SERIKALI imetangaza kuyafutia usajili mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) 109 kwa kuendesha shughuli zao kinyume cha sheria, kikiwamo Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA).
Pia imo Pangoline Elite Sports Foundation inayomilikiwa na Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa, Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA) na Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA).
Kwa mujibu wa Msajili wa NGOs katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, M.S. Katemba, uamuzi huo unaanza leo Machi 30, 2016. Katemba alisema usajili huo umefutwa kwa sababu ya mashirika hayo kwa kuendesha shughuli zao kinyume cha Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002, ambayo imerekebishwa mwaka 2005.
Alisema mashirika hayo ni yale ambayo hayajawasilisha taarifa za mwaka kwa kipindi cha miaka miwili pasipo kutoa sababu za msingi, kutolipa ada ya mwaka au kuendesha shughuli za NGOs bila kusajiliwa chini ya Sheria ya NGOs.
“Kwa taarifa hii, mashirika yaliyotajwa hapa chini yamefutiwa usajili na yataarifiwa kusitisha shughuli zao kuanzia tarehe ya tangazo hili (30/03/2016). Baada ya kipindi hicho, Msajili wa NGOs atayachukulia hatua stahiki mashirika ambayo yatakaidi amri hii na kuendelea na shughuli za NGOs kinyume na sheria husika,” alieleza Msajili huyo
No comments:
Post a Comment