Zaidi ya watumishi hewa 1,850 wamebainika katika idara na taasisi za serikali kwenye mikoa mbalimbali nchini ambao wameisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 3.56.
Taarifa iliyowasilishwa jana jijini Dar es Salaam kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, wafanyakazi hewa waliobainika hadi sasa ni 1,855 ambao taarifa za awali zinaonyesha kuwa katika nyakati tofauti wamelipwa Sh. 3,562,670,000.
Katika taarifa hiyo, mikoa ya Mwanza, Arusha na Singida imeelezwa kuongoza kuwa na idadi kubwa ya watumishi hao hewa. Mkoa wa Mwanza ni kinara kwa kuwa na watumishi hewa 334, Arusha 270 na Singida 202.
Kwa mujibu wa wakuu wa mikoa yote nchini, watumishi waliobainika kuwa ni hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara ni walimu na madaktari ambao ni marehemu na wastaafu.
Utambuzi wa umefanyika kutokana na agizo la Rais Dk. John Magufuli, alilolitoa wakati wa kuwaapisha Wakuu wa Mkoa, Machi 15, mwaka huu, kwamba pamoja na mambo mengine, wahakikishe wanashughulikia tatizo la watumishi hewa, ambalo limekuwa likiigharimu serikali mamilioni ya fedha za walipakodi.
Rais Magufuli aliwapa wiki mbili wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanafanya kazi hiyo na kukabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Simbachawene kabla ya kupelekwa Utumishi na hatimaye kumfikia yeye mwenyewe.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema watumishi hewa 334 walibainika kwenye mkoa huo, hususan katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, ambalo lina watumishi hewa 72.
Katika mkoa wa Arusha watumishi hewa 270 walibainika katika kipindi cha wiki mbili na kusababisha upotevu wa Sh. bilioni 1.188 kwa mwezi Machi pekee.
Katika mkoa wa Singida, watumishi hewa 202 walibainika na mkoa wa Kigoma wenye watumishi hewa 171 ambao wamesababisha hasara ya Sh. milioni 114.6 kwa mwezi.
Mikoa mingine ni Kilimanjaro wenye watumishi hewa 111 ambao walilipwa Sh. milioni 281.4 kwa mwezi mmoja na Dodoma watumishi hewa 101 waliolipwa Sh. milioni 297 kwa muda wa miezi sita.
katika mkoa wa Morogoro watumishi hewa waliobainika ni 122, ambao walilipwa Sh. milioni 450.79 kwa mwezi Machi pekee huku mkoa wa Mara ukiwa na watumishi hewa 94 waliolipwa walilipwa Sh. milioni 121.1 kwa mwezi mmoja.
Mkoa wa Mbeya ambao umeungana na mkoa mpya wa Songwe ulibainika kuwa na watumishi hewa 98 ambao walilipwa mishahara ya Sh. milioni 459.6.
Katika jiji la Dar es Salaam watumishi hewa waliobainika ni 73 ambao wamelipwa Sh. milioni 379 kwa mwezi mmoja.
Mikoa mingine na idadi kwenye mabano ni Pwani (150), Ruvuma (37) waliolipwa Sh. milioni 58. 4, Njombe (34) walilipwa Sh. milioni 20.107 na Rukwa (180 waliolipwa Sh. milioni 55.64.
Mingine ni Simiyu (33) ambao walilipwa Sh. milioni 320.993, Tabora (48) walilipwa Sh. milioni 118, Tanga (24) na Lindi (57) waliolipwa Sh. milioni 36, Katavi (21) walilipwa Sh. milioni 120 kwa miezi sita, Kagera (14) ambao walilipwa Sh. milioni 49. 147 kwa mwezi, Geita (wanane) na Manyara watano.
Aidha, mkoa wa Shinyanga haukubainika kuwa na watumishi hewa kutokana na malengo waliyokuwa wamejiwekea tangu mwaka 2014, ikiwamo kukagua idadi ya watumishi walioko kazini na wanaotakiwa kulipwa mishahara kila mwezi.
Pia katika ripoti hizo walibainika watumishi watoro ambao walikuwa wakiendelea kulipwa mishahara licha ya kutokuwepo kazini kwa muda mrefu.
Katika mkoa wa Dodoma watumishi watoro 38 walibainika, Iringa 145 na Kagera 248 ambao pia wanaendelea kuchunguzwa.
Mkoa mingine yenye watumishi watoro na idadi yao kwenye mabano ni Manyara (50), Mtwara (285), Mwanza (205), Pwani (50), Rukwa (139), Simiyu (62), Singida (29) na Tanga (502).
Watumishi hao watoro ni wale walioacha kazi lakini wamekuwa wakiendelea kulipwa mishahara na wengine walio kwenye matatizo ya kiutumishi.
Akizungumza na wakuu hao wa mikoa baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Simbachawene aliwataka kuhakikisha wanawachukulia hatua za kinidhamu watumishi hao waliohusika kulipa na kupokea mishahara hewa.
“Wakuu wa mikoa mna polisi, magereza na mgambo. Hakikisheni hao watu mnawakamata kwa makosa waliyobainika nayo na hatua stahiki zichukuliwe,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Wananchi wanataka kusikia hawa waliokuwa wanaiibia serikali wamechukuliwa hatua gani, baada ya kutangazwa badala ya kuishia kuwatangaza kuwa ni watumishi hewa na wanalipwa mishahara” .
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment