UKEKETAJI wanawake ni moja ya tatizo sugu lililopo kwenye jamii.
Baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali wanaunga mkono ukeketaji wakidai ni jambo muhimu katika maisha ya mwanamke kama sehemu ya utamaduni wao. Ni tukio ambalo, kunapokuwa hakuna mkono wa sheria, katika baadhi ya maeneo huwa ni sherehe kubwa inayoambatana na zawadi sambamba kula, kunywa na kucheza. Wakeketaji hulifananisha tukio hilo sawa na wanaume ambao hupelekwa jandoni.
Ili likubalike zaidi, baadhi ya makabila, kama Wakurya kwa mfano, wanalinasibisha na madhara au mikosi kwa wale wasiofanyiwa. Imekuwa ikidaiwa, kwa mfano kwamba, mwanamke asipokeketwa husababisha mikosi na hata kizazi chake huandamwa na mikosi, jambo ambalo si kweli lakini wanajamii husika huaminishwa hivyo.
Ukeketaji pia umekuwa ukichukuliwa kama ishara ya kupevuka kwa msichana na kwamba sasa mwanamke anaweza kuolewa na kuleta heshima katika familia, na jamii inaamini kuwa mwanamke asiyekeketwa huwa na uchafu hivyo kitendo cha kukeketwa humweka safi na maridadi. Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya afya wanasema tendo la ukeketaji hutishia maisha ya wanawake kwani ni sehemu ya mfululizo wa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yenye madhara lukuki.
Pamoja na Serikali kupiga marufuku vitendo hivyo, katika baadhi ya maeneo nchini, ukeketaji huendelea kufanyika kwa siri kubwa kwa kuhusisha wanafamilia kwa lengo la kudumisha mila na desturi. Vitendo hivyo havina faida yoyote ya kiafya kwa mwanamke bali vina madhara makubwa vikihusisha uondoaji na kuharibu tezi muhimu katika mfumo wa uzazi. Mwanamke baada ya kukeketwa, hupata maumivu makali, homa, mshtuko, uvujaji wa damu.
Upo uwezekano mkubwa wa mwanamke aliyefanyiwa kitendo hicho kupata ugonjwa wa pepopunda na kufunga njia ya mkojo. Tafiti mbalimbali za kitaalamu zimebaini kuwa, mwanamke aliyekeketwa hukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa pamoja na kupata madhara ya muda mrefu. Madhara hayo ni pamoja na ugumba (kutopata mimba) pamoja na uvimbe kwenye kibofu.
Sababu kubwa inayochangia vitendo hivyo viendelee kufanyika kwa siri ni jamii kukosa elimu inayohusu ukeketaji na madhara yake. Utafiti uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika wilaya ya Kondoa na Chemba umebaini kuwapo ongezeko la upasuaji kwa wanawake wajawazito unachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukeketaji.
Msimamizi wa wadi ya akinamama, Furaha Mhagama anasema wajawazito 48 kati ya 148 waliofikishwa hospitalini hapo kujifungua kati ya Novemba hadi Desemba mwaka 2014, walikuwa wamekeketwa huku 19 wakiwa wamefanyiwa upasuaji. Mhagama anasema kati ya Januari hadi Oktoba mwaka 2015, wajawazito 296 kati ya wajawazito 741 waliochini wa miaka 20 waliofikishwa hospitalini hapo walikuwa wamekeketwa na wajawazito 166 walifanyiwa upasuaji.
Mhagama anasema wamekuwa na kazi kubwa ya kuwasaidia wanawake waliokeketwa ili wajifungue salama ukilinganisha na mjamzito ambaye hajafanyiwa ukeketaji. “Tunatakiwa tunapowasaidia wakati wa kujifungua, tuwe nao karibu, tuwasaidie, kwa kinyume chake mtu huyo anaweza kuchanika vibaya, na ukumbuke kuwa kitaalamu haturuhusiwi kusaidia kuwaongeza njia,” anasema Mhagama.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kondoa inayohudumia pia wagonjwa kutoka wilaya ya Chemba, Reginald Saria anasema kumekuwa na ongezeko la upasuaji unaochangiwa na wanawake wengi kukeketwa. “ Unapomkeketa mwanamke, eneo lile linakuwa kovu baada ya kupona, hivyo hupoteza sifa ya maumbile ambayo yanatakiwa kuwa na uwezo wa kutanuka anapojifungua. Kimsingi ukeketaji ni chanzo cha wanawake kupata uzazi pingamizi,” Anasema Saria.
