Wednesday 16 March 2016

MA- RC KUPIMWA NDANI YA SIKU 15


Rais John Magufuli, amewapa siku 15 wakuu wa mikoa wapya aliowaapisha jana, kuhakikisha wanaondoa  malipo ya wafanyakazi hewa yaliyobainika.
 
Hilo ni moja ya maagizo matano aliyowapa wakuu hao wa mikoa 25 aliowaapisha Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
 
Hata hivyo, Mkuu wa Mko wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, hakuwapo katika hafla hiyo. Hakuna sababu zilizoelezwa kwa kutokuwapo kwake.
 
WAFANYAKAZI  HEWA
Rais Magufuli aliwataka wakuu hao wa mikoa kwenda kusimamia halmashauri kwa kuwa kuna uozo mkubwa.
 
Alisema hakuna sehemu zenye uozo kama katika halmashauri.
 
Alisema serikali ilituma wataalam wake Februari, mwaka huu kwenda kufanya utafiti katika mikoa ya Singida na Dodoma kuhusu ulipaji wa mishahara Desemba na Januari na kubaini wafanyakazi 26,900 katika halmashauri 14 waliofanyiwa uhakiki,  202 wanalipwa mishahara hewa.
 
Alifafanua kuwa kati ya wafanyakazi hao hewa, baadhi wameshafariki dunia, kufungwa na wengine ni wastaafu.
 
Rais Magufuli alisema wafanyakazi zaidi ya 3,320, wakati uchunguzi huo unafanyika hawakukaguliwa kwa kuwa walikuwa na ruhusa, wengine masomoni na baadhi wagonjwa.
 
“Ninawapa siku 15 kuanzia leo, muwe mmeshakamilisha na kurekebisha tatizo hilo, kuwatoa na kuwajumlisha wafanyakazi hewa, kwa mkurugenzi atakayeshindwa kufanya hivyo, kwa mwezi ujao atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe na kupelekwa mahakamani,” alisema Magufuli.
 
"Utafiti huo ulibaini kuwa kuna watumishi walioacha kazi sita, waliokufa na kufungwa 27, waliofukuzwa wanane, wastaafu 158, waliokuwa likizo bila malipo watatu, lakini walikuwa wanalipwa mishahara," alisema Rais Magufuli.
 
Alisema katika halmashauri 180 zilizopo nchini, zina wafanyakazi hewa 5,297, na kwa makadirio ya kulipwa mshahara wa Sh. milioni moja, serikali inapoteza Sh. bilioni 2.59 kila mwezi.
 
Rais Magufuli alisema serikali ina wafanyakazi zaidi 500,000 na inalipa mishahara takriban Sh. bilioni 549, ambayo kati ya fedha hizo kuna malipo ya wafanyakazi hewa.
 
"Agizo la kuondoa wafanyakazi hewa, linatakiwa kutekelezwa hata kwenye wizara na taasisi mbalimbali nchini," alisisitiza na kuongeza:
 
"Haiwezekani Sh. bilioni 549 zitumike kulipa mishahara huku serikali ikilipa Sh. bilioni 850 madeni ya nje kama ilivyofanya Februari, mwaka huu."
 
KUWATEUA WANAJESHI MIKOA YA MIPAKANI
Rais Magufuli alisema kumekuwa na mazoea kwa mabasi ya mikoani pindi yanaposafiri kusindikizwa na polisi, akitolea mfano mikoa ya Geita, Katavi, Kigoma.
 
Alisema haiwezekani nchi kama Tanzania iliyopata uhuru miaka 50 iliyopita raia wake hadi sasa wanaposafiri wasindikizwe na polisi kwa kuhofia majambazi.
 
Alifafanua kuwa kitendo hicho kinamaanisha hakuna usalama nchini, na kwamba ameteua wakuu wa mikoa wanajeshi ambao watasimamia wananchi kwa kusafiri bila kusindikizwa na polisi.
 
“Ulinzi ukamilike, watu wakatembee katika nchi zao kwa uhuru, nitashangaa Meja Jenerali mstaafu kama Salum Kijuu, ambaye ulikuwa mahiri jeshini, ushindwe kuusimamia Mkoa wa Kagera,na watu wakakae bila amani! Nitashangaa, ninajua uwezo huo mnao,” alisema Rais Magufuli.
 
Alisema wakuu wa mikoa wanatakiwa kwenda kumaliza tatizo la ujambazi linaloitikisa nchi.
 
UPATIKANAJI WA CHAKULA
Alisema anataka katika awamu yake pasitokee mahali mkuu wa mkoa au wilaya anaomba chakula, na anakuwa wa kwanza kuwahi katika vyombo vya habari akidai chakula, wakati wakuu wa mikoa wapo, wakurugenzi wapo na wakuu wa wilaya wapo.
 
ELIMU BURE
Pia Rais Magufuli aliwapa jukumu wakuu hao wa mikoa kusimamia upatikanaji wa elimu bure.
 
Alisema kwa sasa wananchi wameitikia na kupokea elimu bure kwa kuwapeleka watoto wao shuleni.
 
Alisisitiza kuwa wakuu hao wa mikoa wanatakiwa kwenda kusimamia upatikanaji wa madawati na majengo katika shule za sekondari na msingi. 
 
Alisema alichelewa kuchagua wakuu wa mikoa kwa kuhofia uwezo wa mtu atakayemteua kuongoza mkoa husika.
 
Kadhalika, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu hao wa mikoa kusimamia vitega uchumi vilivyomo katika mikoa yao ili vijana wengi wapate ajira.
 
“Siku nyingine nilikuwa nafuta majina, siku nyingine nawarudisha niliokuwa nawafuta, siku nyingine dhambi zake unakuta ni kidogo, unaamua kusamehe. Hiyo yote ni katika kupata wakuu wa mikoa imara,” alifafanua Rais Magufuli.
 
KUMUACHA MKUU WA MKOA WA MOROGORO
Alisema alimwacha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, kwa kushindwa kusimamia vizuri migogoro ya mkoani humo iliyosababisha wananchi kuuana.
 
KUTUMIA NGUVU KAZI
Rais Magufuli alisema wakuu wa mikoa wanatakiwa kusimamia wananchi na kuhakikisha wanafanya kazi hasa vijana kwa kuwa haiwezekani kijana akawa anacheza ‘Pool Table’ saa mbili au saa tatu asubuhi halafu waliopo mashambani ni wazee na akinamama.
 
Alisema Watanzania wanatakiwa kufanya kazi na endapo wameshindwa kufanya kazi kwa kuambiwa, wafanyishwe kwa lazima.
 
“Kama vijana wamezoea kukaa kila siku na kucheza cheza bila kufanya kazi, shika, wapelekeni katika makambi wakalime kwa nguvu, akitoka huko atakuwa amejifunza,” alisema Raia Magufuli.
 
MILIONI 50 KILA KIJIJI
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakuu hao wa mikoa kusimamia vema mgawanyo wa fedha wa Sh. milioni 50 kila kijiji zitakazopelekwa kwao kwa ajili ya kuzigawa katika vijiji mara baada ya bajeti kuu kumalizika.
 
Mara baada ya kuapishwa kwa wakuu hao wa mikoa, walisaini katika hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, kazi iliyoongozwa na Kamishna wa Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda.
 
Aidha, Rais Magufuli aliwaapisha pia Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna Velentino Mlowola.

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!