Sunday, 13 March 2016

WAFANYAKAZI NIDA WAGOMEA BARUA ZA "KWAHERI"

 

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambao wamisitishiwa mkataba wa kufanya kazi kutokana na ukata ulioikumba mamlaka hiyo, wamegoma kupokea barua rasmi zinazoonyesha kusitishwa kwa mikataba yao.
 
Mmoja wa wafanyakazi hao, Mpaji Isaya aliiambia Nipashe jana kuwa, waliambiwa wafike kuchukua barua hizo jana, ili kuthibitisha rasmi kufutwa kwa mikataba yao.
 
“Baada ya kutangaziwa na Kaimu Mkurugenzi kuwa mikataba imefutwa, walisema tufike leo NIDA kuchukua barua za uthibitisho," alisema Isaya.
 
"Lakini cha ajabu wanataka tusaini fomu kuthibitisha tumepokea barua na tuondoke, wakati kilichoandikwa ndani ya barua hatukijui.
"Sasa kama stahiki zetu tumepunjwa tutajuaje?” 
 
Isaya alisema NIDA ilitakiwa iwape muda wa kuzisoma barua hizo kama ilivyokuwa awali wakati wa kuajiriwa ambapo walipewa muda wa siku tatu kuusoma na kuuelewa mkataba ndipo wakasaini.
 
Kaimu Mkurugenzi wa NIDA Modestus Kipilimba, alisitisha mikataba ya wafanyakazi 597 wiki iliyopita kwa maelezo ya ukosefu wa fedha za kuwalipa wafanyakazi hao kwa sasa.
 
Kaimu Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa NIDA, Rose Mdami, alipotafutwa na Nipashe ili kutolea ufafanuzi suala hilo, alisema waliwapa taarifa wafanyakazi hao kufika jana kwa ajili ya kuchukua baraua zao.
“Taarifa za kuja leo (jana) ofisini NIDA wafanyakazi ni za kweli, walikuja kufuata barua zao lakini kwa maelezo mengine ufike ofisini kwetu,” alisema Mdami.
 
NIDA ilisema haina fedha za kuwalipa malimbikizo ya mishahara ya miezi miwili wafanyakazi wa 597 waliositishiwa mikataba yao ya muda huku menejimenti ikisema inaendelea kujipanga ili kuhakikisha  inawalipa kwa wakati bila usumbufu wowote ijapokuwa ofisi hiyo haina fedha kwa sasa.
 
NIDA ilisema inaendelea kufanya uhakiki wa mikataba ya wafanyakazi wote 597 na kusubiri pesa kutoka hazina kwa ajili ya kuwalipa kwa mujibu wa sheria.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!