Saturday 26 March 2016

VIGOGO" 150 WAJITOKEZA KUHAKIKI SILAHA ZAO

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani
WAKATI zaidi ya watu 150 wakijitokeza kuhakiki silaha zao, kutii agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani amesema uhakiki huo sasa unafanyika nchi nzima.


Kamishna Athumani amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, huku akikataa kutaja majina ya vigogo waliojitokeza kuhakiki silaha zao kwa sababu za kiusalama.
“Baada ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kufanya uhakiki wa silaha zake hivi karibuni, watu zaidi ya 150 wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wastaafu, mabalozi na wabunge wa nchi mbalimbali wamejitokeza,” alisema.
Mbali na vigogo hao, Kamishna Athumani amesema wananchi wengine wameonesha nia ya kufanya hivyo na kusisitiza kuwa, lengo la uhakiki wa silaha hizo ni kuboresha hali ya usalama kwa kuwajua watumiaji .
Alifafanua kuwa utambuzi huo unafanyika kwa kuwa kunaweza kutokea sababu mbalimbali zitakazofanya wamiliki wa awali wasiendelee kumiliki silaha hizo, ikiwemo vifo na ulemavu.
Kutokana na umuhimu huo, Kamishna Athumani alisema ndio maana uhakiki huo wa silaha sasa unafanyika nchi nzima badala ya Mkoa wa Dar es Salaam pekee, kama ilivyokuwa hapo awali.
Alikumbusha wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa wanaweza kuhakiki silaha zao katika vituo vya Oysterbay Polisi kwa Wilaya ya Kinondoni, Temeke Chang’ombe Polisi na Ilala Kituo Kikuu cha Polisi, ambako wanatakiwa kwenda na kitabu (firearm licence book), picha ndogo nne za mhusika, pamoja na anwani sahihi ya mahali anapoishi mhusika.
Amesisitiza kwa viongozi mbalimbali na wananchi wanaomiliki silaha, wajitokeze kufanya uhakiki wa silaha zao na kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wanaweza kuonana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Kwa wakazi wa mikoani wametakiwa waonane na makamanda wa Polisi wa mikoa yao kwa ajili ya kupewa msaada na maelekezo zaidi ya taratibu za kufuata ili wafanye uhakiki wa silaha zao.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!