Wabunge 12 wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, wameonyesha nia ya kujiuzulu baada ya kusaini waraka maalum wa kupelekwa kwa Spika.
Aidha, wabunge wawili nao wameandika barua kwenda kwa Spika wakitaka uchunguzi wa rushwa dhidi ya kamati yao ufanyike.
Wakati wabunge hao wakichukua uamuzi huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amepangua wajumbe wa Kamati tano za Bunge kutokana na kashfa za rushwa.
Spika Ndugai amesema hatua yake hiyo imetokana na changamoto zilizozikumba kamati hizo.
Hatua hiyo imetokana na vyombo vya habari kuripoti kuwapo na viashiria vya rushwa katika baadhi ya Kamati za Bunge ikiwamo ya Maendeleo na Huduma za Jamii.
WABUNGE WAJITUMBUA
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wabunge hao walieleza kuwa wameamua kujiuzulu ili kupisha uchunguzi wa Bunge ufanyike dhidi ya kamati yao.
Wabunge hao ambao wameshaandika barua ya kujiuzulu na ni miongoni mwa wabunge 12 walioweka saini ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe.
Bashe na Kabwe walithibitisha kuandika barua ya kujiuzulu katika kamati hiyo kwa kile walichokieleza hawawezi kuendelea kuwamo katika kamati inayotuhumiwa.
“Ni kweli nimemwandikia barua Spika, Kamati yetu ina tuhuma za kifisadi, hivyo sijaona sababu ya kuendelea kuwapo katika Kamati inayotuhumiwa kupokea rushwa,” alisema Zitto.
Alisema tuhuma dhidi ya wabunge siyo jambo jipya, hutokea mara kwa mara, alisema suluhisho pekee ni uchunguzi wa kina ili hatua zichukuliwe.
Alisema siku zote hakuna hatua zinazochukuliwa na matokeo yake mambo hayo hujirudia.
Naye Bashe alisema tuhuma za kamati ya huduma za jamii zimeipaka matope kamati hiyo, hivyo hakuona haja ya kuendelea kuwamo ndani yake.
“Nimeandika barua, hata wabunge wenzangu baadhi wametuunga mkono kwa kusaini barua ya kujiondoa katika Kamati hii. Kimsingi sioni haja ya kuendelea kuwapo katika Kamati inayotuhumiwa,” alisema Bashe.
Wabunge walioweka saini ni pamoja na Dk. Raphael Chegeni, Bashe, Dk. Charles Tizeba, Joseph Mbilinyi, Kasuku Bilago, Lucia Mlowe, Jesmine Tisekwa, Jacqueline Msongozi, Mussa Zungu, Juma Nkamia, Zitto Kabwe na Josephine Genzabuke.
KAULI YA MWENYEKITI WA KAMATI
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Chegeni alisema tuhuma zinazoelekezwa katika Kamati yake, siyo za kweli.
lisema Katibu anayetuhumiwa kupokea rushwa, aliondoka katika kikao hicho kabla hakijaisha kutokana na udhuru.
“Wajumbe 12 tumekubaliana na kumwandikia barua Spika tunajiuzulu, pia tunamtaka achukue hatua dhidi ya chombo cha habari kilichoripoti,” alisema Chegeni.
Chegeni ambaye ni Mbunge wa Busega, alisema walikutana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Alhamisi na Ijumaa walikutana na Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Alisema kamati hiyo tangu kuundwa kwake, imekuwa ikiitwa majina ya ajabu ajabu ikiwamo Guatanamo, huku ikienda kwa spidi kubwa.
Dk. Chegeni alisema labda hiyo ndiyo sababu inayosababishwa kuzushiwa maneno.
“Hiyo rushwa ilichukuliwa saa ngapi? Ilitolewa saa ngapi? Kwanza mwandishi hakuja kwetu kutuhoji, wala mimi sikuhojiwa, bali nimelishwa maneno. Mbona CWT wakati tunawahoji walitaka kutulipia semina, lakini tukakataa,” alisema Dk. Chegeni.
Alisema wamemwandikia barua Spika kumtaka mambo matatu ikiwamo kufanya uchunguzi, kumchukulia hatua kali kwa mjumbe atakayebainika alichukua rushwa, Bunge kukitaka chombo cha habari kilichoandika habari hiyo kithibitishe ukweli vinginevyo watakwenda mahakamani.
MABADILIKO YALIYOFANYWA NA BUNGE
Spika wa Bunge, Ndugai alifanya mabadiliko ya Kamati za Bunge na kusema kuwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii inahitaji kupata Mwenyekiti na Makamu wake, Kamati ya Nishati na Madini na Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma zitawekwa Wenyeviti wapya.
Alisema Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, itabadilishwa Mwenyekiti wake na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, itabadilishwa Makamu Mwenyekiti wake.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment