Sunday 27 March 2016

Majambazi yaua wawili, yajeruhi saba, kupora

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus

 Watu wawili wameuawa na wengine saba kujeruhiwa kwa risasi baada ya majambazi kuvamia na kupora Sh2 milioni na vocha za simu za Sh800,000 katika duka la uwakala wa fedha kwa njia ya mtandao.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha alisema tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku huko Bugarika, Mwanza.
Aliwataja waliouawa katika tukio hilo ambao wote walikuwa wapita njia kuwa ni dereva wa bodaboda, Julius Wankaba (30) na mwingine aliyejulikana kwa jina la Mama Yuni (35).
Kamanda Kamugisha alisema majambazi hayo yalikuwa na bunduki aina ya SMG na yalikuwa yakifyatua risasi ovyo kwa nia ya kuwatishia wananchi, ambazo ndizo zilizowaua na kujeruhi wapitanjia.
Aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza kuwa ni Magessa Mungari (38) na Simon Charles (26). Wengine watano ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ni Mwita Ryoba (30), Frank William (19), Said Saumu (20), Masumbuko Kanduru (38) na Emmanuel Francis, wote wakazi wa Bugarika, Mwanza.
Katika tukio jingine, Kamanda huyo alisema kitoto kichanga cha siku moja kiliibwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu baada ya mtu asiyefahamika kuingia wodi ya wazazi na kumkuta mama wa mtoto huyo, Magdalena Petro (16), amepitiwa na usingizi.
“Kwa mujibu wa mashuhuda, kabla ya wizi huo, mwanamke aliyevaa mavazi ya kumfunika kiwiliwili na uso (baibui), alionekana akiingia eneo la hospitali; inasadikiwa ndiye aliyemvizia mama huyu mzazi na kumwibia mtoto wake alipokuwa amesinzia,” alisema Kamanda Kamugisha na kusisitiza kuwa msako mkali unaendelea kumsaka mwizi huyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!