabu na maliasili zichukuliwe bila ya wenyeji kufaidika nazo. Milambo ameelezwa na waliomwona kuwa alikuwa na urefu wa wastani, mwenye mwili imara na mwenye akili nyingi na alikuwa tayari kusikiliza ushauri lakini uamuzi alifanya yeye. Mara akisha kuamua, Milambo alitekeleza maamuzi bila kuchelewa.

Milambo alikuwa mkatili na hakuvumilia utovu wa nidhamu miongoni mwa wasaidizi wake na wananchi kwa ujumla wake.

Katika mazingira ya kukabiliana na ushindani, Milambo aligundua kuwa Uyowa na Ulyankulu peke yake zisingempa uwezo wa kupambana na wageni. Na kwa vile isingekuwa rahisi kuwaelimisha na kuwaunganisha Wanyamwezi kwa hiyari, alitumia nguvu za kijeshi.

Katika kipindi kifupi aliweza kuzivamia na kuziingiza chini ya himaya yake karibu tawala zote za Kinyamwezi isipokuwa Unyanyembe.

Wakati wa kilele cha mafanikio yake, Milambo alidhibiti eneo lote kuanzia Ziwa Victoria hadi bonde la Ziwa Rukwa.

Katika eneo lote hilo hakuna msafara uliopita bila kibali cha mtemi Milambo.

Katika mwaka 1871 Milambo alijitokeza kama mtawala asiye na mpinzani katika ukanda wote wa Afrika Mashariki kufuatia mapambano kati yake na Waarabu walioweka ngome yao Unyanyambe.

Jamii ya Waarabu na Unyanyembe wakisaidiwa na Mtemi Mkasiwa waliandaa jeshi kubwa kupambana na Milambo na kumaliza nguvu zake kabisa.

Lakini Kabla hatujaangalia kisa hiki ni vizuri kusimulia yaliyokuwa yanatokea Unyanyembe hadi kusababisha Mkasiwa (Mnyamwezi) kushirikiana na Waarabu kumwangamiza Milambo.

Tumeona hapo awali kwamba Waarabu wa kwanza wakiongozwa na Mussa Mzuri walifika Unyanyembe wakati mtemi Fundikira I akitawala.

Baadaye jamii ya kiarabu na wa fanyabiashara wa Kiswahili ilipanuka hadi kumfanya Sultan wa Zanzibar kumteua Said bin Salim kuwa liwali wa Unyanyembe.

Katika kipindi hicho waarabu waliweka fungamano na mtawala wa Unyanyembe kwa Muhammad bin Juma (Baba wa Tippu Tip) kumuoa binti wa Mtemi Fundikira I Kalunde.

Bila ya watawala wa Unyanyembe kujijua, kuteuliwa kwa liwali kumwakilisha Sultan wa Zanzibar na mwarabu kumuoa mtoto wa mtemi, kulianza kupunguza nguvu za watawala* wa Unyanyembe na hili lilijidhihirisha waziwazi baada ya kufa Mtemi Fundikira I mwaka 1858.

Baada ya Mtemi Fundikira I kufariki 1858 kulitokea msuguano nani arithi utemi wa Unyanyembe. Katika msuguano huo mshindani aliyeungwa mkono na jamii ya Waarabu alifanikiwa. Tayari Waarabu walisha anza kuwa na nguvu dhidi ya watawala wa Unyanyembe. Mtemi Msabila au Mnywa Sele kama alivyopenda kujiita yeye mwenyewe,* alimrithi Fundikira 1 kwa msaada wa Waarabu.

Mtemi Mnywa Sele alikuwa mkakamavu, mpenda biashara na mzalendo kweli kweli wa Unyanyembe. Haukupita muda Mnywa Sele akagombana na washirika wake Waarabu baada ya kuanza kuwatoza kodi, kudhibiti biashara ya kwenda pwani na baadae kuzuia wasiuziwe nafaka. Mnywa Sele alisahau kuwa alifika hapo kwa nguvu ya Waarabu hao hao. Waarabu walipoona biashara na ustawi wao unatishiwa, mwaka 1860 walimpindua Mnywa Sele na badala yake wakamweka Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.

Mnywa Sele, kwanza alikimbilia Rubunga tawala ndogo kusini mwa Unyanyembe. Lakini Waarabu waliandaa jeshi na kwenda kumfukuza hapo nae akakimbilia Ukimbu ambako aliendesha vita vya msituni kwa miaka mitano akijaribu kurudi Unyanyembe bila mafanikio.

Katika jitihada za kujipatia mahitaji ya jeshi lake la ruga ruga, Mnywasele alianza kuvamia misafara ya kutoka pwani kwenda Unyanyembe.

Mwaka 1861 Speke alikutana na Mnywa Sele porini na la jeshi lake la ruga ruga. Speke alijaribu kutafuta suluhu kati ya Mnywa Sele na Waaraabu wa Unyanyembe bila mafanikio. Mnywa Sele aliuawa baada ya kushindwa na kukamatwa na msafara uliongozwa na Mwarabu Khamisi Bin Abdulla katika eneo kati ya Ugogo na Unyanyembe mwaka 1865.

Tukirudi Unyanyembe kwenyewe, watawala wa Unyanyembe hawakuridhishwa na kitendo cha Waarabu kumsaidia Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.

Wengi walimuona Mkasiwa kama pandikizi la Waarabu.

Mtemi Milambo ambaye alivutiwa na sera za Mnywa Sele za kuwatoza kodi Waarabu na kudhibiti biashara katika Unyamwezi, alimuona Mkasiwa kama kibaraka wa Waarabu.

Katika kipindi chote ambacho Mnywa Sele alipigana msituni, Milambo alimuunga mkono. Kwa hiyo uhasama kati ya Milambo na Waarabu na Unyanyembe ulichukua sura mpya.

Baada ya kumpindua Mnywa Sele na baadae kuuawa, Waarabu waliona kikwazo pekee katika kudhibiti biashara na siasa za Unyamwezi ni Milambo tu.

Milambo aliendelea kuwatoza kadi Waarabu na misafara yote iliyokuwa ikipitia Urambo kwenda Ujiji. Wagogo nao walikuwa na bugudha kubwa kwa misafara ya kutoka pwani kwenda Ujiji kupitia Unyanyembe kwa kudai hongo.

Kwa hiyo Waarabu walijikuta katika mazingira magumu kibiashara na kiusalama.

Mwaka 1871 Waarabu waliandaa jeshi kumkabili Milambo ili kufungua njia ya kwenda Ujiji.

Katika Kampeni hiyo Waarabu walisaidiwa na Mtemi Mkasiwa na mvumbuzi Henry M. Stanley ambaye msafara wake ulikuwa umezuiwa na Milambo kwenda Ujiji kupitia Urambo.

Jeshi la wapiganaji 2255 kati yao1500 wakiwa na bunduki na waliobaki wakiwa na silaha za asili.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za Stanley, Milambo aliandaa rugaruga 1,000 akaunganisha na washirika wake Wangoni 1,500 kuwakabili Waarabu na washirika wao.

Baada ya kuombewa dua za kiislamu na tambiko za Kinyamwezi, Waarabu walianza mashambulizi kwa nyimbo za vita na tumbuizo za ngoma.

Milambo kwa ushujaa wake na utaalamu wa mbinu za kivita aliamuru majeshi yake yasipigane kwa nguvu badala yake wawe wanarudi nyuma kama vile wamezidiwa.

Kwa mbinu hiyo aliweza kuwavuta wavamizi hadi wakafika karibu na Ulyankulu kwa upande wa kaskazini.


Rugaruga mnamo mwaka 1914 /15 wakiwa askari upande wa Wajerumani katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; jina la picha katika kumbukumbu ni "Deutsch-Ostafrika, Hilfstruppen" (yaani "Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, askari wasaidizi")

Baada ya kuona majeshi yote ya wavamizi yameingia katika himaya yake, Milambo aliamuru majeshi yake yaanze kuishambulia.

Baada ya mapambano makali ya ana kwa ana jeshi la uvamizi lilivunjika na kusambaratika na kuanza kukimbia ovyo kurudi Unyanyembe bila ya mpangilio. Milambo aliwafuata na askari wengi wa wavamizi waliuawa. Alipofika Unyanyembe, Milambo aliharibu sehemu kubwa ya boma la Itetemia lakini hakuzingira sehemu alikojichimbia Mkasiwa wala sehemu alikokuweko Stanley.

Aidha Milambo hakuharibu ngome za Waarabu. Lakini ghafla Milambo aliisitisha mashambulizi ya Itetemia na kuamuru wanajeshi wake kurudi nyuma ingawa hakukuwa na upinzani mkali.

Hakuna maelezo yoyote kutoka kwa Milambo kwa nini alisitisha mashambulizi ya Itetemia.

Kuna mawazo kwamba huenda Milambo hakutaka kusababisha madhara yoyote kwa Stanley aliyekuwepo kwenye boma hilo na pia hakutaka kuingia kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Sultani wa Unguja Zanzibar kwa kuwaangamiza Waarabu wa Unyanyembe.

Hata hivyo, wakati majeshi ya Milambo yanarudi nyuma mwarabu moja, Khamisi bin Abdulla aliamurisha wafuasi wake kushambulia kwa kudhani majeshi ya Milambo yalikuwa yameshindwa.

Alijidanganya. Mara moja majeshi ya Milambo ya yalizingira ngome ya Mwarabu huyo na kuuwa wafuasi wake wote pamoja na yeye mwenyewe na kuharibu kabisa ngome yake.

Kitendo cha kutomgusa Stanley ambaye alikuwa amekimbiwa na watu wake na kuwaacha Waarabu salama kinaonyesha jinsi Milambo alivyokuwa mwerevu. Hakutaka kuharibu uhusiano wake na jamii ya kimataifa.

Stanley alichukizwa sana na udhaifu walioonyesha Waarabu katika kampeni dhidi ya Milambo ambaye alimwita ‘’ Jambazi” na pia ‘’Bonaparte wa Afrika,” akimlinganisha na mfalme Napoleon Bonaparte wa Ufaransa.

Stanley alichukizwa na kitendo cha Waarabu kumwingiza kwenye mapambano na Milambo wakati wanajua hawana uwezo.

Stanley aliondoka Unyanyembe kwenda kusini ili kumkwepa Milambo. Alipita Ukonongo kisha akaelekea magharibi na baadaye kaskazini hadi Ujiji alikomkuta Dk. David Livingstone mwaka 1871.

Ushindi wa Milambo dhidi ya Waarabu wa Unyanyembe na washirika wao ulimfanya aonekane kama kiongozi asiye na mpinzani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Yeye mwenyewe alijiita ‘Sultan Mkuu wa Afrika’. Uhasama kati ya Milambo na Waarabu wa Unyanyembe uliendelea kwa kipindi chote cha uhai wa Milambo.

Jaribio jingine la Milambo la kuangamiza Unyanyembe na kuvunja kabisa nguvu za Waarabu lilishindwa. Septemba 1871 Milambo alishambulia Unyanyembe kwa lengo la kuwasambaratisha Waarabu.

Katika mapigano yaliyofanyika katika kijiji cha Mfuto karibu kabisa na Unyanyembe, Milambo alishindwa vibaya. Baadaye iligundulika kuwa, siku ile Milambo aliongoza mapigano akiwa amelewa.

Inawezekana tukio hili ndilo lililomfanya Milambo kuacha pombe kwani alimweleza mmisionari mmoja kuwa asingeweza kuendesha shughuli zote na kutawala watu wake vizuri kama angekuwa anakunywa pombe.

Kutokana na ushindi huo, Waarabu wa Unyanyembe waliamua sasa kumwangamiza Milambo. Waliandaa jeshi kubwa lililojumuisha Waarabu wa Unyanyembe, kikosi kilicholetwa na Waarabu wa Usangu, Mtemi Mulimanombe wa Ugunda, Mtemi Simba Kaung’ando wa Usawila na askari 300 walioletwa na Mwarabu wa Ujiji, Said Bin Majid.

Said bin Majid alitaka kutumia mwanya huo kulipiza kisasi kutokana na Milambo kumuua mtoto wake, Soud bin Majid na Mwarabu mashuhuri wa Unyanyembe Khamis bin Abdulla.

Khamis bid Abdulla ndiye aliyemuua Mnywa Sele (Msabila) ambaye Milambo alimuona ndiye mtemi halali wa Unyanyembe na siyo Mkasiwa.

Kuongozea nguvu mtemi Mkasiwa alipeleka wa rugaruga kwenye jeshi la Waarabu na yeye mwenyewe alikuwepo kwenye mapambano yaliyoongozwa na Said bin Salim, liwali wa Unyanyembe kama mwakilishi wa Sultan wa Zanzabir.

Dk. David Livingstone akiwa Ujiji alipata habari kuwa jeshi la Waarabu lilikuwa na watu 2,000. Katikati ya Mwaka 1872 Waarabu walishambulia Urambo.

Milambo alijua ukubwa wa jeshi la maadui lakini hakutishika sana.

Walipokuwa wanasogelea Urambo, Milambo alifanya shambulio kubwa na kuwashinda Waarabu na mara kikosi chote cha wavamizi kilisambaratika na kiongozi wao, Said bin Salim akakimbia kurudi Unyanyembe.

Wapiganaji baada ya kuachwa na kiongozi wao, kila mmoja alirudi kwao kwa njia aliyojua mwenyewe.

Kushindwa kwa Waarabu katika kampeni hii ambayo ilionekana kuandaliwa vizuri, Milambo alibaki bila tishio lolote katika udhibiti wake wa sehemu kubwa ya Unyamwezi.

Baadaye Milambo alipata washirika wakusaidiana naye. Wa kwanza ni Nyungu ya Mawe ambaye awali alikuwa anazunguka na jeshi lake katika misitu ya Ukimbu bila ya kuwa na makao maalumu.

Kisha alishambulia tawala ya Ukimbu ya Kiwele na kuishinda na kujifanya mtemi wa Kiwele na kuburi lake liko huko hadi leo.

Mwingine ni mtemi Mtinginya wa Usongo. Mtinginya na Nyungu ya Mawe waliwahi kupigana lakini baadaye walipatana na kwa pamoja wakawa washirika wa Milambo bila ya kuwa chini ya uongozi wa Milambo dhidi ya Unyanyembe na Waarabu wake.

Mshirika wa tatu ni Simba Kaung’ando wa Usawila. Huyu pamoja na Mtemi wa Ugunda walimsaidia Mkasiwa na Waarabu wake kumshambulia Milambo, lakini alibadilika na kufanya urafiki na Milambo.

Kwa kushirikiana na Watemi, Mtinginya, Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando, Milambo alidhibiti njia zote za kwenda ziwa Tanganyika na Kongo na njia ya kaskazini kwenda Uganda.

Misafara yote iliyopita katika kipindi cha 1871 na 1879 ilifanywa hivyo kwa idhini yake na aliwatoza kodi. Kulikuwa na njia tatu, moja ilitoka pwani kupitia Ugogo na Unyamwezi* kaskazini kwenda Uganda.

Njia ya pili na maarufu ilipita Ugogo na Unyanyembe kwenda Ujiji na Kongo, na njia ya tatu ilipita Usagara, Usangu, Ukimbu hadi Karema katika Ziwa Tanganyika.

Milambo na washirika wake, Mtinginya na Nyungu ya Mawe walidhibiti njia ya kati ya Ugogo na Unyanyembe na kaskazini kwenda Uganda.

Kwa upande wa Kusini kwa kushirikiana na Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando walidhibiti njia ya kupitia Ukimbu kwenda ziwa Tanganyika.

Wamisionari wawili, Tom Cadenhead na Frederick Carter walipojaribu kumkwepa Milambo kwa kupita njia ya kusini alipeleka jeshi lake kusini.

Kwanza alishambulia Ugunda iliyokuwa imesaidia Waarabu wa Unyanyembe na kisha akaingia Usawila bila ya mapigano kwa kuwa Simba Kaung’ando alifanya mapatano na Milambo.

Baadaye majeshi ya Milambo yakisaidiwa na majeshi ya Simba Kaung’ando yalimshambulia Mtemi Kasogela wa Upimbwe aliyekuwa amewapokea wamisionari hao wawili, Cadenhead na Carter.

Upimbwe iliangamizwa na wamisionari hao wawili wakauawa. Katika kampeni hiyo, Milambo alikuwa pamoja na majeshi yake. Kwa tukio hilo njia ya kupitia Usangu na Ukimbu ikafungwa.

Kwa udhibiti huo, Waarabu wa Unyanyembe hawakuwa na hiyari isipokuwa kupata kibali cha Milambo na kulipa kodi au ushuru wapate kufanya biashara katika eneo la Unyamwezi na hata kupitisha misafara kwenda Kongo.

Waarabu wa Unyanyembe hawakutaka tamaa katika harakati zao za kumwondoa Milambo wapate uhuru wa kufanya biashara ya watumwa na pembe za tembo.

Walimgeukia Sultan Barghash bin Said wa Zanzibar kumtaka apeleke jeshi kummaliza Milambo. Barghash alikubali kujiingiza kwenye mgogoro wa Waarabu wa Unyanyembe na Milambo siyo tu kwa sababu ya kuwasaidia lakini kwa sababu biashara ya pembe za tembo, ilianza kuyumba.

Soko la Zanzibar lilikuwa halipati pembe nyingi kama siku za nyuma.

Agosti 1873, jeshi la Bargash likiongozwa na Amir bin Sultan liliwasili Unyanyembe tayari kuungana na wenyeji wao kumkabili Milambo.

Kwa mshangao Waarabu wa Unyanyembe hawakupenda uteuzi wa Amir bin Sultan ambaye alishawahi kukaa Unyanyembe kabla ya kurejea Zanzibar na kusita kushirikiana naye.

Jeshi hilo ambalo liliundwa na Mabulushi kutoka Zanzibar na Waswahili kutoka Pwani baadaye liligawanyika.

Waswahili kutoka Pwani wakaendelea kumtii Amir bin Sultan na Mabulushi wakahamishia utii wao kwa Waarabu wawili wa Unyanyembe wenye ushawishi mkubwa Shaykh bin Nasibu na Abdulla bin Nasibu.

Ndugu hao wawili walihofu kunyang’anywa madaraka na ushawishi waliokuwa nao katika Unyanyembe na Amir bin Sultan.

Katika Mazingira ya mgawanyiko huo miongoni mwa Waarabu, uwezekano wa kumshambulia Milambo ukawa haupo.

Milambo alijua uwepo wa jeshi la Sultan Barghash hapo Unyanyembe lakini hakushambulia aliwasubiri wathubutu.

Sultan Barghash alimtuma Abdulla Mohammed kwenda Unyanyembe kuchunguza kwa nini Milambo hajashambuliwa. Mjumbe alitoa taarifa kwa Barghash kwamba hakukuwa na umoja miongoni mwa Waarabu kiasi kwamba kumshambulia Milambo isingewezekana.

Barghash kwa hasira akayaondoa majeshi yake kuyarudisha Zanzibar. Waarabu wa Unyanyembe walilalamika lakini Barghash akawajibu kuwa kama wanataka kuendeleza mgogoro na Milambo wanaweza kufanya hivyo kwa wakati wao.

Baadaye Barghasha alimwambia James Elton, mwakilishi wa Uingereza Zanzibar kuwa hana uwezo wa kufanya zaidi ya alivyofanya na mtazamo wake ni kuwaacha wakoloni wa Kiarabu waendeshe mapigano wao wenyewe.

Kisha akaongeza kuwa “hana mamlaka katika nchi hiyo (Unyamwezi)". Said bin Salim ambaye Wanyamwezi walimpa jina la Kissesa na ambaye Milambo alikuwa hampendi kabisa alipeleka ombi kwa Kabaka Mutesa I wa Buganda kumtaka alete jeshi kumwondoa Milambo.

Mutesa I alikubali na kuandaa jeshi la watu 9,000 kwenda Urambo.

