Wednesday, 23 March 2016

MLEMAVU ASIMULIA TAABU ZA MAISHA


YAKOBO Hyera ni kijana anayeishi mtaa wa Misheni, Kata ya Masumini, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. Kijana huyo amezungumza na mwandishi wa makala haya, na kusimulia adha zinazomkabili. Yakobo anaishi na bibi yake Bonita Ndunguru (74), mama yake mkubwa Analice Hyera (54), binamu yake Elifina Hyera (22) na wadogo zake Focus Hyera (29) na Eric Ndomba (21).


Mwandishi: Labda uanze kwa kutueleza kwa kifupi historia ya maisha yako. Yakobo: Nina umri wa miaka 31. Nilisoma Shule ya Msingi Kitanda, kuanzia mwaka 1985 mpaka 1989, baadaye nilijiunga na Shule ya Msingi Huruma kuanzia darasa na nne. Nilifaulu darasa la saba mwaka 2003, na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Makita mwaka 2004 nikiwa nachukua mchepuo wa sayansi. Nilihitimu kidato cha nne mwaka 2009.
Mwandishi: Wewe ulizaliwa ukiwa mlemavu au uliupatia ukubwani. Na Je, kuna changamoto zozote unazipata kutokana na ulemavu wako? Yakobo: Mimi sikuzaliwa na ulemavu. Nilipata ulemavu huu nikiwa na miaka tisa, wakati huo nikiwa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Kitanda. Kabla ya kuwa hivi nilikuwa nacheza kama wenzangu bila shida yoyote. Siku moja asubuhi, wakati nikielekea shuleni ghafla nilihisi mwili ukiwasha nikaanza kujikuna huku nikiishiwa nguvu.
Nikaanguka chini nikapoteza fahamu. Nilipozinduka wiki mbili baadaye nilijikuta nikiwa katika Hospitali ya Mbuyula hapa Mbinga. Walionishuhudia siku ile waliniambia kuwa nilipoanguka nilikuwa natetemeka kama mtu mwenye kifafa au degedege. Kwa kipindi chote hicho sikuweza kuongea hata neno moja. Nilipozinduka nilianza kujifunza kuongea kwa shida k a - ma mtoto kwa kwa sababu upande mmoja ulikuwa umepoteza mawasiliano, na mdomo kwenda upande kidogo.
Kuanzia hapo nilijihisi mtoto nisiye na bahati, ulemavu wangu ulikua kadiri nilivyokuwa nakua, jambo lililonisononesha sana hasa ukizingatia mpaka nafikia umri huo nilikuwa sikuwahi kumjua baba yangu mzazi kwa sababu naambiwa mama yangu mzazi alifariki dunia wiki mbili tu baada ya mimi kuzaliwa. Wakati natembea kwa fimbo kwenda shuleni na wenzangu huku nikijivuta kwa shida na misuli ikiwa inakaza, siku moja mwaka 1994 nilikutana na mtawa w a k i k e wa kizungu, sista Gabriela, kwa sasa ni marehemu.
Aliwasiliana na wamisionari wa Shirika la Mapadre wa Vincentiani huko Ulaya, wakanipatia baiskeli ya magurudumu matatu ninayotembelea mpaka sasa. Msaada huo ulinipa faraja nikaaza kupunguza machungu ya kutokuwa na baba na mama. Sista Gabriela alinihamisha shule niliyokuwa nasoma na kunipeleka katika Shule ya Msingi Huruma ya Mbinga mjini aliyokuwa anaiendesha yeye mwenyewe kwa wakati huo.
Shule hii ya Huruma, ilikuwa nzuri zaidi kwangu kuliko ile ya mwanzo kwa sababu ilikuwa na vifaa maalumu kwa walemavu kujifunzia na huko nilikutana na walemavu wenzangu tukawa tunapeana moyo. Darasani kwetu tulikuwa na bidii ya kusoma kiasi kwamba walifeli wanafunzi wawili tu wengine walichaguliwa kuingia sekondari na mimi nikiwa miongoni mwao. Nikapangiwa Shule ya Sekondari ya Makita ya Mbinga Mjini.
Lakini mazingira ya hii shule ikiwa ni pamoja na miundombinu ilikuwa kikwazo sana kwangu. Mpaka nilijikuta nazunguka na barabara kuomba mitaani kwa sababu kwa akili nilizokuwanazo mazingira ndiyo yaliyonikwamisha. Kuanzia mlango wa darasa lenyewe ulikuwa mdogo, nilitakiwa kuiacha baiskeli nje ili niingie darasani bila baiskeli yangu; isitoshe dawati nililokuwa nakalia ni sawa na wenzangu ambao siyo walemavu.
Kumbuka katika masomo ya sekondari unaandikia madaftari makubwa na unatakiwa kuandika haraka mwalimu anafuta na kuandika tena. Kutokana na misuli na miguu, mikono na shingo kukaza kila mara nilikuwa nashindwa kwenda na kasi ya kuandika wakati mwingine wanafunzi wenzangu walikuwa wananionea huruma na kuniandikia lakini nao walichoka, wakashindwa kunisaidia kila siku.
Kutokana kutokuwa na kasi ya kuandika darasani nilijikuta nabaki kidato cha kwanza kwa miaka miwili. Gharama zote za shuleni nilikuwa nalipiwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. Nilihitimu kidato cha nne mwaka 2009. Kwa kweli sikufaulu vizuri kwa kuwa nilipata daraja la nne alama 34. Mwandishi: Nani anakusaidia na kwa kiasi gani unadhani afya yako inaimarika?
Yakobo: Wapo watu wengi ambao wamekuwa wananisaidia kuanzia hapo ikiwa ni pamoja na kunifanyisha mazoezi, kunipa dawa na kuchua misuli na wakati mwingine napelekwa hospitali mbalimbali lakini, nafuu inajitokeza kidogo kwa mbali kwa muda baadaye hali inarudia karibu na ilivyokuwa awali. Mwandishi: Hospitali gani ambazo ulipelekwa, na pengine vipimo vya madaktari vilibaini nini.
Yakobo: Ni pamoja na Mbuyula, Litembo na Peramiho. Tatizo ni kwamba wakati mwingine unakuta gharama za vipimo zinakuwa juu na kutokana na kutokuwa na mtu wa kunisaidia kwa maana ya baba wala mama inakuwa ngumu kumudu gharama. Mimi ninaishi na bibi yangu ambaye naye ni mzee wa miaka 74 anayehitaji msaada kama mimi. Mara nyingi tunabaki tunaangaliana na kujirudia nyumbani kumuomba Mungu tu basi.
Mwandishi: Kwani, tuseme kwa mujibu wa madaktari unasumbuliwa na nini hasa? Yakobo: Misuli ya shingo, mikono, miguu na uti wa mgongo ni mitihani yangu ya maisha ambayo ni mzigo wa kunielemea kwa siku nyingi na sijui kama kuna siku nitaondokana nayo. Mwandishi: Kwani imeshindikana kupata tiba ya uhakika? Yakobo: Tatizo limekuwa ni gharama za tiba na afya ndiko tatizo langu la kudumu.
Pamoja na kwamba ninapitia shida nyingi mpaka mlo wa siku unakuwa taabu, lakini naona nikishughulikia afya yangu kwanza hayo mengine yatakaa vizuri kwani nitaweza kujishughulisha na vijikazi nitakavyovimudu vitakavyoniwezesha kuishi. Mwandishi: Ni kwa namna gani jamii inayokuzunguka wakiwemo ndugu zako wa karibu wanavyokusaidia ili na wao waunge mkono juhudi hizo kama zipo.
Yakobo: Ukiachilia mbali kufiwa na mama nikiwa mdogo, na kutokumfahamu baba yangu mzazi, bibi ninayeishi naye, ambaye na yeye aliachwa na babu miaka mingi mama yangu akiwa mdogo mambo haya yalisababisha tuwe familia iliyojitenga kiasi kwamba ndugu wasingeona sababu ya kututafuta kwa sababu kuu mbili; Kwanza, bibi alikuwa haelewani na babu kwa muda mrefu na hivyo babu alihamia kwa mke mdogo mbali na nyumbani na hivyo kumwachia familia.
Pili, marehemu mama yangu alizaa watoto watatu na kila mtoto na baba yake na kwa bahati mbaya mpaka anafariki alikuwa hajamtambulisha hata mwanaume mmoja nyumbani, jambo lililosababisha familia yetu ionekane ya ajabu kidogo. Kwa muda mrefu nimekuwa natembea na kibali nilichopewa na Mkuu wa Wilaya kuomba msaada madukani lakini naambulia kwa watu wachache shilingi kati ya 100 na 500.
Mwandishi: Unayazungumziaje maisha ya kila siku kwa ujumla hapa nyumbani. Yakobo: Nina mdogo wangu anafanya kazi gereji, kuna siku anarudi na chochote na kwa sababu bibi naye ni mkulima vinafaka vidogo vinatusaidia na vimichango vidogo vya wasamaria tunasogeza siku ziende ila siku tunashinda au kulala njaa kwetu ni jambo la kawaida.
Kwa mfano leo mchana sijala kitu, nilimwita binamu yangu anayepika hapa nyumbani kumuuliza kuhusu ugali akaniambia unga ulibakia kidogo na kama angepika mchana, basi tusingekula usiku kwa hiyo aliuacha kwa ajili ya kupikia usiku.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!