Polisi wakiwa kwenye eneo la tukio.
MOROGORO: Dereva wa teksi Omari Selemani Mwanamtwa anayeegesha gari lake stendi ya mabasi ya mikoani ya Msamvu, Morogoro na abiria wake ambaye ni mlemavu, wanahisiwa kufanyiwa mauaji wa kutisha baada ya gari walilokuwa wakitumia kukutwa limetelekezwa, Risasi Mchanganyiko lina taarifa zaidi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Machi 7, mwaka huu ambapo Machi 8 gari hilo lilikutwa katika eneo la kituo cha mafuta kilichopo kandokando ya barabara ya lringa kwenye mzunguko wa Msamvu, ikiwa imetelekezwa huku eneo la mbele ya gari hilo likiwa limetapakaa damu na baiskeli inayodhaniwa kuwa ni ya mlemavu huyo ikiwa ndani ya boneti.
Baada ya wananchi wakiwemo madereva wa teksi wa Msamvu kuliona gari hilo, walitoa taarifa polisi ambao walifika eneo hilo kuikagua kabla ya kuondoka nayo kuelekea kituo kikuu cha polisi kwa upelelezi zaidi.
Awali, ilidaiwa kuwa dereva huyo alikodiwa na mteja wake wa siku zote ambaye ni mlemavu na kuwa kutokea hapo, walielekea benki (jina/tawi linahifadhiwa) ambako walitoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hata hivyo haikujulikana kiasi chake.
Mama wa marehemu akiwa na majonzi.
Bosi wa dereva wa teksi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mrisho Harubu, aliyedai yeye ni msimamizi wa tajiri anayeishi Dar, alisema ni kweli Omari alipakia abiria mlemavu na hakuonekana hadi gari lake lilipokutwa eneo hilo.
Nyumbani kwa dereva huyo maeneo ya Chamwino Bagdad, mkewe Asha Ally Sanga alisema kwa muda mrefu mwezi huu alikuwa mgonjwa na kwamba Jumatatu iliyopita mumewe alimuaga anaelekea kazini ili baadaye arudi kumpeleka hospitali.
Mashuhuda wakiwa kwenye eneo la tukio.
Mama mzazi wa dereva huyo Asha Omar akizungumza kwa uchungu, alisema mwanaye huyo aliyechukua jina la baba yake, alikuwa ndiye tegemeo lake kwa kila kitu.
“Ametoweka Jumamatu mpaka leo Jumapili ni siku 6 na siku zote hizo tumekuwa tukilala matanga ya wanandugu, tumepanga ikifika siku 10 hatujamuona tunaanua matanga,” alisema mama huyo na kuangua kilio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa sasa bado wanaendelea kuwatafuta watu hao.
No comments:
Post a Comment