Sunday 27 March 2016

Nguzo kuu ya kunusuru majeruhi wa barabarani, sasa imebaki hoi


Wiki iliyopita mjini hapa, kulikuwapo mjadala mkubwa kuhusiana na hali ya huduma katika Hospitali Teule ya Rufani Tumbi ya mkoa wa Pwani, iliyopo mjini hapa.
 
Ingawaje kuna mengi yanayohusiana na mapungufu ya huduma hospitalini Tumbi, lakini walakini uliotawala wiki iliyopita, ulihusu hali mbaya ya majokofu ya kuhifadhi maiti.
 
Siku chache baada ya mamlaka za juu za serikali, akiwemo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangwala kufika mahali hapo kukagua hali halisi ya majokofu hayo, maamuzi mazito yalichukuliwa.
 
Mojawapo ilikuwa ni kufunga huduma za kuhifadhi maiti hospitalini hapo, hadi siku chache zilizopita zilipofunguliwa kutokana hatua ya dharura iliyochukuliwa kunusuru hali.
 
Kabla ya kufungwa kwa huduma hiyo mihimu ya kuhifadhi maiti, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ulusubisye Cyprian, alizuru mahali hapo kukagua hali mbaya iliyopo.
 
Naibu Katibu Mkuu huyo aliushauri uongozi wa hospitali kufanya mazungumzo na Bohari Kuu ya Madawa (MSD), kuangalia uwezekano wa kununua majokofu mapya.
 
Katika mtazamo wa jumla, bado iko bayana kwamba Hospitali Teule ya Rufani Tumbi, iko katika orodha ya hospitali zinazotegemewa sana nchini, kutokana na umuhimu  katika kuhudumia umma wa Watanzania.
 
Sifa pekee inayoifikia hospitali hiyo, ni huduma ya dharura inayotoa kwa majeruhi wa ajali zinazotokea mara kwa mara katika barabara kuu ya Morogoro, inayopita jirani na mahali hapo.
 
Hospitali hiyo iliyojengwa na Shirika la Elimu Kibaha mwaka 1967, ilianza kama kituo cha afya kikiwa na vitanda 35.
 
Baadaye mwaka 1979 ikiwa ni miaka 12 baadaye, ilipandishwa hadhi na kuwa Hosptali Teule ya Wilaya ya Kibaha.
 
Hatua nyingine ilichukuliwa baada ya maboresho, mwaka 1996 hospitali hiyo ilipandishwa hadhi ikiitwa Hospitali Maalumu ya Tumbi na mwaka 2011, ikawa Hosptali ya Tumbi, katika hadhi ya hosptali ya rufani ya mkoa wa Pwani.
 
Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba, ambaye taasisi yake inamiliki hospitali hiyo anasema kuwa, licha ya hosptali kupanda hadhi, bado miundombinu yake ni ya kizamani.
 
Mpemba anasema hakuna kilichobadilika, ingawa hospitali hiyo inafanya kazi katika hadhi ya hosptali ya rufani ya mkoa.
Analalamika kuwa uendeshaji wa hospitali  hiyo unagubikwa na matatizo lukuki, ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba, dawa, vifaa tiba, mashine mbalimbali za kumuhudumia   majeruhi wa ajali. 
 
“Hospitali hii ilianzishwa miaka takribani 50 ikiwa na idadi ya vitanda 35 hadi leo, inaendelea kutoa huduma kwa kutumia miundo mbinu ya zamani na rasilimali chache pamoja na kuwa idadi ya vitanda katika hospitali imeongezeka kutoka vitanda 35 mwaka 1967 na kufikia vitanda281,” anasema.
 
Mpemba anasema kuwa, wakati zinahitajika zaidi ya Sh. milioni 160 kwa mwezi kukidhi mahitaji ya dawa na vitendea kazi vingine, mapato ya hospitali ni robo ya kiwango hicho, kwa maana ya kiasi cha Sh. Milioni 40.
 
Analalamika kwamba, katika uhalisia wa mahitaji ya bajeti fedha hizo hazitoshi hata mahitaji ya walau idara moja.
 
MGANGA MKUU 
Mganga Mkuu wa hosptali hiyo, Dk.  Peter Dattani, anakiri hospitali yake kukabiliwa na ukata mkubwa hata inashindwa kuwalipa wafanyakazi malipo ya muda wa ziada, likizo na sare za kazi.
 
Mengine anayosema wanakwama, ni uwezo wa kununua vitendea kazi na mahitaji ya kitabibu, kama vile kwenye chumba cha upasuaji, ambako hakuna dawa za dharura wala sare za kufanyia kazi  na miundombinu yake imechakaa.
 
Lingine analoongeza ni upungufu wa wauguzi na madaktari, huku vyoo vilivyopo havikidhi mahitaji na ndiyo hali inayotawala hadi kwenye mapokezi, ambako hakimudu idadi ya wagonjwa kwa siku wanaofia 500.
 
“Kwa ujumla hospitali hii inatakiwa upanuzi na kuboreshwa miundombu yake. Kwa sasa tunafanya kazi katika mazingira magumu sana,” anasema Dk. Dattani.
 
Anaongeza:”Majengo yamekaa mbali kati ya jengo moja na jingine. Kwa hiyo, hata utendaji wake umekuwa mgumu, ingawa serikali imeshatenga bajeti kwa ajili ya upanuzi. Ni heri ingeharakishwa kutokana na umuhimu wake.”
 
Meneja Huduma za Afya, Bryson Kiwelu, anasema baadhi ya changamoto zinazoikabili hosptali hiyo, ni kukosekana lifti ya kupandisha na kushusha wagonjwa ghorofani, pia jukumu la kushusha maiti kwa ajili ya kupelekwa katika chumba cha kuzihifadhi.
 
Anasema katika mazingira hayo ni kwamba wafanyakazi wanalazimika kuwabeba ama wagonjwa au maiti kwa mikono na wakati mwingine, ndugu wa wagonjwa huwabeba mgongoni.
 
“Ni kazi ngumu sana, lakini tutafanyeje? Hata majengo nayo yamekaa mbalimbali. Hii nayo ni changamoto kubwa, hata uwe na wafanyakazi wengi, lakini kutokana na miundombinu ilivyo, ni kazi sana!
 
“Mara kadhaa kadhaa wauguzi wetu wamekuwa wakisumbuliwa na maumivu ya mgongo na hii imesababishwa na kubeba wagonjwa wazito, kuwapandisha ghorofani,” anasema Kiwelu.
 
Anaongeza kuwa upungufu wa mashuka nao ni changamoto nyingine, kwani kuna vitanda 281 vinavyotumia mashuka matatu katika kila kitanda.
 
Kupitia wastani huo, Kiwelu anasema kuna upungufu wa mashuka matano kwa kila kitanda na mashuka hayo yameshachakaa ndani ya miezi mitatu, kutokana na kufuliwa mara kwa mara.
 
“Utaona ni kwa jinsi gani tunavyofanya kazi katika mazingira magumu,” anasema Dk. Kiwelu katika hisia za kulalamika.
 
WAUGUZI WANASTAAFU
Pia anasema idadi kubwa ya wauguzi wanakaribia kustaafu, jambo linaloiweka hospitali katika mazingira magumu, hivyo huenda hospitali hiyo ikakosa wataalamu hao waliajiriwa katika kipindi kimoja na kipindi cha kustaafu kwao kinafanana.
 
Pia anasema chumba cha maiti katika hospitali hiyo ni finyu na hakiwezi kuhudumia idadi kubwa ya maiti na kuwa hata miundo mbinu ya chumba hicho haiendani na hali ya sasa.
 
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, anasema changamoto zilizotajwa zimeshusha kiwango cha utendaji na morali wa kazi kwa wauguzi wengi.
 
“Ukosefu wa dawa ni changamoto kubwa, ukimwambia mgonjwa hakuna dawa hakuelewi, wakati mwingine inafikia hata tunatukanwa kuwa tunaficha dawa. 
 
“Hii inashusha hamasa ya kufanya kazi, wananchi bado hawana uelewa kumbe tatizo haliko kwetu ni la serikali,” anasema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!