Wednesday, 27 April 2016

BARUA YA WAZI KWA LULU


KWAKO muigizaji wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, hujambo? Unaendeleaje na shughuli zako za kila siku? Nisalimie mama yako maana naye kitambo kidogo hatujaonana. Ubize huu, we acha tu!
Ukitaka kujua afya ya mimi kaka’ko sijambo, 




namshukuru Mungu. Naendelea kupambana katika eneo langu. Naelimisha, napongeza na hata kukosoa pale ninapoona inafaa.
Madhumuni ya barua hii ni kutaka kukuambia ushike adabu kwa watu waliokuzidi umri. Kuna tatizo katika mapitio yako. Kwa umri wako unapaswa kujifunza vitu vingi kutoka kwa wakubwa, hupaswi kupotoka wakati kwanza wewe ni kioo cha jamii.

Nilishtushwa sana kusikia umenyanyua kinywa chako na kumjibu vibaya mtu aliyekuzidi umri. Nilijisikia vibaya sana pale mama wa aliyekuwa muigizaji nguli Bongo, Steven Kanumba, Flora Mtegoa alivyokulalamikia kuwa katika majibizano yako na yeye ulikosa staha, ukaweka pembeni aibu, ukafikia hatua ya kumuita kubwa jinga mama huyo.

Mama Kanumba yule si kama mama yako mzazi? Unaanzaje kumuita kubwa jinga? Ujasiri huo unautoa wapi. Nini kimekulevya? Umaarufu au ni kiburi cha uzima? Au unajiona umeshayapatia maisha? Mbona una safari ndefu sana, kwa nini usiishi na watu vizuri?

Najaribu kuvuta picha, mama wa watu yule alikukosea nini? Hata kama alikukosea kitu gani bado hukuwa na sababu ya kumtusi kiasi hicho. Waswahili wana msemo usemao mkubwa hakosei, maana yao si kwamba hawakosei, bali hata wakikosea, inatakiwa staha katika kuwakosoa!

Kwa mtoto aliye na maadili, hathubutu kunyanyua kinywa chake na kutamka neno zito kama lile kwa mtu ambaye ni mkubwa kwake. Mtu ambaye ana watoto wakubwa kuliko wewe unaanzaje kumuita kubwa jinga? Hukupewa mafunzo na wazazi?

Bahati mbaya sana, kama Mungu asingemuita mapema Kanumba, mama Kanumba pengine angekuja kuwa mkwe wako. Sasa mtu ambaye angekuwa mkwe wako unapataje ujasiri wa kumsema vibaya hata kama mwanaye ameshatangulia mbele ya haki?

Mama Kanumba mwenyewe ameshanukuliwa mara nyingi katika vyombo vya habari, kwamba hahitaji msaada wowote kutoka kwako zaidi ya faraja. Kwani ukimfariji unapungukiwa na nini? Ukimheshimu kama unavyoheshimu wakubwa wengine kuna tatizo gani?

Nikushauri tu kama kaka yako, katika maisha haya huna sababu ya kuishi kama hutakufa. Kila mmoja wetu hapa duniani hajui siku wala saa. Tunapaswa kuishi vizuri na watu, hakuna sababu ya kuishi na visasi.

Hakuna sababu ya kuishi na vinyongo. Chunga sana mtu asikuwekee kinyongo, asisikitike juu yako. Mama Kanumba akisononeka juu yako, yawezekana ikawa laana kwako. Kwa nini ujitafutie laana.

Umri wa mama Kanumba unatosha kabisa kukwambia ushike adabu yako na wewe ukamuomba radhi. Muda bado unao, nakusihi muombe radhi kwa dhati kutoka moyoni yule mama na nina hakika atakusamehe na mtafungua ukurasa mpya!
Nakutakia mafanikio mema na Mungu akubariki.

Mimi ni kaka yako;
Erick Evarist

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!