Friday 22 April 2016

Dk. Mengi amwagia sifa Rais Magufuli kupambana na rushwa



MWENYEKITI Mtendaji wa IPP Limited, Dk. Regnald Mengi, amemwagia sifa Rais John Magufuli, kwa ujasiri wa kujitoa kwa moyo wake wa dhati wa kushughulikia changamoto za kitaifa, zikiwamo wizi wa mali ya umma, rushwa na ufisadi.



Dk. Mengi alisema Watanzania, wanapaswa kujiuliza swali moja, na la muhimu kwamba “tulifika, fikaje hapo”.
Alikuwa akizungumza jana katika mahafali ya 24 ya kidato cha sita ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ashira, Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi.
“Kwa bahati mbaya sana, nchi yetu kwa sababu ambazo wote tunafahamu, imegeuzwa kuwa shamba la bibi, na vile vile imekuwa tambara bovu, na kila mahala unapogusa inatoboka kwa sababu ya rushwa,
kwa mapenzi ya Mwenyenzi Mungu tumempata Rais, ambaye amekubali kushughulikia tatizo hili kwa ujumla wake…Mungu amsaidie aweze kutumikia Watanzania katika changamoto hii kubwa ya rushwa na wizi wa mali ya umma,” alisema.


Katika mahafali hayo, ambayo Dk. Mengi alichangisha Sh. milioni 151, kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa uzio wa shule hiyo, alimshukuru Rais Magufuli kwa kuanzisha mpango wa elimu bure, kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
“Chini ya mpango huu wa elimu bure, tunafahamu wazazi na walezi wanatambua pia mchango wao, lakini kitu ambacho ningependa kuwakumbusha ni kuwa, wanao wajibu wa kuangalia maslahi ya maisha ya wanafunzi wetu.”
Aidha, katika kuwatia moyo wahitimu hao, Dk. Mengi ametoa ahadi ya shilingi milioni moja, kwa kila mwanafunzi atakayefaulu mitihani yake ya kitaifa kwa kupata daraja A.
Awali, Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Martin Shao, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, alisema uongozi uliamua kujenga uzio huo ili kuwapa fursa wanafunzi kuishi na kusoma kwenye mazingira tulivu na yasiyo na vishawishi.
“Mheshimiwa Dk. Mengi, tumefanya ujenzi huu kwa awamu, lakini bado hatujamaliza, na katika awamu hii tunahitaji Sh. milioni 150 angalau itusogeze, na awamu ya mwisho itahitajika Sh. milioni 250,”alisema Askofu Shao.
Kabla ya kuanza kwa harambee hiyo pamoja na kuwatunuku vyeti wahitimu 390, Mkuu wa shule hiyo, Elizabeth Abdallah, alimweleza Dk. Mengi kwamba jumla ya wanafunzi 173 waliomaliza kidato cha sita mwaka 2015, walipata nafasi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.
Shule hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo upungufu wa vifaa vya maabara, bwalo la chakula na semina, gari la wanafunzi kwa ajili ya kutoa huduma na uchakavu wa madarasa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!