ARI kesho wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa marudio visiwani humo, ambao utashirikisha wagombea wa urais na wagombea wa ujumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka vyama mbalimbali.
Tayari Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) imeshakamilisha hatua za msingi za kufanyika kwa uchaguzi huo, ikiwemo kuwasili kwa karatasi za kura. Miongoni mwa vyama vilivyothibitisha kushiriki ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ADC, DP, CCK, SAU, AFP, TLP, UPDP, NRA, UMD na Demokrasia Makini.
Wakati maandalizi yakiwa katika hatua za mwisho, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM ), umesema uchaguzi wa marudio utakaofanyika kesho mjini hapa, ndiyo utakaotatua na kuhitimisha mvutano uliopo baada ya ZEC kufuta matokeo kwa mujibu wa sheria.
Umoja huo umewataka vijana pamoja na Wazanzibari kujitokeza kupiga kura, ili kutumia haki yao ya kuchagua nani awe Rais kwa mujibu wa sheria, ili kukwamua kile kinachoitwa mkwamo wa kisiasa Zanzibar.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya UVCCM, Gymkhana mjini Unguja.
Shaka alisema wale wanaosema Zanzibar kuna mgogoro au tatizo linalohitaji kupatiwa suluhu, hawajatambua kiini cha tatizo na ufumbuzi wake. Alisema kiini cha tatizo linalosababisha mivutano ya kisiasa, ni Chama cha Wananchi (CUF) kukaidi utii wa matakwa ya sheria na kutaka kupuuza Katiba ya Zanzibar.
“Zanzibar ina Katiba na sheria zake, vipi sheria na Katiba zipuuzwe ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kisiasa ambayo hayatokani na nguvu za kikatiba wala sheria za Zanzibar?” Alihoji.
Shaka ametoa mwito kwa vijana kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika upigaji kura, ili hatimaye wananchi wa Zanzibar wapate haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Maridhiano hufanyika baada ya kupita mchakato wa uchaguzi na wananchi kuamua kwa kura zao, ikiwa kuna dosari au hitilafu zozote zinaweza kuzungumzwa na viongozi husika na kufikia makubaliano au mapatano,” alisema Shaka.
Hata hivyo, aliwaeleza kuwa iwapo mtu tangu mwaka 1995 amekuwa akilalamika kuibiwa kura, hata kama atashiriki mazungumzo bado ataendelea kushikilia msimamo wake wa kujiona mshindi na hatakubali lolote.
Shaka alisema wale wote wanaosema kuwa Zanzibar kuna tatizo linalohitaji ufumbuzi, pia wanapaswa kujua kuwa Zanzibar ni nchi yenye madaraka yake ya ndani ikiongozwa kwa taratibu za Katiba, sheria na kanuni husika za kiserikali.
“Mazungumzo, majadiliano au upatanishi wa kisiasa utokanao na misuguano ya wanasiasa hauwezi kubatilisha nguvu za kikatiba au sheria za nchi husika,” alisema. Amewataka vijana kujitokeza kwa wingi kupiga kura kesho Machi 20, ili kutumia haki yao ya kimsingi na kidemokrasia huku akiwahakikishia amani na utulivu kutawala visiwani Zanzibar.
No comments:
Post a Comment