Saria anasema badala ya eneo hilo kutanuka, mwanamke anaishia kuchanika vibaya, kuzimia, kupata maambukizi (infection) na kuambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU), maumivu makali, kidonda kutopona mapema, kuchelewa kujifungua na kifo kutokana na kuvuja damu nyingi. “Nidhahiri kuwa uponaji wa kovu la ukeketaji sio mzuri, pia wakati wa kujifungua mtoto anachelewa kutoka. Na tatizo kama hili linakuwa kubwa endapo mama kajifungulia nyumbani kwani anaweza kupoteza maisha kwani eneo lililokeketwa linashindwa kutanuka,” Saria anaeleza.
Anataja madhara mengine ni kuota nyama sehemu za siri baada kupona vizuri, kuziba kwa mirija ya uzazi suala linaloathiri afya ya uzazi kwa wanawake na uwezekano wa mwanamke kupatwa na fistula. Muuguzi Mkuu, Sister Komu anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa wanawake wanapokwenda kliniki kuwa wao ndio wanapata shida kubwa kutokana na ukeketaji.
Pia wamekuwa wakiwataka wanawake hao ambao wamepitia madhira ya ukeketaji kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kupinga ukatili huo na kutowafanya wasiwafanyie hivyo wale watoto wakike wanaowazaa. “Elimu tunaitoa kwa kumueleza kuwa matatizo yaliyokupata yanaweza kumpata binti yako wewe kama mama na umepitia madhira haya hivyo uwe mstari wa mbele kupinga ukeketaji. Kufundisha ni jambo moja na utekelezaji ni jambo jingine”, anasema Komu.
Anaendelea kusema, “ Tatizo kubwa akinamama wa makabila haya tunayowahudumia ni wasiri sana, hawataki kabisa kuzungumzia suala hilo sasa inakuwa vigumu kama wanakwenda kutekeleza au la.” Utafiti uliofanywa wilayani Tarime na waandishi wa habari mwaka 2010 ulionesha pia kwamba ndoa za wanawake waliokeketwa zimeanza kuwa mashakani kutokana na wanaume kupendelea vimada wasiokeketwa.
Katika eneo la Nyamongo ambako kuna muingiliano mkubwa siku hizi kutokana na uwepo wa mgodi unaosababisha ujio wa wanawake wafanyabiashara wasiokeketwa, waandishi waliambia kwamba wanawake hao wamekuwa sababu ya wanaume wengi kutelekeza ndoa zao. Mwanaidi Hamis mkazi wa kijiji na Munguri wilayani Kondoa anasema wajibu wa Serikali kutoa elimu hiyo kwa jamii na kusimamia ipasavyo sheria zinazokataza vitendo hivyo kwa kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua.
Suala la ukeketaji wanawake ni mtazamo potofu ambao awali ulikuwepo kwenye jamii nyingi za Kiafrika ambazo hivi sasa Serikali za nchi hizo zinajaribu kuwaelimisha ili waachane na utamaduni huo ambao umepitwa na wakati. Naye Mwanahamisi Ngede kutoka kijiji cha Kidoka wilayani Chemba anapendekeza Serikali isinyamaze kimya ikidhani wafugaji wameacha ukeketaji.
Elimu iendelee kutolewa kwa wanaume sio wanawake, kwani wanaume wengi hawahudhurii kliniki, hivyo wafuatwe kwenye maboma yao. “Tutafute mbinu ya kuwafanya atakayekutwa na hali hiyo asipewe dawa au matibabu. Nafikiri itasaidia kupunguza tatizo hilo kwa wengine kwani watakuwa na hofu,” anasema Ngede. Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalopiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia na watoto (AFNET), Sara Mwaga anasema taasisi yake imekuwa ikifanya kampeni hasa katika kupunguza ukatili wa kijinsia, ikiwamo ukeketaji.
Mwaga anasema utafiti uliofanywa katika wilaya za Dodoma mwaka 1999, zilikuwa na kiwango cha kati ya asilimia 97 hadi 99 isipokuwa Dodoma mjini ambayo kiwango ilikuwa chini kidogo kutokana na mwingiliano wa makabila mbalimbali. Anaeleza kuwa kwa sasa jamii imekuwa na uelewa kidogo jambo ambalo limefanya hata mangariba kuacha kazi hiyo, lakini jambo ambalo ni gumu ni kuwa baadhi yao bado wameshikilia na kuiamini mila hii potofu jambo ambalo linafanywa wakekete wasichana kwa siri sana.
No comments:
Post a Comment