Milambo mwenyewe alimueleza mmisionari, Dk. Ebenezar Southon aliyekuwa Urambo kuwa jeshi la Kabaka Mutesa I lilisitisha msafara na Kurudi Buganda baada ya kukosa maji ya kunywa kwa watu 9,000.

Kushidwa kwa kampeni ya Mutesa I dhidi ya Milambo kuliwaacha Waarabu wa Unyanyembe na njia moja tu ya kutafuta suluhu na Milambo.

Mwaka 1875 Said bin Salim alipeleka ujumbe kwa Milambo akitaka suluhu. Kilichozungumzwa na kukubalika hakikujulikana lakini matokeo yake ni kwa Milambo kuruhusu misafara ya Waarabu kupita katika himaya yake kwa kulipa ushuru.

Kampeni za kivita za Milambo katika sehemu kubwa ya Unyamwezi na kampeni za Nyungu ya Mawe katika eneo la Kusini na Kusini Mashariki ya Unyanyembe na harakati za Mtinginya Kasikazini Mashariki ya Unyanyembe zilifanya biashara ya pembe za ndovu katika soko la Zanzibar kudorora na Mkasiwa wa Waarabu wake hapo Unyanyembe kubaki kama wafungwa.

Mkasiwa hukuweza kutoka Unyanyembe kwa hofu ya wababe hao watatu. Kwa kulinda soko la Zanzibar na kwa kutotaka mapambano ya kijeshi, Sultan Barghash aliamua kumwekea vikwazo vya biashara Milambo hasa vifaa vya kijeshi kama bunduki, baruti, risasi na fataki.

Vikwazo hivyo vilimwathiri sana Milambo ingawa alivipata kwa njia ya uvamizi na kwa kununua kupitia watu wengine.

Milambo alianza kushindwa katika baadhi ya mapambano aliyoyafanya mwishoni mwa miaka ya 1870 na mwanzoni mwa miaka ya 1880.

Kwa mfano uvamizi aliofanya Milambo katika utawala wa Turu na Iramba ulishindwa na akalazimika kurudi nyuma.

Mwaka 1877 Barghash alieneza vikwazo vya silaha kwa machifu wengine zaidi ya Milambo katika eneo hili la Afrika Mashariki.

Milambo ameelezwa kuwa alikuwa mjanja, mwerevu na mwepesi wa kuchukua hatua wakati mwingine alikuwa mgumu kumuelewa.

Wangoni walipofika katika nchi ya Unyamwezi kuna wakati aliwatumia katika nchi ya rugaruga na wakati mwingine alitofautiana nao na kupigana.

Inasemekana kuwepo kwao katika jeshi lake kulimsaidia sana Milambo. Nyungu ya Mawe ambaye alikuwa mtawala aliyemtegemea kwanza Milambo, aliafiki harakati zake lakini baadaye alitamani Nyungu ya Mawe apunguzwe nguvu zake.

Ingawa baada ya mapatano na Waarabu mwaka 1875 Milambo alianza kuzungumza amani na kwamba vita sasa basi, lakini aliendelea kushambulia maeneo ya Ukongo hadi Ubende.

Milambo hakuvumilia uasi na utovu wa nidhamu. Hali hiyo ilipojitokeza ilizimwa kwa ukatili mkubwa. Viongozi wa tawala moja walipokataa kutii amri ya kuwataka wachangie gharama za jeshi yake, aliamuru wakamatwe na kuuawa.

Kijana mmoja aliyeibia msafara ambao Milambo alikuwa ametoa kibali, alikamatwa na alipofikishwa kwa Milambo, Milambo mwenyewe alimuua kijana huyo.

Milambo alikufa mwaka 1884 akiwa na umri unakadiriwa kuwa miaka 44. Mwaka huo huo alikufa Nyungu ya Mawe na Kabaka Mutesa I.

Maelezo ya kifo cha Milambo yana utata. Wazungu waliokuwepo katika eneo la Unyamwezi wakati wa kifo chake walisema alikufa kwa ugonjwa wa koo. Waliamini huenda ilikuwa ni saratani ya koo.

TAARIFA HII KWA MSAADA WA NASSORO WAZAMBI

No comments:

Post a Comment