Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku nane kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega, Hamis Yuna, kuhamia kwenye halmashauri hiyo kutokana na kuishi nyumba ya kulala wageni iliyopo wilaya jirani ya Magu.
Pia, Majaliwa ametoa siku 13 kwa watumishi wote wanaoishi Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, kuhamia wilaya hapa ifikapo Machi 15.
Akihutubia wakazi wa Kata ya Lamadi wilayani hapa jana, Majaliwa alisema hatapenda kumuona mtumishi kufanya kazi akitokea wilaya nyingine ilhali kuna nyumba nyingi za kutosha.
Alisema watumishi wanaoshindwa kuishi maeneo yao ya kazi, wanawakosesha huduma wananchi wanaotegemea.
Majaliwa alisema haiwezekani mtumishi kuishi wilaya nyingine na kufanya kazi kwingine na kwamba, muda mwingine hufunga mapema ofisi ili kuwahi usafiri.
“Nampa siku nane mkurugenzi kuhamia makao makuu ya wilaya hiyo na watumishi wote kufikia tarehe 15 wawe wamehamia hapa, mkuu wa wilaya utanijulisha kama wameshahamia ili tuje tuone aliyekataa kuhamia makao makuu ya wilaya tujue hatua za kuchukua,” alisema Majaliwa.
Tangu kuundwa kwa wilaya hiyo watumishi wengi wamekuwa wakiishi Wilaya ya Magu, kwa madai kuwa hakuna nyumba za kutosha.
“Nimetembelea na kuona makao makuu ya wilaya hii, kuna nyumba nyingi kiasi kwamba hakuna mtumishi ambaye ataweza kukosa kuishi, tukihamia hapa tutawahudumia wananchi vizuri tofauti na sasa tunafanya kazi ili kuwahi kuondoka,” alisema Majaliwa.
Majaliwa yupo kwenye ziara ya kwanza tangu Serikali ya Awamu ya Tano ichaguliwe, imeanzia Mkoa wa Simiyu baadaye anatarajiwa kwenda Mwanza, Geita na Kagera kukagua shughuli za maendeleo kutatua kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment