Meli tatu za kivita kutoka nchi za Afrika kusini, China na Pakistan zimetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam.
Meli hizo zimesheheni wanajeshi na silaha za kivita ambao watashirikiana na wa vikosi vya majini vya Tanzania kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Akizungumza wakati wa kuipokea meli kutoka Afrika Kusini, Mkuu wa Kikosi cha Majivita, Brigedia Jenerali Richard Mutayoba alisema juzi kuwa ujio huo unalenga kubadilishana mbinu za kukabiliana na uharamia majini.
Alisema Tanzania ikiwa mojawapo ya nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi imeingia makubaliano ya kushirikiana katika vita dhidi ya uharamia na kuhakikisha maji yake yanakuwa salama.
“Tuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa kwani uchumi wa majini umeongezeka na kustahili ulinzi mkubwa,”alisema Brigedia Jenerali Mutayoba
Alisema katika siku ambazo meli hizo zitakuwa nchini, askari wa Tanzania watapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali.
Kiongozi wa meli ya Afrika Kusini, Kapteni Michael Boucher alisema ziara hiyo ni sehemu ya mikakati ya nchi yake kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingine.
“Lengo ni kujenga uhusiano na mataifa mengine, tumezunguka nchi kadhaa kabla ya kufika Tanzania ambako tunategemea tutafanya mafunzo ya pamoja na vikosi vya wanamaji,” alisema Boucher.
Boucher alisema meli hiyo ina wanajeshi 189 kati yao, 39 ni wanawake na inatarajiwa kung’oa nanga kesho.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment